*Walioingia mtegoni, wanapaswa kujitafakari
Na Saleh Ally
UTAMBULISHO mzuri kwa sasa ni kuwa Irene Uwoya ni mfanyabiashara anayechipukia. Mwanadada ambaye angepaswa kupongezwa kutokana na wazo lake la kuanza kuwekeza.
Yeye ameamua kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali tofauti na wengine ambao wangeamini katika kitu kimoja. Mfano yeye, ni msanii, angeweza kuona ni sahihi kubaki kama muigizaji pekee.
Ajabu kabisa, sasa Uwoya huyo amezua mjadala unaosambaa Tanzania nzima na ikiwezekana Afrika Mashariki yote akiamua kumwaga fedha wakati wa mkutano wa waandishi wa habari eti kwamba alikuwa wakiwatuza.
Waandishi baadhi walibaki kuwa waandishi wa habari katika tukio hilo baada ya kugoma kushiriki katika tendo hilo ovu na la kipuuzi kabisa lililofanywa na Uwoya ambaye hakuwa amegundua wakati huo alikuwa ni mpuuzi kabisa.
Wapo waandishi ambao waliingia katika mtego na kuonyesha wana akili zinazofanana kabisa na Uwoya, yaani za kipuuzi.
Maskini ya Mungu waandishi hao ambao wengi huenda waliingia kwenye tasnia bila ya mafunzo, au kutokuwa katika vyumba vya habari ambavyo vingeweza kuwapa mafunzo bora kupambana na hali kama hizo za wapuuzi kama Uwoya, wakaamua kugombea fedha hizo.
Wakati wengine wakigombea fedha hizo, kuna wengine waliendelea kulaani kitendo hicho kilichoonyesha ujuha wa hali ya juu na kilipaswa kupigwa vita, kulaaniwa na kulaumiwa na vyombo vyote vyenye nia ya kusimamia weledi kwenye tasnia ya habari lakini hata tasnia ya filamu yenyewe.
Kwani watu wa tasnia hawataki watu makini? Mfano Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambao wamekuwa wakishirikiana na vyombo vya habari, wanaona ni sahihi kuwa na watu aina ya Uwoya?
Ukienda katika suala la sanaa, unaona kabisa kuna kitu kinapungua kwa Uwoya na hasa ufikiri wa mambo. Kusema unawatuza waandishi wa habari ukirusha fedha utafikiri ukumbi wa dansi!
Nimeambiwa na mtu kwamba ni kiki, ilitengenezwa na yeye na huenda na kampuni aliyokuwa akiizungumzia. Binafsi niliona haiwezekani kampuni hiyo ikawa imeshiriki, kama watakuwa ni kweli walifanya hivyo, basi hawatakuwa na muda mrefu pia katika tasnia.
Huenda dharau Uwoya aliona yuko katika nafasi nzuri ya kufanya lolote akiamini mitandao ya kijamii ambako wengi waliamua kudharau waandishi wakikimbilia huko lakini baadaye wakalazimika kurudi nyuma.
Ndiyo maana unaona, baada ya kutenda kosa mbele ya wanahabari na jamii kwa ujumla, aliona sehemu sahihi ya kuomba msamaha ni kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii na kwake ilikuwa inatosha kabisa!
Wakati fulani nilifanya mahojiano ya ana kwa ana na gwiji wa muziki wa reggae barani Afrika, huyu ni Alpha Blondy. Alinikaribisha nyumbani kwake jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Jambo majawapo ambalo alilisema na sijawahi kuliacha nyuma ni kuhusiana na wasanii wengi kuamini muziki au filamu na sanaa nyingine ni kwa ajili ya kuigiza au kuimba tu na lengo ni kujifurahisha pekee.
Alpha Blondy anasema wasanii wengi wa Afrika wameponzwa au kupoteza ubora wao kutokana na kuifanya kazi ya sanaa bila ya mafunzo. Huku akisisitiza, wasanii wengi wa Ulaya wanafunzwa na hata wanajua umuhimu wa vyombo vya habari kwao na namna ya kufanya navyo kazi, ndiyo maana wanafanikiwa sana.
Huenda hili pia linawahusu wasanii wengi wenye akili kama za Uwoya, kuona mambo rahisi tu na kufanya lolote.
Wakati wengi wakimuwazia kisanii, mimi nilikuwa nikifikiria zaidi kuhusiana na biashara yake, kama kweli mfanyabiashara makini leo anaweza kusimama na kurusha fedha iwe mkutanoni au barabarani! Ukiona mtu anafanya hivyo na ana biashara yake, jiulize sana.
Biashara ya Uwoya bado ni changa, inahitaji mtu “mwenye akili timamu kibiashara” kuweza kuiendeleza. Kama unakutana naye akiwa ndio ana mtaji unaochipukia halafu anarusha fedha hivyo, basi hajitambui.
Kuna jambo ambalo bado anatakiwa kufanya kuonyesha hakuwa amekusudia. Si kwenda kuzungumza kwenye mitandao ya kijamii. Kama haitoshi, sehemu zinazohusika na sanaa, waandishi nazo zitoe matamko.
Nikiachana na Uwoya na mambo yake hayo ya ufikiri duni, waandishi walioamua kutogusa fedha zake wanastahili pongezi na kuwa mfano. Ninashukuru kulikuwa kuna waandishi watatu wa Global Publishers katika tukio hilo, wawili wa runinga na mmoja wa gazeti, hawakuingia mtegoni.
Kwa wale walioingia kwenye mtego huo wa kipuuzi na kijinga kabisa wa Uwoya, wakubali wamehusika katika kuidhalilisha tasnia hii. Wamefanya jambo la hovyo kabisa ambalo kipimo chake kinakuwa na jibu la ubabaishaji wa hali ya juu, hivyo wanapaswa kujitazama upya.
Hapa ndio sehemu ambayo tunapaswa kukumbushana, si kila mwandishi wa blogu au YouTube Channel ni mwandishi kwa kuwa tu ana uwezo wa kubwabwaja maneno, uwezo wa kununua kipaza sauti na kukipaka rangi. Uandishi ni taaluma yenye heshima kubwa na ina miiko yake.
Kwa mwandishi najua, inawezekana huna fedha mfukoni lakini haiwezi kuwa tiketi ya kukubali kudhalilishwa. Tunajua njia sahihi za kupata fedha ambazo zinaweza kulinda heshima zetu kwa maana ya taaluma, familia lakini tasnia yenyewe na nchi kwa ujumla.
Kama uligombea noti zile “haramu kwa uandishi”, basi jiulize mara zaidi ya tatu na ikiwezekana kama kweli unataka kuwa mwanahabari sahihi, basi juta, jifunze na ubadilike.
Binafsi ninalaani kwa nguvu zote kitendo cha kijinga na kinachoonyesha nguvu ndogo ya ufikiri kilichofanywa na Uwoya ambaye anastahili adhabu ili kuwazuia wengine ambao wangeweza kuwa na uamuzi unaotokana na mawazo duni kama aliofanya yeye.
0 COMMENTS:
Post a Comment