September 15, 2019


KOCHA wa Yanga Mwinyi Zahera amewasisitiza mashabiki wa timu hiyo kutembea kifua mbele wala wasitishwe na sare ya jana ya bao 1-1 dhidi ya Zesco kwenye Uwanja wa Taifa.

Yanga ililazimishwa sare hiyo kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku timu hizo zikirudiana Septemba 27 ugenini mjini Ndola. Bao la Yanga lilifungwa na Patrick Sibomana dakika ya 25 kwa mkwaju wa penati huku lile la Zesco likipachikwa na Thabaan Kamusoko kwa shuti kali la nje kidogo ya 18 dakika ya 90+4.

Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili isonge mbele kwenye hatua ya makundi. Lakini ikishindwa kupata matokeo kwenye mchezo huo itaangukia katika hatua ya mtoano katika Kombe la Shirikisho kuwania kuingia kwenye makundi.

Licha ya mashabiki wa Yanga kuonekana kunyongea kutokana na bao la usiku pamoja na kejeli za wenzao wa Simba ambao walikuwa wakiishangilia Zesco ya George Lwandamina, Zahera amewatoa hofu. Zahera amesisitiza kwamba; “Kutoka na sare hii haimaanishi kwamba tumetoka, kwa vile tuna uwezo wa kwenda kushinda bao 1 ugenini kama tulivyofanya kwa Township Rollers.”

“Kwanza leo(jana) nitalala usingizi kwa vile timu yangu imecheza vizuri na wachezaji wamefuata maelekezo yangu, walikosa bahati tu kwani walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuweza kuingiza goli,”alisisitiza.

“Hata kama tungeshinda kwa lile bao moja lazima kule tungelazimika kwenda kushinda bao lingine ili tuwe na uhakika wa kupita, kwa hiyo sare hii haijabadilisha chochote sababu bado mchezo unaendelea,”aliongeza Zahera kwa kujiamini.

4 COMMENTS:

  1. Uko sahh kikubwa wafungaji na beki za pembeni uziandae vizuri na vilivyo wakawaida sana wale.

    ReplyDelete
  2. hata ubingwa wa TPL mwaka jana ulisema hivyo wakati mahesabu yalikuwa hayaendi kabisa..Kule ni Zambia na sio Botswana

    ReplyDelete
  3. Huyu ni Mwanasaikolojia, sio kocha wa mpira. Anaweza akakupa moyo kuwa utapona hata akiona unatupa mikono na miguu ikiwa ishara ya kukata roho. Mzee Zahera, kwa Straika wako hawa walivyocheza jana hapa Taifa, kule Zambia Golikipa wa Zesco ataingia uwanjani na kitanda cha kulalia. Kwa upande wenu, mkifungwa goli 2 itabidi mshukuru sana. Kule mnaenda kulala 4 : 0.

    ReplyDelete
  4. Wanayanga wameumia kweli....sasa sina sababu ya kuwalaumu kwanini wanakuwa baridiiii....Timu inawaangusha....yaani watu wanajitokeza kwenye mechi na matokeo mfukoni na wakiwa wanajiamini mno na Kocha wao anawaaminisha ushindi mwisho wa siku sare au kufungwa....ule utamaduni wa Yanga (umoja wa kuhakikisha mechi Inachezwa nje ndani haupo)....kuna sehemu au kuna kitu hakipo sawa tatizo haijulikani ni kitu gani hicho au sehemu ipi inaleta "nuksi".....Nilisema na nitaendelea kusema kama hakuna mabadiliko katika ufundishwaji......MAUMIVU YATAENDELEA KWENYE MECHI ZILIZOBAKI WAKIANGUKIA KWENYE KUCHEZA MTOANO ILI KUFUZU CAF FEDERATION CUP NA HATA KWENYE LIGI.....TATIZO HAMTAKI KUCHUKUA HATUA.....SASA MSISEME HATUJAWAAMBIA!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic