Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa mshambuliaji wao Mrundi, Amissi Tambwe jana alirejea mazoezini rasmi na leo anaweza kuitumikia timu yao.
Tambwe anarejea uwanjani baada ya mchezo dhidi ya Biashara kugongana na kipa wa timu hiyo, Nurdin Balora katika mchezo wa Kombe la FA uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tambwe ambaye aliukosa mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara walipocheza na Coastal Union ya Tanga na kutoka sare ya bao 1-1, leo huenda akawa sehemu ya kikosi hicho kitakachoivaa Singida United kwenye Uwanja wa Namfua huko Singida.
Daktari mkuu wa timu hiyo, Edward Bavu alisema kuwa mshambuliaji huyo jana jioni alianza mazoezi kwenye Uwanja wa Namfua.
“Tambwe amepona na yupo fiti kucheza mchezo wetu wa ligi dhidi ya Singida tutakaocheza kesho (leo), baada ya kutolewa nyuzi zake usoni ambako alipasuka na kushonwa.
“Pia, kiungo wetu Fei Toto naye amepona majeraha ya misuli aliyoyapata katika mchezo wetu na Coastal Union ambayo yalimsababishia ashindwe kumaliza mchezo huo,”alisema Bavu.
Tambwe hadi sasa ameshapachika mabao sita kwenye ligi na Kombe la FA amefunga mabao manne akiwa ni kati ya washambuliaji mahiri zaidi hapa nchini kwa sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment