February 15, 2019





NA SALEH ALLY
SIKU chache zilizopita, mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji alijitokeza kwa mara ya kwanza hadharani na kuzungumzia kuhusiana na klabu hiyo.


Hii ilikuwa mara ya kwanza Dewji kuzungumza hadharani kuhusiana na Simba ikiwa ni miezi kadhaa kukutana na misukosuko ya kutekwa.


Tangu atekwe, Mo Dewji hakuwa amewahi kuzungumza na Wanasimba pamoja na wapenda mpira wa Tanzania waliotamani kumuona tena anarejea katika hali ambayo walikuwa wakimuona nayo.


Mo ameamka tena na kuzungumza. Amekubali kuzungumza katika kipindi ambacho alikuwa anahitajika sana kufanya hivyo kulingana na wakati wenyewe.

Ulikuwa wakati ambao ulihitaji mtu kama yeye kuzungumza na kuinua upya matumaini ya Wanasimba ambao wengi walishaanza kuona kiza mbele yao.


Kipigo cha mabao 10 katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Makundi, kiliwachanganya. Walianza kuchapwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita ya DR Congo wakiwa Kinshasa. Mechi iliyofuata wakasafiri hadi Alexandria, Misri ambako walikutana na kipigo "pacha" kwa kuchapwa mabao 5-0 dhidi ya Al Ahly.


Baada ya mechi hiyo, ilikuwa ikifuatia mechi tena dhidi ya Al Ahly na safari hii, ilikuwa nyumbani Dar es Salaam, lakini Ahly ni walewale na mashabiki wengi waliapa kutokwenda uwanjani kwa hofu ya kukutana na kipigo kingine cha mabao 5-0.



Simba ilikuwa na nafasi ya kushinda uwanjani, lakini ilihitaji ambaye anaweza kulithibitisha hilo kabla ya mechi. Mwenye uwezo wa kuwashawishi mashabiki wafike uwanjani na kuicheza mechi hiyo lakini mzungumzaji wa safari hii, alihitajika kuwa makini na tofauti, asifanane na mzungumzaji aliyepita ili kubadili upepo.


Lilikuwa jambo zuri kwa Mo kuzungumza na si msemaji wa klabu, Haji Manara ambaye alijitahidi kwa kiwango chake, bahati mbaya timu ikapoteza mechi zote hizo mbili.

Pamoja na hivyo, uwezo wa Mo Dewji kuwa wazi, kueleza Simba inaweza kufunga lakini ile kukubali uwezo wa Al Ahly uko juu lakini wanachotaka ni kuhakikisha wanashinda kwa kupambana kwa kiwango, lilikuwa jambo zuri zaidi kuonyesha inawezekana.


Sura yake ya msisitizo, sura yake iliyoonyesha yu tayari kwa mapambano na yu tayari kwa mabadiliko, iliamsha upya morali na mashabiki wa Simba wakaendelea kuweka rekodi ya wingi wa idadi ya watu wanaojitokeza uwanjani.


Kwa kuwa Simba hawakati tiketi za msimu, kitendo cha kufungwa mabao 5-0 katika mechi mbili mfululizo, halafu mechi ya tatu mashabiki wanajaa pomoni, hii ni rekodi ya aina yake.

Nani ambaye angekuwa na jeuri hiyo, kuinua mguu tena siku za kazi kwenda uwanjani kuangalia "maumivu" kutoka kwa Waarabu?


Nani aliyekuwa tayari tena kuiamini Simba katika kipindi hicho kigumu, kipindi ambacho kilionyesha wazi mambo yameishaharibika? Hakika mtu kama Mo Dewji alihitajika.


Sura yake ya upande wa pili wa sarafu, imetengeneza mambo tofauti, mabadiliko ya nguvu na imani na huenda ikawa sura muhimu inayohitajika zaidi katika Klabu ya Simba.

Sura hiyo inahitajika kwa mashabiki wa Simba kwa maana ya kuwaambia ukweli, kukubali upungufu na kuonyesha ukweli ndani ya kushinda.

Vizuri kama sura hiyo pia ikatumika kwa wachezaji, kuwaeleza namna mambo yalivyokuwa na kuwasisitiza kwamba mambo muhimu yanayotakiwa badala ya kulewa sifa na kushuka kwa kiwango.


Mo Dewji ni mfanyabiashara mkubwa, amefikia kiwango cha juu cha mafanikio. Hili si jambo rahisi na yeye atakuwa anajua anafanya nini kuyafikia mafanikio.

Sura yake ya mwendo wa mafanikio ndiyo inayohitajika zaidi Simba kwa kipindi hiki ili kuwe na mwendo sahihi unaofanana na uwekezaji.

Simba imewekeza, lakini lazima tukubali ndani yake kuna matundu ya upungufu wa mambo na kunatakiwa kuwe na wasema ukweli kwa nia ya kufanya mambo sahihi.



Bado kuna baadhi ya wachezaji wa Simba hawajawa makini. Inaonekana wazi sura ya Mo Dewji inayoashiria hataki utani, imewasaidia kubadilika na kucheza katika uwezo wao ulioisaidia Simba. Hivyo vizuri akaendelea kuihifadhi sura hiyo na inapotakiwa, aitoe na kuivaa ili kumaliza kazi.

2 COMMENTS:

  1. Naona Ukiandika Wewe Makala Inaeleweka Lakini Hawo Wengine Kwenye Blog Hii Wanatuandikia Pumba Tupu Ila Ww Unasimamia Kwenye Ukweli Na Umeonyesha Kuwa Wewe Kweli Ni Mkongwe Kwenye Kazi Ya Uandishi Wa Habari Za Michezo
    Big Up Saleh Ally A.k.A Salehjembe

    ReplyDelete
  2. Makala mazuri siku zote nasema Mo ni kiongozi na mueledi wa mambo na kama alivyosema kiongozi Mkongwe wa simba Jabiri Ali shika Mkono yakwamba Simba wamejichelewesha kukosa kuwa na Mo mapema zaidi ya sasa. Unajua wakati mwengine sisi watanzania ni watu wa ajabu katika masuala ya uwekezaji,Mohamedi Mo ni Mtanzania,Anauwezo,ni Mwanafamilia wa Simba asilia na anamapenzi na uchungu wa club lakini bado alikuwa akiekewa figisu kuekeza Simba? Utashi,hamu na dhamira ya Mo kuekeza ndani ya Simba umejaa zaidi kutaka kuiona club yake hiyo pendwa ikifanya vizuri nakuwa moja ya timu imara zaidi barani Africa kuliko kufikiria faida yake binafsi ndani ya Simba, na faida gani hasa kwa Mo ndani ya Simba wakati yeye ni Dollar billionaire tayari.Hakika ni mapenzi yane binafsi na anastahili pongezi kwa kujitoa kwake kuhakikisha maendeleo yanapatikana ndani ya simba. Kwa upande mwengine kama Mo angeiacha Simba iteseke kama aliyofanya hapo awali wakati uwezo wa kuisaidia Simba anao basi asingekuwa anaitendea simba haki vile vile.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic