LEO Jumatano, mechi za raundi ya 25 katika Ligi Kuu Bara zinatarajiwa kuchezwa. Jumla ya mechi saba za raundi hiyo zitachezwa leo ambapo katika mechi hizo, timu kongwe za Simba na Yanga zitashuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi.
Ratiba ya mechi za leo ipo hivi; Prisons v Mbao (Sokoine), Singida United v Yanga (Namfua), Kagera Sugar v Mbeya City (Kaitaba), Azam v Alliance (Azam Complex), Stand United v Ndanda (Kambarage), Lipuli v KMC (Samora), JKT Tanzania v Biashara United (Maj.Gen. Isamuhyo)
Kesho ni Simba v Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa na Coastal Union v Ruvu Shooting Uwanja wa Mkwakwani.
Huu ni mzunguko wa pili wa ligi hiyo na wakati mzunguko huu ukiwa umeanza, bingwa mtetezi, Simba bado ana mechi tano za mzunguko wa kwanza mkononi ambazo ni dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Taifa, Coastal Union (Mkwakwani), Kagera Sugar (Kaitaba), Azam (Taifa) na Mtibwa Sugar (Taifa).
Yanga yenyewe haijacheza mechi moja ya mzunguko wa kwanza ambayo ni dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa.
Mzunguko wa pili tayari Yanga imecheza mechi mbili, Simba bado, na kufanya jumla ya mechi ambazo Yanga imeipita Simba ni saba ambazo zina jumla ya pointi 21. Simba imecheza mechi 14 na Yanga 21.
Mechi za mzunguko wa pili ambazo Simba haijacheza ni dhidi ya Prisons na Mbeya City, zote kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 54 ikiwa na michezo 21, inafuatiwa na Azam FC yenye pointi 47 na michezo 20, KMC imecheza mechi 23 imekusanya pointi 33, inafuatiwa na Simba yenye pointi 33 na mechi zake 14.
Pointi za Simba ni sawa na zile za Lipuli na Mbao ambazo zote zimecheza mechi 23 na zinashika nafasi ya tano na sita.
Awali wakati Yanga imecheza mechi 19 na kukusanya pointi 52 huku ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja, mashabiki wa timu hiyo walianza kuona tayari wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na kuiacha Simba kwa pointi 19 ambapo ilionekana hata Simba ikishinda mechi zake tano za kiporo na kukusanya pointi 15, haiwezi kuipiku Yanga.
Hivi sasa mambo yamebadilika baada ya Yanga kupata matokeo yasiyoridhisha kwenye mechi zake mbili zilizopita kutokana na kufungwa bao 1-0 na Stand United, kisha sare ya 1-1 na Coastal Union.
Tunaweza kusema kwa sasa ubingwa wa ligi hiyo umekaa mezani na timu yoyote kati ya hizo mbili au hata Azam FC inaweza kuchukua kama ikichanga vizuri karata zake.
Mzunguko wa pili ambapo Yanga inatakiwa kucheza mechi nyingi zaidi ugenini, tayari kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera anaona kuna kitu hakipo sawa kwa TFF na kinapaswa kufanyiwa kazi.
Baada ya wikiendi iliyopita Yanga kutoka sare na Coastal Union, ratiba ya mechi zake zipo hivi; leo Jumatano itakuwa mkoani Singida kucheza dhidi ya Singida United, kisha Jumapili ijayo itakuwa Tanga kucheza dhidi ya JKT Tanzania.
Februari 16, itacheza jijini Dar es Salaam dhidi ya Simba, kisha Februari 20 itakuwa Mwanza kupambana na Mbao. Baada ya hapo, itatakiwa kwenda Lindi kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya wenyeji wao, Namungo FC.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kati ya Februari 22 na 25, mwaka huu.
Haipo hivyo kwa Yanga pekee, bali hata Azam nayo mwezi huu itakuwa na ratiba ngumu yenye mechi mfululizo ndani ya kipindi kifupi.
Leo ikiwa nyumbani itacheza dhidi ya Alliance, Februari 11 dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Samora, Iringa, baada ya hapo, Februari 14 itakuwa Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine kucheza dhidi ya Prisons.
Haijaishia hapo, Februari 18 itacheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Februari 22 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kabla ya kumaliza mwezi kwa kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Kwa upande wa Simba, ratiba yao ya mwezi huu ipo hivi; kesho ni dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. Februari 12 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa ukiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha siku nne mbele uwanjani hapo itacheza na Yanga mechi ya Ligi Kuu Bara.
Februari 19 itakuwa kule Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kucheza dhidi ya African Lyon, kisha Februari 22 itarudi Uwanja wa Taifa kucheza na Azam, ratiba hii inaonyesha kuwa Yanga hana tena jeuri ya kujipa ubingwa.
Kutoka Championi.
0 COMMENTS:
Post a Comment