September 18, 2019


LICHA ya Klabu yake ya KRC Genk kufungwa mabao 6-2, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta,  ameweka rekodi ya aina yake ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga goli kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya!

Katika mechi hiyo iliyokuwa ikifuatiliwa na maelfu ya Watanzania duniani kote, ilichukua dakika 53 kwa Samatta kupata goli lake la kwanza kwenye Uefa Champions League akiifunga RB Salzburg katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi hiyo kubwa duniani.

Matokeo hayo pia yamemfanya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kupata bao kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo.

Ushindi huo wa mabao sita ulitoa ishara kwa Salzburg kuuanza msimu kwa nguvu.

Dakika ya 80, Samatta alipigwa kadi nyekundu na kuondoa matumaini ya Watanzania lakini refa alipokwenda kutazama kwenye mfumo wa VAR akagundua kosa lile halikuwa na adhabu ya kadi nyekundu hivyo akampa kadi ya njano.

Matokeo yalikuwa hivi: RB Salzburg 6-2 KRC Genk (Haland 2′ 34′ 44′
Hwang 36′
Szoboszlai 45+2′
Ulmer 66′) (Lucumi 40′
Samatta 52′).

Tanzania ni ya Mbwana Samatta, Tanzania ni ya Mbagala na Tanzania ni mtu mmoja linapokuja suala la soka kwenye nyanja za kimataifa. Mbwana Samatta ndiye aliyebeba ndoto za nchi hii katika kuwanyanyua na kutoa mwanya utakaowaruhusu Watanzania wengine kunufaika, kufika mbali kupitia soka.

Ni ndugu yetu ambaye miguu yake tangu akiwa na Simba mpaka TP Mazembe aliijengea urafiki na nyavu na mahusiano yao yakawa imara kuliko marafiki wengi alionao mpaka ikampatia visa ya Ubelgiji na sasa yuko na klabu ya KRC Genk.

Mchezaji bora wa Afrika wa wachezaji wa ndani mpaka mchezaji bora mwenye asili ya Afrika anayecheza ligi ya Ubelgiji, yote yaliyoandikwa na yote yakawa sehemu ya ndoto ya taifa na ndoto zake binafsi.

Hata hivyo inawezekana kabisa yote haya kwa pamoja yalikuwa aina ya mapishi huku chakula pekee Watanzania walitamani kukila kutoka kwake ikawa ni ligi tano kubwa. Chakula ambacho wanaweza kukipata kwa urahisi kutoka sebuleni kwao kupitia runinga, chakula ambacho kinafuatiliwa duniani kote, yaani ligi kuu ya England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa na Italia.

Kila mtu alitamani kuona Samatta akikimbizana kwenye magoli na Aubameyang, Salah na Mane. Acheze mechi na Ronaldo na kila mmoja afunge au afunge goli kwenye mchezo ambao Messi hatofunga kabisa na pia afunge goli ambalo lingeweza kumkera Neymar pale Ufaransa.

Haya ni maisha ya ndoto, maisha ambayo Watanzania tumeungana kwa maombi tukihitaji baraka juu ya Mbwana ili afike mbali huku yote haya yakuonekana kutowezekana walau kwa msimu huu hata baada ya msimu uliopita kumfunga Karius kipa wa zamani wa Liverpool.

Kuna nafasi kubwa ziaidi kwa Mbwana Samatta, fursa bora zaidi kama utakuwa na kiwango cha msimu uliopita, bahati nzuri kaanza msimu kwa kasi ileile na sasa mwaka huu kikombe cha dhahabu kipo mbele yake kinaitwa klabu bingwa barani Ulaya.

3 COMMENTS:

  1. Wewe Saleh Jembe acha kuongea uongo mchezaji wa kwanza wa Africa mashariki kufunga kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE alikuwa Victor Wanyama wakati akichezea Celtic, 07/11/2012 wakati Celtic ilipoifunga Barcelona goli 2-1. Kama hamjui bora muulize kabla ya kutuma utumbo wenu. Yaani nyinyi kila siku lazima mdanganye watu halafu mnajiita waandishi wa habari.

    ReplyDelete
  2. Hivi mariga hakufunga goal lolote uefa...mc donald mariga bro wa wanyama....

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hakufunga goli ila alikuwa mkenya wa kwanza kucheza uefa na kushinda kombe la Uefa, Intermilan alivyomfunga bayern katika fainali

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic