BAADA YA KAMATI YA FITINA KUMALIZA KAZI, KOCHA SIMBA AONGEZA HOFU
SIMBA, leo Jumamosi inatarajiwa kujitupa uwanjani kucheza na AS Vita ambapo kocha mkuu wa timu hiyo Mbelgiji, Patrick Aussems amepanga kuutumia mchezo huo kuweka historia kwa kupata ushindi kisha kucheza Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kauli hiyo, aliitoa juzi mara baada ya kumalizika kwa mazoezi wakiwa katika maandalizi ya mwishoni kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Ni mechi ngumu kwetu kwa sababu tunacheza na wapinzani ambao walitufunga kwao, lakini hakuna namna inabidi tushinde sasa kwa ajili ya kufika hatua ya robo fainali kukamilisha kile ambacho tulikuwa tunakiwaza kila mmoja hapa,” alisema kocha huyo.
Simba itashuka uwanjani ikiwa na hasira ya kupoteza mchezo uliopita wa michuano hiyo dhidi ya JS Saoura uliochezwa Algeria ambao ulimalizika kwa timu hiyo kufungwa mabao 2-0.
Aussems alisema kuwa mchezo huo wanauchukulia kama fainali ili kuhakikisha wanashinda.
Aussems alisema tayari amekamilisha maandalizi ya kikosi chake kuhakikisha wachezaji hawafanyi makosa kama yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita.
“Mchezo huo na AS Vita wa mwisho, hivyo ni lazima tucheze kufa au kupona ili kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu tuliyojiwekea ya kuwafunga wapinzani wetu na kutengeneza historia kubwa nchini.
“Na hilo linawezekana kabisa kwetu, kwani tutakuwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani, hivyo ninatarajia kuwaona mashabiki wa Simba wakijitokeza uwanjani kwa ajili ya kuisapoti timu yao ili tuchukue pointi nyingine tatu baada ya kuzichukua za Al Ahly na JS Saoura hapa nyumbani.
“Lakini wakati tukiweka mikakati hiyo ya ushindi, tutaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ya kuwahofia wapinzani wetu kwa maana ya kulinda na kushambulia goli la wapinzani ili Vita wasipate bao golini kwetu,” alisema Aussems.
0 COMMENTS:
Post a Comment