BOCCO NJE MWEZI MZIMA, KAGERE NAYE MAJANGA MATUPU
Majanga juu ya majanga! Ndiyo neno jepesi unaloweza kulitumia kwa mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Bocco ambapo licha ya kukaa nje kwa wiki kadhaa amekumbwa tena na balaa ambapo safari hii atakosekana uwanjani kwa mwezi mzima.
Nahodha huyo wa Simba yuko pembeni ya kikosi hicho tangu kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kutokana na kukumbwa majeraha ya goti.
Straika huyo wiki iliyopita alirejea na kuanza mazoezi mepesi lakini jana Jumanne hakuwa sehemu ya wachezaji waliofanya mazoezi kutokana na kuambiwa akae nje kwa mwezi mzima.
Akilithibitisha hilo, Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema straika wake huyo atakaa nje kwa muda huo kutokana na kupewa taarifa na daktari wa timu hiyo kuwa jeraha lake ni kubwa.
“Bocco hajaonekana leo kwa sababu anatakiwa kuwa nje kwa wiki nne kwa sababu ya ukubwa wa tatizo lake tofauti na vile ambavyo tulifikiria awali.
“Daktari aliniambia jana (juzi) baada ya kuongea naye kuwa Bocco hataweza kucheza kwenye mechi zetu hapa karibuni na anahitaji kuwa nje kwa muda huo na akimaliza ndiyo ataungana na wenzake.
“Lakini siyo yeye kwani Kagere (Meddie) naye hayupo leo kwa sababu ana tatizo la majeraha lakini siyo makubwa.
Kagere aliumia mechi iliyopita na nilimpumzisha apate muda wa kukaa sawa kwa sababu ndiye straika pekee ninayemtegemea sasa.
“Pia Deo Kanda naye ana majeraha, kama umeona hakufanya mazoezi na sisi badala yake alikuwa nje tu akifanya mazoezi mepesi, lakini yeye atapona kwa sababu hana tatizo kubwa sana,” alisema Aussems.
Muda wa wilker henriquez da silva na ibrahim Ajib
ReplyDelete