AZAM YAINGIA VITANI NA YANGA
UONGOZI wa Azam FC umeweka mikakati thabiti kuhakikisha inachukua Kombe la FA msimu huu ili kuweka rekodi ya kulichukua kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Kwa kauli hiyo, Azam watakuwa wameingilia mipango ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera aliyoiweka ya kuutaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, mwaka huu.
Azam, tangu imepanda kucheza ligi mwaka 2008 haijawahi kutwaa taji hilo ambalo tayari limechukuliwa na Yanga, Simba na Mtibwa Sugar pekee tangu 2016. Akizungumza na Championi Jumatano, mratibu wa timu hiyo, Philipo Alando, alisema malengo yao lazima yatimie msimu huu kwa kuhakikisha wanachukua kombe hilo kutokana na ubora wa kikosi chao kinachoongozwa na Obrey Chirwa na Donald Ngoma.
“Azam tangu tumefanikiwa kupanda kucheza ligi tumechukua mataji tofauti ya ubingwa ambayo ni ligi, Kombe la Kagame na Mapinduzi lakini hatujawahi kuchukua la FA pekee.
“Malengo yetu hivi sasa ni kuchukua msimu huu tukamilishe tageti yetu tuliyojiwekea ya kuchukua makombe yote tuliyowahi kushiriki katika vipindi tofauti,” alisema Alando.
Bingwa wa michuano ya FA, ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Azam tayari imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya hiyo ambayo imepangwa kucheza na Kagera Sugar mwishoni mwa mwezi huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment