MANULA AVUNJA REKODI YA DAU USAJILI SIMBA
Kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars na Klabu ya Simba, Aishi Manula, anatajwa kuwa mchezaji wa kwanza mzawa kusaini kwa dau kubwa ambalo ni Sh milioni 120.
Manula ni kati ya wachezaji walioboreshewa mikataba yao baada ya ile ya awali kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Wachezaji wengine walioboreshewa mikataba yao ni Erasto Nyoni, John Bocco, Shomari Kapombe, Meddie Kagere, Clatous Chama na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kipa huyo awali alikataa dau la Sh milioni 80 alilowekewa mezani na mwekezaji wa timu hiyo bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kabla ya kukubali kusaini kwa dau hilo la Sh mil 120, awali kulikuwepo na mvutano mkubwa baada ya mabosi hao wa Simba kumtaka apunguze huku yeye mwenyewe akishikilia msimamo wake.
Aliongeza kuwa, wachezaji wengine wazawa wanaofuata kwa kusajiliwa kwa dau kubwa ni Erasto Nyoni na John Bocco wote Sh Mil. 100, Kapombe 70 na Beno Kakolanya Sh mil 50.
“Hadi hivi sasa mchezaji mzawa aliyeongoza katika dau la usajili ni Manula pekee, wapo wengine waliosajiliwa kwa dau kubwa lakini yeye ndiye anayeongoza.
“Usajili wake uliopita akitokea Azam FC alisajiliwa kwa dau la Sh Mil. 50 kabla ya kusaini hivi karibuni mwingine mpya kwa dau hilo la Sh Mil. 120.
“Hivyo ameweka rekodi kubwa kwa wachezaji wazawa katika msimu ujao na upo uwezekano mkubwa wa rekodi hiyo kutofikiwa na mchezaji yeyote katika usajili,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa mwenyekiti wa timu hiyo, Swedy Mkwabi kuzungumzia hilo alisema: “Mkataba ni siri kati ya mchezaji na uongozi, hivyo ni ngumu kuweka wazi suala hilo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment