August 4, 2019





Na Saleh Ally
SIKU tatu zimepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli alipokuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha 21st Century Food and Packaging Limited kilicho chini ya Makampuni ya MeTL Group.


Kiwanda hicho kilizinduliwa jijini Dar es Salaam na Rais Magufuli kuhudhuria. Mwenyeji wake alikuwa ni Mwenyekiti wa Makampuni ya MeTL, Mohamed Dewji ambaye ni bilionea kijana zaidi barani Afrika na maarufu sana nchini kutokana na soka.


Kwa sasa Dewji ni mwekezaji katika moja ya klabu kubwa nchini, Simba. Na utaona pamoja na mengi yaliyokuwa yameongelewa, wanamichezo wengi walijadili ile kauli ya Rais Magufuli aliyoitaja Simba na Yanga.



Wakati wa hotuba yake, kidogo Rais Magufuli alizigusa Yanga na Simba akisema: “Wawekezaji wa ndani na nje this is your time, ndugu yangu Dewji usiwe mnyonge. Na kama unavyowafanyia mazuri timu ya Simba na maslahi ya wafanyakazi wako pia endelea kuyajali, hata Yanga pia uwakumbuke.”


Kauli hii ya Rais kwa umbali inaweza kuonekana kama utani kidogo na hasa kwa kuwa ndani yake kuna Simba na Yanga lakini ukitulia utagundua kwamba Rais Magufuli anajua kinachoendelea katika michezo ya Tanzania.


Anajua kwa kuwa ametamka kuwa anajua Dewji anawafanyia mazuri klabu ya Simba, kidogo akaongeza asiwasahau na Yanga. Kujua kuwa kuna mazuri yanafanyika Simba, ni jambo la kupima kwa sisi wanamichezo.



Kumekuwa na pingamizi kadhaa kuhusiana na uwekezaji ndani ya Simba na wako wengi wamekuwa wakiamini kuna mkono wa Serikali, jambo ambalo linafutika kabisa kwa kauli ya Rais.


Hii inaonyesha Serikali ipo tayari kwa ajili ya uwekezaji lakini kikubwa kinachotakiwa hasa katika awamu hii ya tano ni suala la kufuata utaratibu sahihi ili kutimiza yale ambayo ni sahihi.


Kuna kila sababu ya kujifunza, kwamba kama Dewji atafanikiwa kuwekeza na mwisho kufanya vizuri, itachangia kufanya mabadiliko. Hata kama kutakuwa na maoni tofauti lakini vizuri kujaribu kutoa nafasi na uwekezaji ukafanyika.


Kikubwa kabisa ambacho kibaki kama msingi sahihi ni wanaopita katika mpito huu kwenda katika uwekezaji huo ni kufuata utaratibu sahihi ili kuepusha kuacha maswali yasiyojibika nyuma.


Huenda maneno ya Rais kuhusiana na Simba na Yanga yanaweza kuwa baraka lakini sote tunaujua utaratibu wa Rais Magufuli, ni kufuata utaratibu bila ya kupindisha mambo.


Mimi nilijifunza zaidi na kutafakari upande wa pili pale Dewji alipokuwa akielezea makampuni ya MeTL yalivyofanikiwa katika kutoa ajira kwa takriban Watanzania 30,000 huku Dewji akisisitiza: “Na ndiyo kampuni kubwa zaidi hapa Afrika Mashariki na Kati ikiongoza kutoa ajira kwa watu wengi zaidi.”


Hapa utaona kwamba, tayari Dewji ana uzoefu mkubwa, akiwa mmoja wa wawekezaji ndani ya Klabu ya Simba, itasaidia kuutumia uzoefu wake wa kuongoza kampuni iliyotoa ajira nyingi zaidi kuisuka Simba itengeneze ajira na faida.


Kilichonivutia zaidi aliposema: “Kampuni ilianza uwekezaji mnamo mwaka 2005, ambapo ilianza na kiwanda chenye uwezo mdogo wa kusaga tani 240 kwa siku za ngano pamoja na uwezo wa kuhifadhi hadi tani 20,000 za nafaka. Kwa hivi sasa kiwanda kimeboreshwa kwa kuwekeza kwenye mitambo mikubwa iliyogharimu jumla ya shilingi bilioni 105 na inatumia teknolojia ya kisasa zaidi.”


Hii maana yake uzoefu kwamba mwekezaji kama Mo Dewji ana faida zake, kuanzisha kitu na kukiendeleza. Aliyakuta makampuni ya MeTL lakini amefanikiwa kuyaendeleza zaidi. Ana nafasi ya kujua njia sahihi ya Simba inapopaswa kupita.


Dewji alizungumzia kuhusiana na uwekezaji wa awamu ya tano akisema hivi mbele ya Rais Magufuli: “Uwekezaji huo umefanyika chini ya Awamu ya tano. Leo tunashuhudia kiwanda cha kusaga mahindi chenye uwezo wa kusaga tani 300 kwa siku; kiwanda cha ngano chenye uwezo wa kusaga tani 1,240 kwa siku; Mitambo yenye uwezo wa kupokea tani 600 kwa saa za nafaka; na uwezo wa kuhifadhi nafaka hadi tani 50,000.


Pia akapiga hesabu kuhusiana na namna walivyoweza kupunguza bei ya unga kwa kilo kutokana na kazi nzuri ya uwekezaji ya Rais Magufuli katika reli pia akipongeza umeme na barabara.


“Nikupe mfano tu. Kwa upande wa reli, Mh Rais, ningependa kukupa mfano mmoja tu; sisi tunazalisha na kusafirisha ngano kwenda kuiuza Kigoma. Hapa Dar-es-Salaam, unga wa ngano tunauza shilingi 1,090 kwa kilo. 


Gharama ya kusafirisha kwa barabara hadi Kigoma ni shilingi 220 kwa kilo, ukilinganisha na shilingi 100 kwa kilo kwa usafiri wa reli. Tukizingatia kuwa gharama ya kusafirisha kwa reli ina unafuu kwa takriban asilimia 80, kwa hiyo mwananchi wa Kigoma atapata unafuu wa shilingi 120 kwa kilo.”


Maneno ya Dewji yanafikirisha, kwangu niliona yanashawishi na ikiwezekana katika mpira tunahitaji watu wa namna hii. Wawe kwenye suala la uwekezaji na vinginevyo lakini kuwa na wafanyabiashara wanaopeleka mambo yao kwa hesabu za mabadiliko na kusonga mbele, ni jambo litakalobadilisha mambo.


Tumekubaliana Simba na watani wao Yanga wana mtaji mkubwa wa watu, mtaji huu umekuwa ukitumika vibaya kwa miaka nenda rudi na ndio maana klabu hizo zimeendelea kuonekana ni za kawaida hadi leo.

Kama hesabu za kibiashara anazopiga au kuzizungumzia Mo Dewji zingekuwa zimeanza kutumika ndani ya klabu hizo angalau miaka 10 iliyopita, basi kungekuwa na hatua kubwa iliyopigwa.



Inawezekana kungekuwa na mengi hasa ya kuzungumzia yakionyesha hatua zilizopitiwa kama ambavyo Dewji alivyoweza kuzungumzia kuhusiana na Makampuni ya MeTL.
Dewji amemhakikishia Rais Magufuli kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, MeTL Group wana mpango wa kuwekeza shilingi bilioni 520 kwenye viwanda vinavyoongeza thamani ya Tanzania.


Muwekezaji wa shillingi bilioni 520, ninaamini anaweza kujua afanye nini kuhakikisha angalau Sh bilioni 10 iliyowekezwa sehemu, ikue namna gani.


Tayari Serikali imepitisha uwekezaji ndani ya Simba na kutangaza utaratibu, Mo Dewji ameshaahidi hatarudi nyuma na kuwatoa hofu Wanasimba. Basi vizuri akatekeleza kauli yake na kushirikiana na Wanasimba wenzake kuleta hayo mabadiliko ili yakifanikiwa yawe funzo la kuanzisha mabadiliko mengine ndani ya mpira wetu ambao unahitaji mabadiliko ili kukua na hili halipingiki.




1 COMMENTS:

  1. Brother Saleh kila mtu au mtanzania anajua kuwa Mo atafanikiwa Simba ila kinachoendelelea kwa wale wanaomuekea vikwazo ni wivu na roho mbaya kutotaka kuiona Simba inapiga hatua. Kwa kauli ya muheshimiwa raisi Magufuli ya kwamba Mo wakumbuke na Yanga pia ni dhahiri anajua jinsi gani Yanga inavyoteseka bila ya uekezaji na kwa kweli Yanga wataendelea kuteseka.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic