February 7, 2019






Na Saleh Ally
BAADA ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wamerejea nyumbani na sasa ni akili ya kusonga mbele kwenye michuano ya hapa.


Wakati wakiwa wamerejea si kwamba wamemaliza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Maana yake wanatakiwa kushiriki michuano ya hapa nyumbani hasa Ligi Kuu Bara lakini hawawezi kutoa akili yao kwenye Ligi ya Mabigwa Afrika.


Mechi bado zinaendelea na mechi inayofuatia ni dhidi ya A Ahly tena ingawa safari hii itakuwa jijini Dar es Salaam.


Mechi iliyopita wamefungwa mabao 5-0 jijini Alexandria lakini kabla ya hapo tayari walikuwa wamebandikwa mabao mengine kama hayo dhidi ya AS Vita.


Simba imepoteza kwa jumla ya mabao 10-0 ndani ya mechi mbili, kitu ambacho kwa mtu anayetaka maendeleo hakika kinafikirisha.


Najua, wengi wangependa hili lipite na kuangalia mbele kwa kutumia ule msemo wa Wahenga, "Yaliyopita si ndwele…". Sawa inawezekana kuwa hivyo lakini unawezaje kwenda mbele wakati nyuma yako kuna matatizo rundo ambayo umeshindwa kuyatafakari.


Simba wanataka kusonga ambalo naona ni jambo zuri lakini tujiulize, huku nyuma wameona matatizo ambayo wameyapitia kweli na wana nafasi ya kuyarekebisha.


Ninahoji kwa kuwa baada ya Simba kufungwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita, wakasema wamejifunza na kuahidi kuyafanyia kazi. Wakasema kutakuwa na mabadiliko makubwa watakaposafiri kwenda Misri kuwa Ahly.


Walipoingia uwanjani, ndani ya dakika 45 tayari walikuwa wamefungwa mabao 5-0. Hii ilionyesha wazi hawakuwa wamejiandaa au kujifunza kutokana na kile ambacho walikosea DR Congo.

Nimemsikia Kocha Patrick Aussems akisema kwamba hata wao kama benchi la ufundi waliona kuna ugumu sana kwao kushinda mechi hizo mbili za ugenini na hasa ya Ahly.


Sasa wanakutana na Ahly tena, ukubwa wake ni uleule na hakika haijabadilika. Wanaweza kuwaambia Wanasimba maneno yanayofanana baada ya mchezo huo?

Mnatakaje kuganga yajayo wakati matatizo bado yako mbele yenu? Aussems naona kama yuko salama sana na hili linaweza kuwa tatizo mbele.


Simba walisema kwamba wanachotaka ni kufika katika hatua za makundi ambazo wamefika. Lakini huwezi kusema baada ya kufika basi uboronge ili ujiandae kuvuka siku nyingine.


Nafasi ya kufika makundi inawezekana isiwe ya kila msimu. Nilishaeleza kuhusiana na Simba ninaamini wamejifunza na kujua katika kiwango hicho mambo yanakuwaje na utofauti wake uko vipi.


Kikubwa ni lazima Simba waonyeshe wamejifunza angalau. Aussems naye anapaswa kuwa na hofu ya kupoteza kibarua chake. Huenda amehakikishiwa sana ndio maana hata timu baada ya kufungwa mabao 10 katika mechi mbili, inaonekana ni kawaida.

Kumbuka, mwaka 2003, Simba ilikuwa katika hatua hiyo tena baada ya kumvua ubingwa Zamalek ambaye wakati huo alikuwa timu bora Afrika. Hatua ya makundi hawakufungwa idadi hiyo ya mabao.

Sasa ni kipindi tofauti, Simba mpya na tofauti, lakini imepoteza kwa idadi hiyo. Hili si sawa na ingekuwa Simba pia wanafanya kazi kwa mfumo wa timu zenye malengo zaidi katika hatua hiyo, angepoteza kazi.


Angalia Kocha Chiheb Elilli sasa hana kazi, kisa ni mechi mbili tu, kupoteza 3-0 dhidi ya Simba na kutoka sare na Al Ahly ambayo kweli ni kubwa kama alivyosema Aussems.

Ndani ya mechi mbili, JS Saoura wamepata pointi moja, wamefunga bao moja na kufungwa manne, kocha amepoteza kazi. Simba, mechi mbili, hawajafunga hata bao moja, hawana hata pointi moja na wamefungwa mabao 10, kocha hana hofu hata kidogo na mambo yanaendelea.


Hapa kuna jambo la kujifunza na hakika Simba hawajaanza kufanya kazi kwa mfumo wa timu zinazofika kwenye hatua hiyo. JS Saoura licha ya kuwa ni wageni katika hatua hiyo kuliko hata Simba lakini bado wamehakikisha wanaendana na kiwango walichofikia.


Simba haiwezi kuwa kubwa bila ya kuanza kufanya kazi kama wakubwa. Mfano, Aussems abaki lakini lazima aelezwe kwamba kama atapoteza mechi yoyote ya nyumbani basi safari imemkuta.


Maneno yake yanaonyesha kuwa laini sana, Simba inaweza kupoteza dhidi ya Al Ahly hapa nyumbani akarudia kusema ni kwa kuwa wao ni timu kubwa, hili haliwezi kuwa lengo la Simba.
  
