YANGA YASAINI JEMBE LINGINE LA STARS
YANGA wabishi balaa! Hili ndiyo neno pekee unaloweza kusema kwa sasa baada ya uongozi wa timu hiyo kufanikiwa kuinasa saini ya mlinda mlango wa timu ya Tanzania Prisons, Aron Kalambo ambaye kwa sasa yupo nchini Misri na kikosi cha Taifa Stars.
Kalambo amemalizana na Yanga kwa kandarasi ya miaka miwili ambapo anaenda kukamilisha idadi ya makipa watatu waliosajiliwa Yanga kwa ajili ya msimu ujao. Awali, Yanga iliwasainisha Farouk Shikalo kutoka Bandari FC ya Kenya na Metacha Mnata aliyekuwa Mbao FC.
Chanzo makini cha habari hii kutoka ndani ya Yanga, kimelidokeza Championi Jumamosi kuwa, klabu hiyo imefikia hatua ya kusajili makipa watatu baada ya kuachana na Beno Kakolanya aliyejiunga na Simba, Klaus Kindoki raia wa DR Congo anayerudi kwao, huku Ramadhan Kabwili akipata dili la kucheza soka nchini Sudan.
“Tulianza harakati za kuwasajili makipa hawa kimyakimya na kwamba hakuna aliyejua mazungumzo yetu na Kalambo zaidi ya kamati ya usajili na sisi viongozi tu, hivyo kwa usajili huu wa makipa sidhani kama timu yetu tena itakuja
kupata tabu kwenye nafasi hiyo ambayo kiukweli msimu uliopita tuliteseka sana.
“Tumejiridhisha sana kabla ya kukamilisha usajili wa Kalambo, Farouk na Metacha, kwani ukiangalia wote tulifikia muafaka baada ya kuridhishwa na uwezo wao uwanjani lakini pia utaona hakuna kati yao ambaye hachezei timu ya taifa, hivyo Yanga yetu itakuwa ya moto sana msimu ujao na wala hatuna hofu na kuondoka kwa Kakolanya,” kilisema Chanzo hicho.
Championi lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela ambaye simu yake iliita bila kupokelewa.
0 COMMENTS:
Post a Comment