KIUNGO MPYA YANGA ATIBUA USAJILI
MAMBO ni moto Yanga! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiungo mpya wa Yanga, Abdulaziz Makame kutibua usajili wa klabu hiyo.
Makame ambaye amejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea Mafunzo ya Zanzibar, anadaiwa kutibua usajili wa aliyekuwa kiungo wa Singida United, Kenny Ally.
Inaelezwa kuwa sababu kubwa ni uwezo wake uwanjani hali ambayo imesababisha uongozi wa timu hiyo umpotezee kiungo hiyo ambaye pia amewahi kuitumikia timu ya Mbeya City.
Yanga ilikuwa na mpango wa kumsajili Kenny kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu katika safu yake ya kiungo. “Kwa hiyo sizani tena kama Kenny anaweza kusajiliwa ila ngoja tusubiri tuone kwa sababu nafasi ambayo anacheza hivi sasa yupo Makame na Papy Tshishimbi,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa Kenny kuhusiana na hilo alisema: “Kwa muda mrefu sasa Yanga ni kama wamenipotezea kwani ni muda mrefu sina mazungumzo nao.
“Hata sijui kuna tatizo gani kwani mpaka sasa naweza kusema hakuna kitu kipya kati yangu na Yanga. Tangu nilipozungumza nao huko nyuma sasa yapata mwezi na siku kadhaa bila ya mawasiliano.”
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema: “Usajili wa wachezaji wa ndani bado unaendelea, kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema chochote.”
Wakati dili hilo la Yanga na Kenny Ally likiota mbawa, tayari ameshasaini kuitumikia KMC.
0 COMMENTS:
Post a Comment