July 8, 2019



KAZI imeanza kwa timu ya Halmashauri ya Kinondoni ‘KMC’ baada ya kumpata mrithi wa mikoba ya aliyekuwa kocha wao Etienne Ndayiragije ambaye kwa sasa yupo na mabingwa watetezi wa kombe la Kagame Azam FC.

Jackson Mayanja amebeba mikoba ya Ndayiragije na amepewa kandarasi ya mkataba wa mwaka mmoja ambao una kipengele cha kuongeza iwapo atakidhi vigezo ambavyo vimewekwa na uongozi wa KMC.

Ikumbuwe kwamba si mara ya kwanza kwa Mayanja kuja Bongo kufundisha kwani alishawahi kuifundisha Kagera Sugar, Coastal Union, Simba na sasa ameibukia ndani ya KMC ambayo inashiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza.

Mayanja ana mengi ambayo anafikiria kuyafanya ndani ya KMC, huyu hapa anafunguka:-

“Kuna vitu vingi ambavyo kocha ni lazima awe navyo kwenye kazi yake ambayo anaifanya kati ya hivyo ni suala la makombe hasa kwa mashindano ambayo anashiriki hivyo malengo makubwa baada ya kutua hapa ni kuanza kupanga kikosi imara kwa ajili ya ushindani uliopo kwenye ligi.

Kwa nini KMC?

“Ni miongoni mwa timu bora hasa ukizingatia namna ya uendeshaji wao hivyo ni miongoni mwa sababu ambazo zimenivutia kusaini ndani KMC.

“Viongozi ambao walizungumza nami awali walinipa picha kamili ya kikosi cha KMC na namna inavyojiendesha nilipenda na nikawa tayari kuitumikia.

Hesabu kubwa ni zipi?

“Kwa muda huu itakuwa ni mapema kuzungumzia kutokana na ukweli kwamba bado sijakaa na kikosi na kutambua aina ya wachezaji ambao nipo nao kwenye timu, ila nina imani haitakuwa ngumu kwangu kwenda nao sawa.

“Kama timu imemaliza ligi ikiwa nafasi za juu inatoa picha kwamba ipo imara na ina wachezaji wapambanaji nina imani watanifaa kwa ushindani.

Aina ipi ya wachezaji ungependa kuwa nao?

“Wachezaji wote wenye uwezo na nidhamu nje na ndani ya uwanja ni siri kubwa ambayo imejificha kwenye mafanikio ya timu inayotafuta mafanikio.

Unaweza kuendana na sera ya KMC?

“Uendeshaji wa KMC hauna tofauti kubwa na timu ya KCC ya Uganda ambayo nayo ni ya manispaa hivyo nina uzoefu hakuna utofauti na hapa ambapo nipo kwa sasa.

Unawaamba nini wana KMC?

“Ahadi yangu ni kufanya makubwa ndio maana nimekubali kutua hapa kufanya kazi, kikubwa ni sapoti, ushirikiano na juhudi katika kila jambo.

Ushindani wa Ligi ya Tanzania unauzungumziaje?

“Nimefanya vizuri kwenye timu nyingi hapa Bongo na ipo wazi hasa nilipokuwa hapa, hivyo hainipi taabu kwangu kuanza upya na timu nyingine, napenda mpira na ninaweza kufudisha hivyo nitapambana kuleta ushindani.

Muda gani utakutosha kuandaa kikosi?

“Sitachukua muda mrefu nitafanya makubwa ndani ya muda mfupi ambao nitakuwa na kikosi ukizingatia kwamba mpira una lugha ambazo zinaeleweka.

“Najua namna bora ya kuitengeneza timu na itafanya mambo mengi makubwa, nitatambulisha mradi mpya na wenye matokeo chanya nikiwandani ya KMC na kila mmoja atajua kwamba huu ni utamaduni wa KMC.

“Nina furaha kuwa ndani ya KMC nina imani ya kubadili mfumo kwa muda mfupi ni jambo la kusubiri na kuona yale yatakayotokea.

Una amini katika makosa kwenye mpira?

“Makosa yapo, ila kwangu ni sehemu ya kujifunza na kusonga mbele kwa manufaa ya timu na mashabiki kiujumla.

Historia yako ya kutwaa makombe ipoje?

Makombe mawili kwenye ligi nilipokuwa naifundisha URA ya Uganda yananipa nguvu kuamini kwamba  nina uwezo wa kutwaa kombe hata nikiwa ndani ya KMC.

Utasajili wachezaji wako ndani ya KMC?

“Nadhani sio jambo jema kwa kocha kuondoka na wachezaji, labda benchi la ufundi.

“Wachezaji wapo na timu, hivyo sina mpango wa kuleta wachezaji wapya kutoka timu yangu ya zamani nitawakuta labda benchi la ufundi hilo lipo mikononi mwangu.

Hesabu za kimataifa je zipoje?

“Uzoefu kwenye michuano ya kimataifa ninao na ukizingatia timu ambayo nimechezea ni ya Manispaa hivyo nina amini itakuwa ni kazi nyepesi kwangu kufanya vizuri kimataifa.

“Michuano ya Kagame nitaitumia kuandaa kikosi cha mauaji kitaifa na kimataifa, ratiba yangu ni ngumu na muda ni mfupi hivyo nitapata kikosi bora ambacho nitakitumia ndani ya ligi pamoja na michuano mingine,” anamalizia Mayanja ambaye jana mchezo wake wa kwanza aliambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Atrabala.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic