KIUNGO wa kibrazili, Arthur Melo ndio ametokea kuwa tegemeo la Barcelona kwenye safu ya kiungo katika siku za karibuni.
Arthur ana rekodi ya kutisha kwani tangu amejiunga na Barcelona hajawahi kupoteza mechi kubwa.
Mbrazili huyo sasa anatazamiwa kuendeleza rekodi yake wakati Barcelona itapoivaa Real Madrid kwenye `El Clasico’ ya Copa del Rey, leo.
Arthur amekuwa anawekwa benchi kwenye mechi mbalimbali msimu huu lakini kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde amekuwa akimpanga kwenye kikosi cha kwanza kwenye mechi dhidi ya timu kubwa.
Dogo huyo mwenye umri wa miaka 22 yupo vizuri na alitoa mchango mkubwa kwa Barcelona kuicharaza Sevilla 6-1 kwenye mechi ya marudiano ya robo fainali ya Copa del Rey, Jumatano iliyopita.
Arthur amecheza mechi 15 za La Liga msimu huu na hakuna mechi kubwa ambayo amepoteza.
Alikuwemo katika kikosi kilichoicharaza Real Madrid 5-1, pia Barcelona ilitoa sare za ugenini dhidi ya Atletico na Valencia (zote 1-1) na pia timu hiyo ilipoichakaza Sevilla 4-2 kwenye Uwanja wa Nou Camp (4-2).
Pia Arthur alicheza soka ya kiwango cha juu wakati Barcelona ilipopata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Tottenham kwenye Uwanja wa Wembley katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment