TSHISHIMBI ABADILISHIWA MAJUKUMU YANGA, APEWA MENGINE
KATIKA kukiimarisha kikosi chake, Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amembadilishia majukumu kiungo wake Papy Tshishimbi. Kiungo huyo alirejea hivi karibuni akitokea kwenye majeraha ya goti aliyoyapata katika mechi za mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Bara na kusababisha akae nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Tshishimbi tangu amerejea uwanjani ameonekana kuwa na msaada mkubwa katika timu hiyo na kusababisha ushindi baada ya bao lake la kwanza alilolifunga katika mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya KMC.
Zahera alisema kuwa, kiungo wake huyo, hivi sasa atakuwa anamtumia kama namba 10 badala ya namba sita na 8 katika michezo ijayo ya ligi na Kombe la Shirikisho.
Zahera alisema, kikubwa anataka kumuona kiungo wake huyo anaiongezea nguvu safu ya kiungo ya kati kwa kukaba na kumtengenezea nafasi za kufunga mabao mshambuliaji wake Heritier Makambo. Aliongeza kusema, alichukua maamuzi hayo baada ya kumuona Tshishimbi akifanya kazi isiyo yake ya kukaa na mpira, huku akipiga chenga zisizokuwa na faida katika timu.
“Tshishimbi ni mchezaji mzuri, lakini mara nyingi amekuwa akicheza bila kufuata maelekezo ambayo nimekuwa nikimpa kabla ya kuchukua maamuzi ya kumsogeza mbele na kumbadilishia majukumu.
“Mwanzoni nilikuwa nikimchezesha namba 6 na 8 kabla ya kumtoa na kumchezesha Fei Toto namba 6 huku Kamusoko na Boban nikiwabadilisha kucheza kwa kupokezana namba 8 na kikubwa ni katika kukiimarisha kikosi changu.
“Lengo ni kumuona Tshishimbi akifanya vitu vyake vingi mbele kwenye goli la wapinzani wetu na hiyo yote ni baada ya kumuona akifanya masihara kwa kupiga chenga na kuuchezea mpira bila ya sababu,” alisema Zahera.
0 COMMENTS:
Post a Comment