RAUNDI HII YA PILI KWA WANAWAKE TUTAONA MENGI
MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti Lite, umeanza wikiendi iliyopita.
Katika mechi za Jumamosi na Jumapili, matokeo yalikuwa hivi; Yanga Princes 3-2 Sisterz, Marsh Queens 2-2 Baobab, Mlandizi Queens 4-0 Mapinduzi Queens, Simba Queens 4-0 Tanzanite Queens na JKT Queens 5-0 Evergreen Queens.
Kuendelea kwa mzunguko wa pili, kumekuja baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika Februari 3, mwaka huu ambapo JKT Queens ilimalizika mzunguko huo ikiwa kinara kwa kujikusanyia pointi 33, baada ya kushinda michezo yote 11.
Katika mzunguko huo, tulishuhudia rekodi kadhaa zikiwekwa, ikiwemo ya JKT Queens kuibamiza Evergreen Queens mabao 16-0, huku mshambuliaji wa JKT Queens, Fatuma Mustapha akifunga mabao 15 kwenye mechi tatu pekee.
Katika mechi hizo tatu ambazo Fatuma alifunga jumla ya mabao 15, kila mechi moja alifunga mabao matano. Ikumbukwe kuwa Fatuma ndiye aliyekuwa kinara wa mabao kwenye ligi hiyo kwa msimu uliopita alipomaliza akiwa na mabao 18.
Championi Jumatano limekuandalia baadhi ya rekodi zilizowekwa toka kuanza kwa ligi hiyo, huku ikiangazia nafasi ya ubingwa na timu ambazo zipo kwenye uwezekano wa kushuka daraja.
JKT QUEENS BADO WABABE JKT
Queens inayotumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ndiyo bingwa mtetezi wa ligi hiyo, ambapo msimu uliopita iliutwaa bila ya kupoteza mchezo wowote. Kwa hali ilivyo, kuna uwezekano wakarudia kile walichokifanya msimu uliopita, kwani hadi hivi sasa wameshacheza michezo 12 na hawajadondosha alama yoyote. Wapo kileleni na pointi 36. Inayofuatia ni Mlandizi Queens ambayo imevuna pointi 26, ikiwa imeshuka dimbani mara 12. Imezidiwa pointi 10 na kinara.
VITA YA UFUNGAJI IMENOGA
Fatuma Mustapha na Asha Rashidi ‘Mwalala’ ambao wote wanaitumikia JKT Queens, wamejikuta wakiingia kwenye vita ya kuwania Tuzo ya Mfungaji Bora msimu huu ambapo kwa sasa wamepishana bao moja.
Fatuma amefunga mabao 23, huku Mwalala akishika nafasi ya pili akiwa amefunga mabao 22. Ukiwaondoa hao, wachezaji wengine wenye mabao mengi ni Donesia Minja mwenye 14 na Stumai Abdallah mwenye 13. Hawa wote wanacheza JKT Queens.
YANGA PRINCES YAPATA MATUMAINI
Ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sisterz wikiendi iliyopita, umeiweka pazuri timu hiyo mara baada ya kuwa na mwanzo mbovu wa ligi katika mzunguko wa kwanza.
Vipigo vya mabao 7-0 kutoka kwa Simba Queens, kisha 8-1 kutoka kwa JKT Queens, vilianza kuivuruga timu hiyo na kuiweka pabaya kwenye msimamo wa ligi hiyo hadi mashabiki wakaanza kuhisi huenda timu hiyo ikashuka daraja.
Kwa sasa Yanga Princes wamejihakikishia usalama wa kubaki ligi kuu, ikiwa watafanikiwa kushinda michezo miwili inayofuata, ambayo itawafanya wavune pointi 22, ambapo kwa sasa wapo nafasi ya saba na pointi zao 16. SIMBA
QUEENS WAPO VIZURI
Wapo nafasi ya tatu wakiwa imevuna pointi 25, kwenye michezo 12 waliyocheza. Katika michezo hiyo, wamepoteza mitatu pekee na kutoka sare mchezo mmoja. Wameibuka na ushindi mara nane Wameanza vyema raundi ya pili kwa kuvuna ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzanite, wanaonekana kuimarika kadiri siku zinavyokwenda, huku wakitamba na viungo wao wawili raia wa Burundi, Asha Djafar na Joelle Bukuru, ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
HAWA WANAWEZA KUSHUKA DARAJA
Hali siyo mzuri kwa Evergreen Queens na Mapinduzi Queens, ambao hadi sasa wapo nafasi mbili za chini. Mapinduzi wamevuna pointi mbili pekee kwenye michezo 12 waliyocheza, huku Evergreen wenyewe wana pointi tano, wakicheza michezo 12.
Wamerudi wakiwa na hali ileile ya mzunguko wa kwanza, ambapo mechi zao za kwanza mzunguko wa pili wamejikuta wakila vichapo. Evergreen wamefungwa 5-0 na JKT Queens, huku Mapinduzi wakilambwa 4-0 na Mapinduzi Queens.Endapo hawatabadilika kwenye michezo 10 iliyobaki, yawezekana kabisa wakashindwa kubaki ligi kuu na wakarudi zao Ligi Daraja la Kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment