Na Saleh Ally
SIMBA inaweza kuifunga AS Vita lakini kila anayehusika lazima akubali kwamba haitakuwa kazi nyepesi hata kidogo.
Kazi ni ngumu sana kwenye Uwanja wa Des Mertyrs jijini Kinshasa kwa kuwa AS Vita watakuwa wanacheza mbele ya umati wa mashabiki wao lukuki.
Simba inaweza kupambana lakini tofauti kubwa kati ya mechi watakazocheza na leo. Kitu cha kwanza ni lazima kuamini pamoja na rekodi nzuri ya kutofungwa nyumbani, bado Vita wanafungika.
Lakini hata kama ikiwezekana kuamini hivyo, basi wahusika wajue, si kazi ndogo na inahitaji uhakika sahihi bila ya kubahatisha.
Ukiangalia kabla ya Simba kufikia hatua ya makundi ilicheza mechi nne, mbili zikiwa nyumbani na nyingine ugenini.
Katika mechi za ugenini, kuna tofauti kubwa sana na hii ya leo jijini Kinshasa. Hawa ni Vita Club wenye umakini na uzoefu mkubwa wa michuano ya Caf.
Unawakumbuka Al Masry ambao waliwang’oa Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya sare ya mabao 2-2 Dar es Salaam na sare ya bila kufungana mjini Port Said, Misri? Walipotua Kinshasa walikutana na kipigo cha mabao 4-0.
Mechi dhidi ya Mbabane Swallows, uliona idadi ndogo ya mashabiki wao uwanjani. Ile ya Nkana FC, walijitokeza wengi lakini uwanja ni mdogo. Leo utaona tofauti maana mashabiki wanakuwa wengi sana na wanajua namna ya kushangilia.
Kikubwa wachezaji wa Simba wanapaswa kutojihusisha nao. Mashabiki wa AS Vita ambao wengi wao ni wakorofi na wanaamini jina vita kwao ni sahihi, wana uzoefu wa michuano ya kimataifa na hutumika kuzichanganya timu pinzani. Kwa wachezaji wa Simba, hili haliwahusu na wanapaswa kutowajali hata kama wanawasikia.
Hawa jamaa ni wazuri na Simba wanapaswa kukubali lakini kuna mambo 10 ambayo lazima wayafanye kuhakikisha inawezekana kuvuka na kupata ushindi au sare.
MAMBO 10:
1. Ni lazima Simba icheze Total Football, kushambulia na kukaba kwa pamoja kwa kuwa AS Vita hushambulia mfululizo. Hivyo, suala la kutegea, halina nafasi, viungo wawe fiti kweli.
2. Mkude, Niyonzima na Chama wanatakiwa kutumia uwezo wao kupoza mipira kwa kuwa Wakongo hao hucheza kwa kasi muda wote. Kuacha wacheze hivyo ni hatari.
3. Lazima watatumia mabeki wa pembeni kwenda kupiga krosi. Kawaida wana kasi sana, muangalie namba 3, Patou Ebunga. Hivyo, Mohamed Zimbwe na Nicholas Gyan, lazima wapande kwa tahadhari.
4. Simba wasithubutu kulinda muda mwingi bila ya kufanya mashambulizi. Waarabu Al Masry na Raja Casablanca hii iliwaponza na kuambulia vipigo vya 4-0 na 3-0. Kasi ya Okwi, Chama itumike kuwarudisha nyuma.
5. Kiungo mkabaji Glady Ngonda anayevaa namba 14 ni rasta, si wa kumpa nafasi ya kucheza muda mwingi. Simba wanapaswa kujaza kiungo kinachocheza zaidi.
6. Kiungo cha Simba kinaweza kumiliki muda mwingi mpira. Hii itawafanya Vita kuutafuta mpira zaidi badala ya kushambulia sana.
7. Simba lazima wajue, sifa ya Wakongo ni kasi na nguvu. Wajiandae kwa hili na wahakikishe wanashindana hasa kuanzia mwanzo hadi mwisho.
8. Kupoza mashambulizi ni jambo sahihi kwa Simba, aina ni hizi: Moja wamiliki mpira na kwenda nao taratibu ili kuwafanya wapaniki. Pili, kipa anaweza kutumika kutuliza kasi.
9. Vita ni wazuri kwa mashuti ya mbali. Makusu Mundele ni kati ya watu hatari. Kingine, mipira ya krosi na upigaji vichwa, Wakongo ni wepesi.
10. Suala la kupoteza mipira kama ilivyokuwa kwa Hassan Dilunga dhidi ya Nkana FC. Hili ni hatari na halipaswi kujirudia. Kupoteza mipira ni kukaribisha mashambulizi na fiziki ya Wakongo iko juu sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment