MSIMU mpya
wa 2019-20 utakuwa ni moto wa kuotea mbali kutokana na timu zote kujipanga vema
msimu huu wa usajili ili kufikia malengo ambayo wameyapanga.
Mpaka sasa
hekaheka za usajili zinaendelea huku kila timu ikitamba kufanya usajili kwa
matakwa ya ripoti ya mwalimu na wana imani kubwa kwa wachezaji ambao wamesajiliwa.
Wengi wao
waliopata ulaji, rekodi zinaonyesha kwamba walizisumbua Simba na Yanga na kwa sasa tayari wamepata ulaji kwenye timu nyingine kama ifuatavyo:
Kassim Khamis
Nyota huyu
amesajiliwa na Azam FC kwa kandarasi ya miaka miwili ametoka Kagera Sugar
inayoshikilia rekodi ya kuvuna pointi sita mbele ya Simba ya Mbelgiji Patrick
Aussems msimu wa 2018-19.
Kwenye
mchezo wa kwanza walipokutana na Simba uwanja wa Kaitaba alifunga moja ya bao
kwenye ushindi wa mabao 2-1 hali iliyompandisha chati na kuitwa ndani ya Azam
FC, pia Simba na Yanga zilikuwa zinaiwainda saini yake.
Idd Suleiman
Mshambuliaji
mpya wa Azam FC, amesaini kandarasi ya miaka miwili ametokea Mbeya City.
Deogratius Munish ‘Dida’ anaijua shughuli yake kwani alimtungua bao moja msimu
uliopita mchezo ulichezwa uwanja wa Sokoine licha ya Simba kushinda mabao 2-1.
Ramadhan Kapela
Mshambuliaji
huyu nyota yake iling’ara kwenye mchezo wao dhidi ya Simba alipokuwa Kagera
Sugar ambapo alihusika kwenye mabao yote mawili, kwa kutoa pasi ya bao kisha naye
akafunga bao lililoipa Kagera Sugar pointi tatu uwanja wa Kaitaba mbele ya
Simba.
Kwa sasa
ujuzi wake utaonekana na watoto wa mjini Kino boys kwa kuwa amesaini kandarasi
ya miaka miwili.
Jacob Massawe
Alikuwa
nahodha wa Stand United mchezo wa kwanza wa Yanga kupoteza ilikuwa uwanja wa
Kambarage ambapo Jacob Massawe alifunga bao hilo dakika ya 88, kwa sasa amejiunga
na Gwambina FC kwa kandarasi ya mwaka mmoja na timu yake ya Stand United nayo
ilishuka daraja.
Salim Aiyee
Alikuwa na
msimu mzuri kwa mwaka 2018-19 aliifunga Yanga nje ndani kwani mchezo wa kwanza
uliochezwa uwanja wa Mwadui Complex licha ya Yanga kushinda mabao 2-1 na ule wa
marudiano uliochezwa uwanja wa Taifa alifunga bao licha ya Yanga kushinda mabao
3-1.
Kwa sasa
amesaini kandarasi ya miaka miwili ndani ya KMC, alimaliza msimu akiwa amefunga
jumla ya mabao 18 dili lake la kutimkia Swedeni ilibuma kwa kukosa viza.
Vitalis Mayanga
Alizua gumzo
kwa kuwapiga chenga magolikipa wawili wa Yanga ambapo alianza na Beno Kakolanya
ambaye yupo Simba kwa sasa, kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Taifa kabla ya
kutoa pasi ya bao na akamalizia na mlinda mlango Klaus Kindoki uwanja wa
Nangwanda na alifunga bao.
Kwa sasa ni
mali ya KMC alimaliza msimu akiwa na mabao 10, alisajiliwa kimkakati na Simba
usajili wa awali kabla ya mkataba wake kuvunjwa.
Ally Ally
Beki mpya wa
Yanga wengi wanapenda kumwita ‘Mwarabu’ amesaini kandarasi ya miaka miwili
ndani ya Yanga, licha ya kujifunga bao 1 alipokuwa anaitumikia KMC ilipocheza
dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa bado uwezo wake ulikuwa ni tishio kwa wapinzani.
Simba na
Yanga hawakuwa na raha anapokuwa uwanjani kwani alikuwa ni mtibua mipango kwa
hatari nyingi ndani ya uwanja, kwa sasa ni mali ya Yanga.
Raizin Hafidh
Kasi yake
akiwa uwanjani na uwezo wa kujiamini viliipa taabu safu ya ulinzi ya Simba na
aliwafunga nje ndani kila walipokutana kwa kuanza mchezo wa kwanza uwanja wa
Mkwakwani ambapo Simba ilishinda kwa mabao 2-1 na ule uliochezwa uwanja wa
Taifa ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 8-1.
Kwa sasa
amepewa kandarasi ya mwaka mmoja ili kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Gwambina
FC ambacho kinashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment