July 9, 2019


KWA asilimia kubwa, mpaka sasa kikosi cha Simba kimekamilika kwani kutokana na aina ya wachezaji iliowasajili, vinaweza kutengenezwa vikosi zaidi ya vitatu na vyote vikawa moto wa kuotea mbali.

Simba ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara, mpaka jana Jumapili ilielezwa kuwa imekamilisha usajili wa wachezaji wapya kumi ambapo sita ni wa kimataifa na wanne wazawa.

Wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa kipindi hiki ni Francis Kahata raia wa Kenya, Deo Kanda (DR Congo), Sharaf Shiboub (Sudan), Gerson Fraga Vieira, Tairone Santos da Silva, Wilker Henrique da Silva ambao wote ni raia wa Brazil.

Wazawa ni Kennedy Juma kutoka Singida United, Ibrahim Ajibu, Beno Kakolanya na Gadiel Michael ambao wote ni kutoka Yanga. Kwa majembe hayo ambayo Simba imesajili, vinaweza kutengenezwa vikosi vitatu kwa kutumia mifumo mitatu tofauti ambayo ni 4-4-2, 3-5-2 na 4-5-1.

Katika kikosi cha kwanza kinachoweza kutumia mfumo wa 4-4-2, kinaweza kuwa hivi; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Gerson Fraga Vieira, Pascal Wawa, Sharaf Shiboub, Ibrahim Ajibu, Wilker Henrique Da Silva, Deo Kanda, Meddie Kagere  na Francis Kahata.

Cha mfumo wa 3-5-2, kinaweza kuundwa na Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude, John Bocco, Tairone Santos da Silva na Clatous Chama.

Huku kile cha tatu kitakachotumia mfumo wa 4-5-1, kinaweza kupangwa hivi; Ally Salum, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Gerson Fraga Vieira, Sharaf Shiboub, Jonas Mkude, Deo Kanda, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.

Hata hivyo, ukiachana na wachezaji ambao wanaunda vikosi hivyo bado kuna wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa ambao watakuwa wamekaa benchi wakisubiri kuingia uwanjani kuchukua nafasi za wale watakaoonekana kuchoka.

Kutokana na hali hiyo, msimu ujao Simba inaonekana itakuwa na kikosi tishio na kipana ambacho kitafanya kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems kuwa na uhuru mpana wa kupanga kikosi na kila mchezaji atakayempatia nafasi ya kucheza akafanya vuzuri.

Kwa hali hiyo, wapinzani wa Simba katika michuano ya Ligi Kuu Bara pamoja na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wajipange kwelikweli kukumbana na mziki mnene pindi watakapokutana na moja kati ya vikosi hivyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic