ZAHERA AONYESHA MAKUCHA YAKE TENA YANGA
KOCHA Mkuu wa Yanga raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera, ameonyesha makucha yake baada ya kukerwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga wanaotumia jina lake kumsema vibaya jambo ambalo amelitafsiri ndivyo sivyo na kutangaza hali ya hatari kwao.
Hali hiyo imejitokeza siku chache tu baada ya timu hiyo kuonekana kufanya vibaya kwa kufungwa mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara na Stand United kisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union na suluhu ya 0-0 dhidi ya Singida United.
Zahera alisema takribani mwezi sasa ameanza kuona kama kuna baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wanatumia jina lake kumdharau na wengine kumtukana bila sababu za msingi jambo ambalo halimpendezi kwani yeye hajawahi kumdharau mtu.
“Kuna mtu mmoja anaitwa Jitu, huyu amekuwa akiniudhi sana kwani amekuwa akijirekodi video na kusambaza kwenye mitandao akitumia jina langu kunidhihaki na hata akiulizwa anasema amezungumza na mimi, hivyo aache tabia hiyo kwani mimi siyo mtu wa kuchezewachezewa ovyo.
“Mbali na huyo, kuna wengine wengi wamekuwa wakinitukana bila sababu na hasa ukiangalia mimi nipo Yanga kwa mapenzi yangu tu, na ndiyo maana nafanya kila hali ili timu ifanikiwe, hivyo wasione timu inapopoteza ndiyo iwe sababu ya kunifedhehesha badala ya kunipa moyo.
“Sipendezwi na jambo hilo hata kidogo na naweza kuwachukulia hatua zaidi,” alisema Zahera.
0 COMMENTS:
Post a Comment