September 14, 2019


AZAM FC inajivunia uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Uwanja huo umekuwa na faida kubwa kwao kwani katika michuano ya kimataifa umewabeba sana.

Hivi karibuni, Azam FC ikicheza uwanjani hapo, iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia. Ushindi huo umewafanya watinge hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo ulikuwa ni wa marudiano baada ya ule wa awali Azam FC ikicheza nchini Ethiopia, kufungwa bao 1-0. Sasa wamesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.

Msimu uliopita, Simba ilikuwa bora zaidi ilipocheza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilicheza uwanjani hapo mechi sita. Ilishinda tano na sare moja. Haikupoteza hata moja.

Takwimu hizo ziliwafanya Simba kuamini moja kwa moja kwamba uwanjani hapo ni salama kwao, wakajinadi kwamba msimu huu watashinda mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika za nyumbani, lakini imekuwa tofauti baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji na kutupwa nje ya michuano hiyo hatua ya awali kwa bao la ugenini kutokana na mechi ya kwanza matokeo kuwa 0-0.

Kwa Azam FC ndani ya Azam Complex kwao pamekuwa machinjioni halisi kwani timu nyingi Afrika hata wale wababe ambao wamewahi kwenda kucheza hapo dhidi ya timu hiyo, zimekwama.

Azam FC iliyoanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008, imefanikiwa kucheza Kombe la Shirikisho Afrika misimu mitano na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu mmoja.

Ikiwa uwanjani hapo, Azam FC imecheza jumla ya mechi tisa. Imeshinda sita, sare tatu. Haijapoteza hata mechi moja.

Katika mechi ilizoshinda, zipo timu ambazo zimewahi kuwa wababe Afrika, lakini mbele ya Azam ndani ya Uwanja wa Azam Complex, hazikuambulia ushindi.

Championi linakuchambulia mechi hizo za Azam FC ndani ya Uwanja wa Azam Complex ambapo mechi ya kwanza ya kimataifa kwao ilikuwa mwaka 2013 iliposhiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC vs El Nasir
Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Azam FC kushiriki michuano ya kimataifa tangu ipande daraja mwaka 2008. Ilianzia nyumbani kucheza dhidi ya El Nasir ya Sudan Kusini katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni hatua ya awali.

Mechi ya nyumbani Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, ilipokwenda ugenini, Azam FC ikashinda 5-0. Ikasonga hatua ya kwanza ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 8-1.

Katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo, ikaanzia ugenini nchini Liberia kucheza dhidi ya Barrack Young Controllers II, Azam FC ikashinda kwa mabao 2-1, nyumbani matokeo yakawa 0-0. Ikasonga hatua ya pili kwa jumla ya mabao 2-1.

Ilipotinga hatua ya pili, mechi ya nyumbani ikawa dhidi ya FAR Rabat ya Morocco. Matokeo yakawa 0-0. Ugenini ikaenda kufungwa 2-1 na kutupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1. Hii ilikuwa mwaka 2013.

Azam FC vs Ferroviário da Beira
Baada ya mwaka 2013 kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, mwaka uliofuata yaani 2014, ikashiriki tena michuano hiyo. Safari hii haikufanya vizuri sana kwani iliishia hatua ya awali.

Licha ya kuishia hatua ya awali, lakini ilipocheza katika Uwanja wa Azam Complex, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ferroviário da Beira ya Msumbiji. Ugenini ikafungwa 2-0. Safari ikaishia hapo kwa kuondolewa kwa jumla ya 2-1.

Azam FC vs Al-Merrikh
Ulikuwa ni msimu wa tatu mfululizo kwa Azam FC kushiriki michuano ya kimataifa. Baada ya misimu miwili kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, msimu huu ikashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ilikuwa mwaka 2015.

Azam FC ilianzia hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan. Azam FC ikicheza Azam Complex, ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0. Ugenini ikafungwa 3-0. Ikaondolewa kwa jumla ya mabao 3-2.

Bidvest Wits vs Azam FC
Ulikuwa mwendelezo mzuri kwa Azam FC kwenye michuano ya kimataifa. Mwaka 2016, ikashiriki kwa mara ya nne. Safari hii ilikuwa tena ni katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ilianzia hatua ya kwanza, mechi ya kwanza ilikuwa ugenini dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Nyumbani ikashinda 4-3 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 7-3.

Hatua ya pili ikacheza dhidi ya Espérance de Tunis ya Tunisia. Azam FC ilianzia nyumbani ambapo ilishinda kwa mabao 2-1, ugenini ikafungwa 3-0. Ikaondolewa kwa jumla ya mabao 4-2.

Azam FC vs Mbabane Swallows
Tangu ilipoanza kushiriki michuano ya kimataifa mwaka 2013, Azam FC ikawa inashiriki michuano hiyo mfululizo na mwaka 2017 ikashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikianzia hatua ya kwanza kwa kucheza dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini.

Azam FC ilianzia nyumbani ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0, ilipokwenda Eswatini, ikafungwa mabao 3-0. Azam FC ikaaga kwa jumla ya mabao 3-1.

Fasil Kenema vs Azam FC
Azam FC mwaka 2018 haikushiriki michuano ya kimataifa. Inashiriki mwaka huu ambapo tayari imefuzu hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ilianzia ugenini kwa kufungwa na Fasil Kenema ya Ethiopia bao 1-0, nyumbani Azam FC ikashinda 3-1 na kusonga hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao 3-2.

Sasa itacheza dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe ambapo Azam FC itaanzia nyumbani pale machinjioni kwao.

Rekodi ya Azam FC inapocheza nyumbani inawabeba sana, kinachosubiriwa ni kuona Wazimbabwe hawa wakiondoka bila ya ushindi watakapokutana Jumapili ya wiki hii.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic