May 2, 2019

MEI 5 2019 ni siku muhimu kwa wanachama wa Yanga kufanya uchaguzi wao kwa ajili ya kupata viongozi ambao wataendeleza jahazi la uongozi kwenye klabu kubwa Tanzania.

Mpaka kufikia hapa mchakato umepitia sarakasi nyingi kufika hapa kwa sasa sio jambo la kubeza bali pongezi ni kitu muhimu.

Mfumo wa maendeleo kwa timu zetu zote zinategemea uongozi ambao unasimamia maslahi na sera za timu katika suala zima la uendeshaji.

Kumpata kiongozi ni mchakato ambao unafanywa na wanachama kwa kuzingatia katiba pamoja na utaratibu ambao umwekwa hasa kwa kuzingatia makubaliano ambayo watakuwa wamefikia.

Kwa sasa kwenye soka la Tanzania ni timu ya Yanga ndio ipo kwenye mchakato wa kuchagua viongozi ambao wataiongoza timu hiyo kuelekea kwenye mafanikio.

Rai kubwa ambayo napenda kuwaambia wanachama wa Yanga kuwa makini kipindi hichi ambapo kwa sasa tayari mchakato wa kampeni umezinduliwa na wagombea wameshaanza kumwaga sera zao.

Kitu cha msingi ambacho kinapaswa kizingatiwe na wanachama ni kuhudhuria mikutano na kusikiliza sera kwa umakini ili kupata picha ya aina ya kiongozi ambaye watakwenda kumchagua.

Nafasi zote ni muhimu na nyeti kwa kila idara hivyo kosa moja litaigharimu timu na kuirejesha kule ambako ilikuwa awali kwenye migogoro hii haitapendeza.

Cha msingi viongozi ambao wanagombea wafanye kampeni safi bila kuchafuana kwani mpira ni amani na sio ugomvi wala chuki, kwa kufanya hivyo kutavunja matabaka yote na kuendeleza umoja.

Vitendo vyote vya rushwa ambavyo hushamiri kipindi cha uchaguzi visipewe nafasi bali sera makini zenye lengo la kuikomboa Yanga kutoka hapa ilipo.

Uwezo wa kuleta mabadiliko kwa sasa upo mikononi mwa wanachama wenyewe ambao watafanya uchaguzi Mei 5 hali itakayoleta sura mpya ya timu ya Yanga ambayo imekuwa kwenye kipindi kigumu kwenye suala la uchumi.

Kikubwa ni mipango makini kwa wagombea kuwa na nia ya dhati ya kuipigania Yanga na sio kuweka maslahi mbele haitasaidia kuleta mabadiliko ya kweli.

Ile tabia ya wengi kupuuzia kusikiliza sera na kuibukia kwenye uchaguzi ni tatizo ambalo linatakiwa lipewe tiba mapema na wanachama wenyewe.

Wanachama mnatakiwa kuangalia aina ya kiongozi ambaye mnataka na ni yule mwenye sifa ambazo zinatakiwa.

Kiongozi bora hatazamwi kwa uwezo wa pesa mfukoni wala maneno mengi mdomoni bali anapimwa kupitia uadilifu kujitoa pamoja na kutambua vema uhitaji wa Yanga.

Kwa yule ambaye anatambua mahitaji ya timu ni rahisi kwakwe kutetea na kufanya kazi bega kwa bega na wanachama kwa kuwa anaitambua vema timu yake inataka nini hivyo atafanya kile kinachohitajika.

Endapo wanachama wataamua kumchagua kiongozi kwa kutazama sura na uwezo wa fedha itakuja kuwagharimu hapo baadaye kwa kuona kwamba kile walichotarajia hakifanyika bali anatanguliza maslahi yake.

Kama atakuwa anatambua uhitaji wa timu ni rahisi kutumia muda wake kutatua matatizo ya klabu kwa wakati kwa kuwa alikuwa anatambua anachotakiwa kukifanya kabla hata hajawa ndani ya uongozi.

Uadilifu kwa wagombea pia ni miongoni mwa sifa za kiongozi ambaye ana uwezo wa kuhimili ushindani ndani ya Yanga licha ya kusuasua ila bado wanapata matokeo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic