MUZIKI unalipa! Si jambo geni kusikia wasanii wanamiliki majumba na magari ya kifahari kutokana na mauzo ya kazi zao na hivyo ndivyo ilivyo kwa mkali wa Bongo Fleva, Aslay Isihaka ambaye sasa fedha imemtembelea.
Mdau wetu mzuri ameshusha ubuyu kama wote kwamba, Aslay kwa sasa ni miongoni mwa wasanii ‘wanaokula wanachotaka’ na siyo kula anachopata, anayeishi kwenye mjengo wa ghorofa uliopo maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar.
“Eeeh mjini hapa kama unaishi kwenye ghorofa tena maeneo ya ushuani unafikiri ni gharama kiasi gani? Ghorofa la ushuani huwezi kulifananisha na ghorofa lililopo nje ya mji kama vile Kibaha na kwingineko, iwe ni la kupanga au kumiliki,” alieleza mdau wetu.
MKOKO WAKE
Mdau huyo hakuishia hapo, alizidi kushusha ‘vesi’ kuwa, mbali na Aslay kuishi kwenye mjengo huo ushuani, bado anatembelea ndinga kali aina ya BMW X3.
“Unajua kwa msanii kama yeye ambaye alitoka chini, akaingia kwenye Kundi la Yamoto, akatoka na kuanza kujitegemea hadi leo hii kufikia mafanikio aliyonayo si jambo dogo.
“Huwezi kumfananisha na wasanii ambao wanasimamiwa na menejimenti kubwa ambao hata magari yao unaweza kukuta wanapewa kwa mkataba fulani,” alisema mdau huyo.
MSAADA KWA NDUGU
Aidha, mdau wetu huyo alisema mbali na kujitegemea kwa maana ya kula, kunywa na makazi mazuri pia amekuwa msaada mkubwa kwa ndugu zake ambao wanamtegemea.
“Anawasadia pia ndugu zake kadiri ya uwezo wake, ni kijana ambaye anajituma na Mungu anazidi kumbariki siku hadi siku,” alisema.
NI NYUMBA YA KUPANGA?
Risasi Jumamosi lilijaribu kumbana mtoa habari huyo ili kuweza kujua nyumba hiyo anayoishi Aslay amepanga au vipi lakini suala hilo hakuwa na majibu nalo.
“Hilo sasa labda umuulize mwenyewe mimi ninachojua tu ni kwamba anaishi ushuani, ana mkoko wa maana na akaunti yake benki pia si haba,” alisema.
HUYU HAPA ASLAY
Risasi Jumamosi lilimvutia waya Aslay ili kumsikia anazungumziaje mafanikio hayo aliyoyano pamoja na mipango yake ya baadaye katika muziki.
Alipopatikana alisema anaona bado hajafika mbali sana kimafanikio lakini kwa kidogo alichonacho anamshukuru Mungu kwani ndiye mtoa riziki.
“Namshukuru Mungu kwa hiki kidogo nilichonacho. Ni kidogo tu hiki bwana,” alisema Aslay.
AZUNGUMZIA GARI
Kuhusu BMW X3, Aslay alikiri kuwa analimiliki na kwamba amelinunua kwa kipato anachokipata kutoka kwenye shoo pamoja na vyanzo vyake vingine ikiwemo mtandao wa kijamii wa YouTube.
“X3 (BMW) ni yangu kama unavyoona, nimekuwa nikiiposti sana tu kwenye akaunti zangu za mitandao ya kijamii hususan Instagram, kuhusu bei nafikiri inajulikana sitapenda kuitaja,” alisema Aslay.
Licha ya Aslay kutotaka kutaja thamani ya ndinga hilo, Risasi Jumamosi linafahamu kwamba bei yake si ya kitoto, magari ya aina hiyo yametofautiana kulingana na muundo pamoja na mwaka lililotengenezwa gari husika.
Kwa fedha za madafu, ndinga hiyo inacheza kuanzia shilingi milioni 50 na kuendelea.
NYUMBA JE?
Kama ilivyokuwa kwenye gari, kwa upande wa nyumba ya ghorofa anayoishi alikiri kuwa ndiyo anayoishi lakini hakutaka kufafanua kwa undani kama amepanga au anaimiliki.
“Hiyo nyumba ninayoishi ni ileile ya pale Mbezi Beach Kwa Zena lakini nimeona kuna watu mitandaoni wanachanganya baada ya mimi kuposti nikiwa nje ya mjengo mwingine wa kifahari.
UFAFANUZI
“Iko hivi, pale ambapo nilipiga picha maeneo ya Mbezi Beach (tazama picha ukurasa wa mbele) ni kwa rafiki yangu ambaye anaishi Uingereza, alikuja akafikia kwenye zile apartment nikaenda kumtembelea kwa hiyo siyo kweli kuwa nimehamia kwenye huo mjengo,” alisema Aslay anayesumbua na wimbo wa Bembea alioshirikiana na Ally Saleh Kiba ‘Alikiba’.
NINI SIRI YA MAFANIKIO?
Alipoulizwa kuhusu siri ya mafanikio aliyonayo sasa kwenye muziki na maisha kwa jumla, Aslay alisema ni kumtegemea Mungu na kufanya kazi kwa bidii.
“Hakuna kitu cha ziada zaidi ya Mungu na bidii, nimetoa nyimbo nyingi sana ambazo ni ‘hits’, napata fedha YouTube kwa sababu zinatazamwa na watu wengi,” alisema Aslay.
NYIMBO ZA ASLAY
Baadhi ya nyimbo kali za Aslay ambazo zimetazamwa na watu wengi zaidi katika Mtandao wa YouTube ni pamoja na Natambaa ambao umetazamwa na watu milioni 8.9, Usinitie Doa (milioni 7.2), Likizo (milioni 5.7), Ananikomoa (milioni 3), Nyaku Nyaku (milioni 2.6), Chuki (milioni 1.1) na Nichombeze (milioni 1).
AMWAGIWA SIFA
Hata hivyo baadhi ya watu kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii wamekuwa wakipongeza mafanikio ya Aslay na kumtaka aendelee kujituma zaidi.
“Wengi tulijua baada ya Yamoto Band kufa na yeye atapotea mazima lakini jitihada hazijawahi kumtupa mtu,” alisema mchangiaji mmoja kwenye akaunti yake ya Instagram.
Asnattz wa Sinza aliandika katika ukurasa wake wa Facebook ujumbe ulioambatana na picha ya Aslay ukisomeka: “Wasikutishe muziki unajua na ridhiki ni popote.”
0 COMMENTS:
Post a Comment