May 21, 2019


LIGI Kuu Bara kwa sasa ipo lala salama kwani kila timu imekuwa ikipambana kutafuta matokeo hasa kutokana na ukweli kwamba kwa sasa mbivu na mbichi lazima zijulikane hakuna wa kuzuia.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni wajibu wao kutazama na kufuatilia mwanzo wa lawama hizi za waamuzi kwani wahenga walisema kwamba pafukapo moshi ujue pana moto hivyo kuna kitu huenda kimejificha nyuma za lawama za waamuzi.

Kwa timu ambazo zimepanda Daraja msimu huu ambazo ni pamoja na Namungo ya Mtwaa na Polisi Tanzania ya Arusha nasema karibuni kwenye ligi hongera kwa kupambana kufikia hapo na karibuni kwenye ligi yetu ambayo bado wafalme ni watatu wanatamba.

Ushindani wa Simba, Yanga na Azam unafurahisha kwa kiasi fulani ila unaangamiza ligi yetu kutokana na mazingira ambayo tupo hivyo kuna umuhimu wa kujiuliza tatizo lilipo ili tutafute suluhisho na sio kuishia kuzishangilia.

Tumeona kwa muda mrefu nafasi tatu za juu zimekuwa na wenyewe ambao wamejimilikisha kwa kipindi kirefu hapa inamaanisha ushindani umebaki kwa timu tatu ndani ya ligi kama tutakubali hali hii iendelee itakuwa ngumu kuyafikia mafanikio hasa kwenye soka letu.

Muda wa kubaki na mafahari wawili kwenye ligi yetu umepitwa na wakati tunahitaji kuwa na ligi bora kama ilivyo kwa wenzetu ili kufikia ushindani wa kimataifa ambao tunaufikiria siku zote hasa kwa mshindi ambaye atakwenda kuiwakilisha timu hatua za kimataifa.

Hali halisi ya ligi ambayo kwa sasa ipo lala salama inajulikana, hakuna mdhamini mkuu kwa timu zote hali inayofanya kutengeneza ufalme kwa baadhi ya timu ambazo zinajiweza huku zile ambazo hazina mdhamini mambo yao kwao yakiwa magumu.

Vilabu vingi vinashindwa kumalizia ligi katika hali ya ushindani ambao walianza nao mwanzo chanzo ni ukata, kuendesha timu sio kitu chepesi kama watu ambavyo wanafikiria kunahitaji fedha za kutosha ili kufanya mambo yaende sawa.

Tusiwapongeze Simba bila kujua kwamba wao wameandaliwa mazingira hasa kutokana na uwekezaji ambao wameufanya hali inayowafanya wawe na jeuri ya kupata matokeo ambayo wanayahitaji kwa kuwa hawana tatizo na pesa ipo je kwa wengine wenye matatizo unadhani ni nini kitatokea?

Timu nyingi zimekuwa dhaifu uwanjani hivyo ni muda wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua za kuhakikisha wanapata mdhamini msimu ujao kurejesha ushindani ambao ulianza kuonekana mwanzoni ila mwishoni wenyewe ukakata kwa baadhi ya timu.

Swali la msingi tunalopaswa kujiuliza ni wapi tumeshindwa kuiendesha ligi yetu mpaka kufikia kwenye hali hii kwa timu kuungaunga na wachezaji kuwa na maisha ambayo hayaendani na hadhi yao licha ya kufanya kazi kubwa kupambana kwenye timu zao.

Ni namna gani ligi yetu inaweza kupambana na timu kama TP Mazembe ambao ni majirani zetu na tumekuwa tukipata tabu kupata matokeo mbele yao kwa timu zetu zinapokwenda kwao?

Mapenzi ya Simba na Yanga yasitufanye tujisahau na kubaki tukishangilia timu zetu huku ubora wa ligi yetu ukizidi kuporomoka kwa kasi haipendezi kwani ligi ikiwa dhaifu na timu yetu ya Taifa pia itakuwa dhaifu.

Ligi bora hutoka kwenye timu bora ambazo zinaandaliwa mazingira bora tangu awali na ushindani unapaswa uwe kwa zaidi ya timu 10 na sio zinatazamwa timu mbili au tatu haileti maana halisi ya kutengeneza timu bora.

Tuangalie namna ligi ya England inavyodhihirisha kwamba ni bora hii inatokana na timu zake nne kutinga kwenye fainali ya mashindano makubwa mawili tofauti ukianzia lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Ligi ya Europa hii linapaswa litazamwe kama darasa.

Hii kwa wenzetu haijatokea kama ndoto bali ni utafiti ambao wenzetu walifanya kwa muda mrefu na kupata suluhisho la kuifanya ligi yao kuwa bora pamoja na uwekezaji wa kutosha kwenye timu zao za ndani.

Ndivyo ambavyo inapaswa iwe kwenye Ligi yetu ya Bongo, tuitengenezee ramani ambayo itaifanya iwe ni namba moja kwa ukanda wa Afrika Mashariki kuanzia Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na tupasue anga mpaka Congo.

Ufanisi makini utaifanya ligi yetu kuwa imara na yenye kuheshimiwa na sio kuungaunga, kama itakuwa ni mwendo wa kuendeshwa na wachezaji 10 wa kigeni hali itakuwa mbaya hapo baadaye maana hakutakuwa na vipaji kwenye timu kubwa ambazo zinatazamwa.

Kama hili litafumbiwa macho mwisho wa siku tutakuwa na timu ya Taifa ambayo itakodi wachezaji wa kigeni kama ilivyokuwa kwa Rwanda mwaka 2009 ambapo timu ya Taifa ilinunua wachezaji kutoka Congo, Nigeria na Ivory Coast kwa kuwauzia uraia.

Hii ikitokea kwetu ni aibu kwani sisi tuna watu wengi je itashindikana kuwapata wachezaji ndani ya nchi yetu? Ila kama siasa zitaendelea kutumika tusahau kuwa na ligi bora, tujifunze kwa nchi kama Ivory Coast, Ghana na Nigeria namna zinavyothamini wachezaji wa ndani na wachezaji wenye uwezo.

Somo hili lichukuliwe hatua kwa vitendo na kila mmoja atimize majukumu yake bila kujali ana mapenzi na timu gani, wakati wa kuwa na ligi bora ni sasa na kila timu ipambane kupata matokeo na sio kusubiri kubebwa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic