Na Saleh Ally
MECHI ya leo, mashabiki watakwenda uwanjani
wakiwa na tambo za kila aina kutoka kila
upande.
Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu Bara na wana kila
sababu ya kujitapa, lakini Simba wanawaona
Yanga ni wepesi kwa kuwa wanaamini viporo
walivyonavyo ndivyo vinavyowafanya watani
wao kuonekana wanatamba.
Kawaida katika mpira, mechi ya leo ni mpya,
haiwezi kuwa zile zilizopita ingawa kutakuwa na
vitu kadhaa kwa ajili ya kukumbushia.
Mechi ya leo inajitegemea na itakuwa na
matokeo yake yanayojitegemea. Kikubwa ni
suala la ufundi ambalo linaweza kuwa gumzo
mwisho wa mchezo huo.
Mashabiki wengi wa Simba, wanawadharau
Yanga na wako baadhi wa Yanga wanaiamini
timu yao lakini hii haiwezi kuwa mechi laini
badala yake ya ushindani ingawa suala la
matokeo ya kushitua linaweza kujitokeza leo.
Yanga ina kikosi kizuri, tayari wamefunga
mabao 40 katika mechi zao 23, maana yake
wana uwezo wa kufunga tena katika mechi
yoyote ingawa Simba wanaonekana kuwa
hatari zaidi kwani pamoja na upungufu wa
mechi zao, wanazo 15, tayari wamefunga
mabao 31, ukiwa ni wastani wa mabao mawili
kila mechi.
Shida kubwa katika mechi hii huwa ni presha
kutokana na ukubwa wake na kuna wachezaji
hupoteza asilimia ya viwango vyao kwa uoga.
Kama si hivyo, basi wana nafasi kubwa ya
kufanya vema na kuifanya mechi kuwa bora.
Mechi ya leo ni nzuri kuangalia kila dakika kwa
kuwa ina uamuzi wa nani kuwa bingwa baada
ya hapa. Nafasi ya sare katika mechi ya leo ni
finyu sana.
Kagere:
Vile vichwa vyake vya kurukia, ile hamu yake ya
kufunga na kucheza bila ya kuchoka, ni hatari
kwa Yanga.
Tegemea kuona mapambano ya kweli kati yake
na Shaibu Abdallah; kwa kuwa wote ni wazuri wa kuruka vichwa.
Hatari zaidi ya Kagere ni Anajua akae wapi kwa wakati gani lakini uwezo wa kuchomoka ghafla na kuwa katika sehemu inayotakiwa na inaonekana Simba wameishajua uwezo wake huo, hivyo wanautumia vizuri. Lazima Yanga wawe makini.
Chama & Mkude:
Kama Jonas Mkude atakuwa katika kiwango
chake basi, Simba itacheza ule mpira wake wa
kasi na pasi nyingi za haraka, umiliki wa mpira
utakuwa wao.
Mzambia Claytous Chama akiwa katika kiwango
chake, maana yake Kagere na Okwi watacheza
katika kiwango kizuri na akishirikiana na Mkude
vizuri, maana yake Simba itatulia na kuwapa
wakati mgumu Yanga.
Wakati huo, James Kotei atakuwa na nafasi
nzuri ya ulinzi. Hii itakuwa ni kazi ngumu kwa
Yanga kupitisha mashambulizi na kuzuia kwa
uhakika.
Okwi:
Huyu ni hatari sana kwa Yanga kwa kuwa
anajua afanye nini katika mechi hiyo. Wakati
fulani huwa anapania mechi inamshinda. Lakini
siku akiwa vizuri yamekuwa mateso makubwa
ya Yanga.
Okwi anakuwa hatari kwa Yanga kwa kuwa kwa
upande wa Simba ndiye mchezaji mwenye
uzoefu zaidi na mechi hiyo kuliko wengine wote
kama ilivyo kwa Yondani upande wa Yanga.
Mganda huyo ana uwezo wa kupiga kushoto na
kulia, ana uwezo wa kuwahadaa mabeki hata
wawili na mwepesi kuingia kwenye eneo la
hatari kwa kuwa hadi sasa anashikilia rekodi ya
kusababisha penalti tatu katika mechi moja
dhidi ya Yanga.
Maana yake, lazima kumchunga asisababishe
penalti, lazima kumchunga asipige mashuti,
jambo ambalo linataka utulivu wa hali ya juu
sana.
Juuko:
Huyu ni beki mzuri lakini si mtu makini. Huenda
mashabiki wengi wanampenda lakini amekuwa
hafikirii nini kitafuatia baadaye.
Uchezaji wa Makambo asipoangalia anaweza
kusababisha penalti. Awe makini na faulo zisizo
na sababu za msingi lakini suala la ujanjaujanja,
kucheza faulo za kimyakimya mwamuzi akiwa
makini, ataambulia kadi nyekundu na kuipa
wakati mgumu Simba.
Zana:
Uchezaji wake ni kama hayuko makini hivi lakini
ni hatari kusababisha madhara hasa pale timu
inapokuwa inashambulia. Simba tayari
wamejua namna ya kumtumia hasa zile krosi
zake za nusu uwanja.
Ana shabaha ya kufikisha mipira eneo sahihi na
anafanya hivyo kwa haraka, jambo ambalo
litawalazimisha Yanga kuwa wepesi la sivyo
wataingia kwenye kucheza faulo zitakazozaa
penalti au kadi au kufungwa kabisa.
Ajibu:
Ana asisiti 10 hadi sasa, hili si jambo dogo
ukiachana na kwamba ana uwezo wa kufunga
mabao tena katika sehemu ambayo
haijategemewa.
Tambwe:
Katika wachezaji watakaoingia leo, katika mechi
tano zilizopita, Amissi Tambwe ni mmoja wa
waliofunga mabao.
Katika mechi hizo tano, Shiza Kichuya ana
mabao mengi zaidi lakini leo hatakuwepo.
Hivyo Tambwe si mchezaji wa kumdharau hasa
kulingana na uwezo wake katika umaliziaji na
uzoefu wa Simba na Yanga kwa kuwa
amefanikiwa kuivaa Yanga akiwa Simba na
akaifunga halafu akaifunga Simba akiwa Yanga.
Fei Toto:
Hivi karibuni amekuwa akikata pumzi mapema,
lakini akiwa katika kiwango chake kizuri lazima
wamuangalie katika mipira ya mbali hasa
upigaji mashuti.
Ajibu amefunga mabao ya mikwaju ya mbali
hasa ile ya faulo, kama Simba watacheza karibu
na lango lao na kusababisha faulo, wajue safari
imewakuta.
Moja ya mabao aliyofunga mengi ni mashuti ya
mbali, ni mchezaji mwenye shabaha. Lakini ana
uwezo mkubwa wa kupiga pazi za mwisho,
jambo ambalo kama Simba watatoa nafasi,
wamekwisha.
Makambo:
Ana mabao 11 katika ligi, unaweza vipi
kumbeza? Ni mmoja wa wachezaji hatari zaidi
kwa mipira ya juu na amekuwa akiutumia vizuri
urefu wake.
Wachezaji wa Simba ukiachana na Erasto Nyoni
ambaye ndiye amerejea na hatacheza leo,
wamekuwa wavivu kuruka vichwa na uliona
mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika
walivyofungwa mabao laini ya kichwa. Lazima
Simba wawe makini na Makambo.
Ninja & Dante:
Mmoja kati yao lazima ataanza na Kelvin
Yondani. Hawa ni mabeki wazuri na hasa katika
mipira ya vichwa na wanacheza kama mabeki,
wanajituma na kwa nguvu.
Kikubwa wanachotakiwa kuwa nacho makini ni
faulo karibu na eneo la hatari au ndani ya eneo
la hatari.
Kuitengenezea Simba faulo eneo la karibu na
lango ni hatari lakini penalti itakuwa ni hatari
zaidi kwao.
Pamoja na kujitahidi kukwepa adhabu, kwa
kuwa wanakutana na washambulizi na viungo
wepesi na wajanja na hasa kadi.
MECHI 5 ZILIZOPITA YANGA VS SIMBA
OKT 1, 2016
Simba 1-1 Yanga
Yanga: Amissi Tambwe
Simba: Shiza Kichuya
FEB 25, 2017
Simba 2-1 Yanga
Yanga: Saimon Msuva (penalti)
Simba: Laudit Mavugo, Shiza Kichuya
OKT 28 2017
Yanga 1-1 Simba
Yanga: Chirwa
Simba: Kichuya
APR 29,2018
Simba 1-0 Yanga
Nyoni
SEP 30, 2018
Simba 0-0 Yanga
WALIOFUNGA MABAO MENGI MECHI 5
ZILIZOPITA:
3-Kichuya
1-Tambwe
1-Msuva
1-Mavugo
1-Nyon
1-Chirwa
0 COMMENTS:
Post a Comment