MBELGIJI SIMBA AWAFANYIA UMAFIA HUU WAARABU
Ilizoeleka katika mechi za nyumbani za Simba za Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems alikuwa akitumia mfumo wa 4-3-3 yaani akianza na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.
Mfumo huo ndiyo ulikuwa ukimwongoza kupata ushindi mnono katika mechi dhidi ya Mbabane Swallows ambapo walishinda mabao 4-1 lakini pia dhidi ya Nkana FC ya Zambia ambayo walishinda mabao 3-1.
Lakini katika mechi ya juzi dhidi ya JS Saoura iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar, Aussems aliwafanyia kitu mbaya Waarabu hao ambao waliamini kwenye mchezo huo angetumia mfumo huo wa 4-3-3 ambao tayari walikuwa wamejipanga kukabiliana nao.
Badala yake Aussems alionyesha ukomavu wa hali ya juu katika soka na akaamua kubadili mfumo na kutumia mfumo wa 4-4- 2 akianzisha mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili, lakini pia katika dakika za lala salama alibadili tena mfumo na kutumia 4-5-1 yaani mabeki wanne, viungo watano na mshambuliaji mmoja.
Hali hiyo iliwavuruga Waarabu hao na kujikuta wakipoteana kwa kiwango kikubwa katika eneo la kiungo ambalo katika mechi hiyo wakati akitumia mfumo wa 4-4-2 lilichezwa na Mghana, James Kotei, Jonas Mkude, Mzambia Claytous Chama pamoja na Hassan Dilunga.
Katika mfumo wa 4-4- 2 ambao Aussems alianza nao kwenye mechi alianza kwa kuwatumia mabaki Nicholaus Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid na Pascal Wawa, wakati washambuliaji wakiwa Emmanuel Okwi na John Bocco.
Baadaye alifanya mabadiliko kwa kumtoa Bocco na nafasi yake ikachukuliwa na Meddie Kagere, pia alimtoa Dilunga sehemu ya kiungo na kumuingiza Mzamiru Yassin.
Katika dakika za lala salama alipoamua kubadili mfumo na kutumia ule wa 4-5-1, alimtoa Okwi na kumuingiza Shiza Kichuya ambaye ni kiungo na kuifanya timu hiyo icheze ikiwa na mabeki wanne, viungo watano na mshambuliaji mmoja ambaye alikuwa ni Kagere pekee.
Akizungumza hali hiyo, Aussems alisema: “Lengo lilikuwa kupata ushindi kwa hiyo ndiyo maana nililazimika kubadili mfumo kutoka ule wa 4-3-3 kwa sababu niliamini wapinzani wetu walikuwa wameshaufanyia kazi ili waweze kutuzuia kirahisi.
“Hata hivyo niwapongeze vijana wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya na tumeweza kupata ushindi katika mechi yetu ya kwanza na sasa sisi ndiyo tunaoongoza kundi letu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment