ATLETICO YAPINGA BARCA KUMNYAKUA GRIEZMANN
ATLETICO Madrid imepinga kitendo cha Barcelona kumsajili Antoine Griezmann kinyume cha sheria za usajili.
Barcelona ilidai jana imemnyakua Griezmann baada ya kulipa pauni milioni 108 (Sh. bilioni 310) kama ilivyokuwa inaelekezwa kwenye mkataba baina ya Griezmann na Atletico.
Kifungu hicho kinatoa ruhusa kuanzia Julai Mosi kwa timu yoyote yenye pauni milioni 108 kutoa fedha hizo na kumchukua mchezaji huyo. Kutokana na Atletico kugoma kupokea fedha basi Barcelona walichukua uamuzi wa kulipa fedha hizo kwenye Shirikisho la Soka Hispania kama kanuni inavyotaka.
Rais wa Atletico Madrid, Enrique Cerezo amedai kuwa Barcelona wanapaswa kulipa kiasi cha pauni milioni 180 (Sh. bilioni 517) kwa kuwa walivunja kanuni za usajili kwa kuzungumza na mchezaji mwenyewe tangu Machi wakati wakiwa na mkataba naye.
“Tuna ushahidi kuwa Barcelona walivunja kanuni za usajili kwenye ishu hii ya Griezmann, kwa hiyo tunaliangalia suala lote hili ambapo baada ya hapo tutachukua hatua stahiki,” alisema Cerezo.
Aliongeza kuwa, watapeleka suala hilo kwenye Shirikisho la Soka Hispania na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Cerezo alisema kuwa wamechukizwa na tabia ya Griezmann kwa kuikosea heshima klabu aliyochezea kwa miaka mitano.
0 COMMENTS:
Post a Comment