ACHA KABISA!! YANGA YAIENDEA SIMBA MORO
KUELEKEA mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amefunguka kuwa, watalazimika kuweka kambi mkoani Morogoro ili kujiwinda na mchezo huo uliojaa presha kubwa kwa wachezaji na mashabiki.
Yanga na Simba zinatarajiwa kupambana Februari 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo mbili uliochezwa uwanjani hapo, timu hizo hazikufungana.
Yanga ambayo kesho Jumapili inatarajiwa kucheza dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, baada ya mchezo huo ndiyo itaenda Morogoro kuweka kambi.
Zahera alisema anafanya hivyo ili kuweza kuona anaimarisha kikosi chake ambacho kimekuwa kwenye mechi za kusafiri hapa na pale.
“Baada ya mechi yetu na JKT hapa Tanga, tutaweka kambi ya muda pale Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mechi zetu za ligi zijazo ikiwemo ya Simba.
“Tunataka kuendelea kujipanga na mechi za mzunguko huu wa pili kwani zimekuwa na changamoto kubwa, hivyo tunapaswa kupambana kweli, japo waamuzi nao wanatakiwa kuwa makini na kazi yao,” alisema Zahera.
0 COMMENTS:
Post a Comment