Simba inataka kuwa kubwa, lazima ipambane na wakubwa na kama inakosea basi ijifunze kuanzia hapo na si kuendelea na makosa halafu iendelee kuonekana ni kawaida tu kwa kisingizio hicho hao ni wakubwa.

Kama Simba itapoteza mechi ijayo, hawana maana ya kucheza mechi mbili za mwisho, tayari itakuwa ni hasara kwao.

Kama nilivyowahi kueleza kuhusiana na wachezaji lakini benchi la ufundi na hasa Aussems anapaswa kuwajibika kunapokuwa na madudu kwa kuwa yeye ndio kiongozi na mtengeneza mfumo kama umefeli na yeye amefeli.


6 COMMENTS:

  1. Nyinyi wachambuzi njaa ndio mlikuwa mkiilaumu Simba kwa kubadirisha mako cha Kila Mara hivi wakimfukuza wewe ndio utatoa pesa za kuvunja mkataba kwa sababu timu ya Algeria wamefukuza kocha ndio na Simba wawsige swala la Simba kuvurunda limechangiwa na Mambo mengi ndio maana bodi ya Simba ilikutana wako kwa ajili ya kuijenga timu

    ReplyDelete
  2. Makanjanja at work.Kocha anafukuzwa kosa akipewa muda kosa.
    Soura walimbadilisha kocha baada ya kufungwa 3 na Simba na kushindwa kushinda nyumbani. Wacheni kupindisha ukweli.
    Ingekuwa timu zinabadilisha kocha kwa kufungwa mechi 2 basi hakuna kocha angekuwa salama.
    Kulinganisha Soura na Simba ni makosa kwani huyo aliyeandika anajua makubaliano ya
    kocha wa Soura na menejimenti ya timu yake?
    Tuige tu kama nyani?
    Naamini majeraha ya Nyoni na Kapombe umechangia safu ya ulinzi ya Simba kuyumba.

    ReplyDelete
  3. Ni vizuri ukiwa mchambuzi ukwfanya kazi yako ya kuchambua na ukawaacha wenye nafasi ya maamuzi wakaamua. Huwezi kuchambua na kuamua we mwenyewe, leo unasema simba akifungwa mechi ingine kocha afukuzwe, hili ni suala la ajabu kabisa maana pengine hujui hata terms za mkataba na mlengo ya simba na kocha wao. Wachambuzi wengine mnakera...

    ReplyDelete
  4. Muandshi yupo sahihi kabisa namuunga mkono. Kocha pamoja na wachezaji wake wa Simba hawapo serious au hawana uwezo wa kuiwakilisha Simba kwa ngazi waliofikia hivyo mabadiliko makubwa ya kikosi Simba yanahitajika pamoja na benchi lake la ufundi la sivyo hakuna jipya.

    ReplyDelete
  5. Kw amara ya kwanza naona ndugu mwandishi kawaambia ukweli #Simba.
    Na mimi ngoja niongezee; #Simba hawana kocha.. Aliyepo anakula pesa bure!!
    Huwezi kuwa kocha wa timu kama #Simba; timu ipo mashindanoni ukaruhusu wachezaji kadhaa (zaidi ya watano) waondoke kambini kwa visingizio mbali mbali huku ukijua kuwa una mechi ngumu ya nusu-fainali.. Haijalishi ni mashindano gani..!! Hata kama ingekuwa #Ndondo Cup! HAIWEZEKANI!! Kocha asiyeweza kujenga nidhamu huyo si kocha!
    Haya; kama hiyo haitoshi.. Wewe ni kocha wa timu unazungumzia tu mipango yako bila kujikita kwenye kukabiliana na ubora wa timu pinzani.. Utamsikia anasema tumekuja hapa si kukaba bali kufunguka, kutengeneza nafasi na kufunga bila kujali ubora wa timu pinzani.. na kweli alienda DR Congo na Misri kafunguka jamaa wakawa wanajifungia tu..!!
    Kocha makini lazima ujue muda muafaka wa kufanya mabadiliko muhimu ndani ya mechi...namna ya kukaba.. namna nzuri ya kupanda kutafuta goli bila kuhatarisha usalama wa lango lao...namna ya kuhamasisha hamasa ya timu inapokuwa nyuma ya mpira... namna ya kuwaadhibu wachezaji wasiojituma...!! Yeye yupo yupo tu kama shabiki kashikilia kidevu chake..!!

    Na cha ajabu kisa ni kocha mzungu basi kina Haji Manara wanaamua kujibebesha majukumu ya kuwajaza ujinga na matumaini hewa mashabiki wao!!Kocha hataki msaidizi..(ujue hata wale wasaidizi wake wengine ni makocha sema idara tu ndo zinatofautiana ila sidhani kama anawasikiliza make hataki mawazo mbadala..!!
    Kocha hajui thamani ya jezi ya #Simba! Kocha hana mikakati ABCD ya ushindi!!

    Tumjadili kocha wa #Simba si kwa muonekano wake..bali kwa maneno, maamuzi na matendo yake..!!
    Pale hakuna kocha aisee!! MO anapigwa na mashabiki wa #Simba "wanabemendwa"!
    Huyu mzungu tupeni kule make namuona kama tapeli tu..!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic