Na Saleh Ally
MICHUANO ya SportPesa Super Cup inafanyika kwa mara ya tatu ikiwa imeanza rasmi jana kwenye Uwanja wa Taifa.
Inafanyika kwa mara ya tatu tokea ianzishwe hii ikiwa ni mara ya pili hapa nyumbani Tanzania. Kama unakumbuka wakati inaanzishwa ilifanyika jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia Nakuru nchini Kenya na sasa, hapa Tanzania.
Wakati inarudi nyumbani, inakwenda na rekodi mbovu kabisa kwa timu za Tanzania, jambo ambalo ninaamini limekuwa likiwakera mashabiki wapenda soka wa Tanzania.
Wakati yaliponzishwa kwa mara ya kwanza, pamoja na kufanyika jijini Dar es Salaam, bingwa ilikuwa ni Gor Mahia ya Kenya lakini kibaya zaidi, hata fainali, ziliingia timu mbili za Kenya.
Ilichezwa Derby ya Nairobi katika Jiji la Dar es Salaam baada ya Gor kukutana na FC Leopards.
Kulikuwa na sababu nyingi ambazo hazikuwa na msingi hata kidogo kwa timu za Tanzania kutoweka nguvu ya kutosha na ahadi ikawa pale michuano itakapohamia Kenya, basi timu za Tanzania zingelipa kisasi na kurudi na kombe nyumbani.
Kule Nakuru mambo yalikuwa yaleyale na tulichoambulia ni Simba kufika fainali na kuambulia kipigo kutoka kwa Gor iliyokuwa ikiongozwa na Meddy Kagere ambaye sasa ni mshambuliaji tegemeo wa Simba.
Bingwa anabeba dola 30,000 (zaidi ya Sh milioni 69), hii ni baada ya kucheza mechi nne tu! Pia kuna zawadi kubwa kabisa kama utazungumzia mpira wenyewe kwa maana ya taaluma hasa suala la kujifunza.
Zawadi hii ni kucheza dhidi ya Everton. Hii ni timu inayoshiriki Ligi Kuu England. Maana yake timu inapata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu inayoshiriki ligi bora zaidi.
Gor Mahia imecheza mechi mbili dhidi ya Everton baada ya kushinda kombe hilo mara mbili, yaani hapa Tanzania na kwao Kenya.
Hivi kweli, Gor ichukue kombe hili kwa mara ya tatu na moja kwa moja? Au kweli timu za Kenya zirejee na kombe hili kwa mara nyingine tena kwao? Mashindano haya iwe mwisho wa aibu.
Aibu inaweza pia isiwe kigezo pekee cha timu za Tanzania kukomaa. Lakini zionyeshe ubora na hatua mpira wetu ulipofikia kwa kuwa Kampuni ya SportPesa imeleta kitu ambacho kinapaswa kuwafanya wachezaji na viongozi wa timu za Tanzania kuona kwamba wanastahili kupata kinachotolewa.
Zawadi ya Sh milioni 69 si haba, tena baada ya kucheza mechi nne tu. Lakini nafasi ya kucheza na timu kutoka England si jambo jepesi. Kukutana na Everton kunakuwa na mengi sana ya kujifunza.
Pia tujifunze biashara maana safari hii, waandaaji wa mashindano hayo kampuni ya SportPesa wameamua hivi; kama bingwa atatokea Tanzania, Everton itakuja hapa Tanzania na kama atatokea Kenya watakwenda Kenya.
Sasa ujio wa Everton tunajua ni faida pia katika kujitangaza kwa maana ya mpira wetu lakini faida kubwa pia kulitangaza taifa.
Nguvu sahihi iwekwe, kama itakuwa Singida United, Simba, Mbao au Yanga basi kombe hilo libaki hapa nyumbani.
Njia namba moja ya kulibakiza ni kuhakikisha timu za Tanzania zinaingia fainali. Baada ya hapo, atakayechukua yeyote, faida inakuwa palepale.
Kupatikana kwake, tukumbushane itakuwa ni uwezo uwanjani na si utetezi wa visingizio kibao. Naweka msisitizo, mashabiki wa Tanzania, wamechoshwa na uonevu kutoka Kenya.
TIMU SHIRIKI
TANZANIA KENYA
Yanga Kariobangi Sharks
Simba Bandari
Singida AFC Leopards
Mbao Gor Mahia
Wewe kama mchambuzi ulipaswa uzungumzie vile vile ratiba tatanishi ya hilo bonanza la #SportPesa..
ReplyDeleteTimu za Tanzania zipo katika majukumu mbali mbali hasa ukizingatia ni katikati ya ligi kuu, FA na kuna timu ipo kwenye mashindano bora kabisa ya mabingwa wa soka Afrika.
Haya mashindano (bonanza la #SportPesa) yasiwe ya kubahatisha kama yalivyo yale ya Mapinduzi Cup...
We imajin madhara yake endapo timu moja ikapata majeruhi wa wachezaji muhimu..!!
Udhamini wa #SportPesa sawa lakini usiwe kikwazo cha maendeleo ya soka la ushindani..
Daaaah, tayari Singida na Yanga out, na mchana huu kwa uchezaji wa timu zetu Mbao na Simba inaweza ikawa ndio bye bye.... Sijui nani katurogaaa... Tukkutana wenyewe kwa wenyewe maneno kibaoooo, ila wakija wageni kwisha habari yetu. Wachezaji na viongozi wanatakiwa kubadilika shida hawako serious na hawa focus kwenye mafanikio ya kimataifa.
ReplyDeleteHili Bonanza liwe sehemu ya Pre season kwa Timu zetu ndipo itapendeza kama wafanyavyo wenzetu ulaya kwenye makombe mbalimbali ambayo timu hucheza huko wakati zinawajaribu wachezaji wao wapaya waliosajiliwa kwenye msimu unaofuata! Hii iatakuwa na msisimko zaidi kuliko hivi sasa!
ReplyDeleteDeogratias nakubaliana na wewe. Itafutwe muda mwingine wa haya mashindano. Preseason ni wazo zuri .
ReplyDelete