IMEKUWA ni kama bahati mbaya sana kwa Watanzania wapenda soka kutokana na kutamani pepo zaidi kuliko kujitengenezea njia ya kufika huko.
Maisha ya mkato kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiligharimu soka letu kila kukicha kutokana na wadau walioshika hatima ya uongozi kuamini ni rahisi kufanya vizuri bila mipango.
Wanasahau ukweli wa mambo kuwa hakuna njia ya mkato ya kuweza kufikia hayo wanayotutamanisha kuwa tutayafikia kutokana na kutokuwepo mipango yakinifu kuanzia ngazi ya chini.
Mara nyingi nimekuwa nikishuhudia umati mkubwa wa Watanzania ukifurika Uwanja wa Taifa kuipa nguvu timu yao ya taifa au klabu zao katika michuano mbalimbali ya kimataifa, lakini mara nyingi baada ya mechi kuisha kila mmoja huondoka uwanjani kichwa chini.
Matokeo mabovu katika michuano ya kimataifa yamekuwa yakiwasononesha wapenda michezo wengi ambao dhahiri siku zote wana mapenzi ya dhati na timu yao ya taifa au klabu zao lakini matokeo mabovu yanawaangusha.
Inawezekana mashabiki Watanzania ni mfano wa kuigwa kutokana na kuonekana kutokata tamaa ya kuziunga mkono timu zao, licha ya mara nyingi kuonekana kama kichwa cha mwendawazimu.
Kwa sasa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano mikubwa ya Afrika kwa vijana ‘AFCON’ ambayo imepangwa kufanyika Aprili 14 mpaka 28, mwaka huu.
Wawakilishi wetu ambao ni Serengeti Boys wamepangwa kundi moja na timu za Uganda, Nigeria na Angola, hivyo hapa hakuna mchezomchezo.
Nimesikia mara kadhaa kuwa wengi wanalalamikia maandalizi duni wanayopewa vijana wetu, hakika unaweza kusema ni lazima wahusika waweke nguvu kubwa kabla ya michuano kuanza ili tuweze kufanya vyema.
Kama Waswahili wanavyonena, mcheza kwao hutuzwa, kwa maana hiyo shime Watanzania ni jukumu letu kuwaunga mkono vijana hao ambao ndio tumaini pekee lililobakia kwa timu zetu za taifa za vijana.
Wachezaji pia hamtakiwi kukata tamaa, mnatakiwa kuliwakilisha vyema taifa kwani mashindano haya ni mara ya kwanza kuchezwa kwenye ardhi ya Tanzania, hivyo ni vyema tukaweka rekodi ya kuyatwaa pia.
Tunajua vijana mna moyo wa upambanaji, hivyo mnaweza pia kutumia fursa hii pia kujifunza kimataifa kwani lazima kutakuwa na mawakala mbalimbali watakaokuja kusaka vipaji.
Wenzetu Ulaya wanafahamu kwamba mchezaji anajengwa kuanzia akiwa mdogo ambapo kuna baadhi ya vitu anakuwa akielekezwa, hivyo inakuwa rahisi kwake kushika mambo mbalimbali kabla ya kuwekwa timu ya wakubwa.
Kama tutawekeza zaidi kwa vijana hao wa Serengeti Boys ni dhahiri ipo siku ile pepo ambayo tunaitamani kuiona katika soka letu itakuja kuonekana ingawa kiuhalisia si kazi rahisi.
0 COMMENTS:
Post a Comment