September 28, 2019












Na Saleh Ally
UKIANGALIA nchi zilizopiga kura katika tuzo za kuwania mchezaji bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), zile zinazoanzia na herufi E kwa maana ya lugha ya Kingereza, Egypt au Misri haipo.


Misri ndiyo anayotokea kiungo nyota Mohamed Salah ambaye ni mchezaji nyota zaidi katika Bara la Afrika katika kipindi hiki.


Salah alishika nafasi ya nne katika tuzo hizo ambazo mwisho, Muargentina Lionel Messi alifanikiwa kuibuka kinara akimpiku mpinzani wake, Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya tatu.

Messi pia alifanikiwa kumpiku Virgil van Djik, beki Mholanzi aliyeonekana ana nafasi kubwa ya kuwa mshindi wa tuzo hizo za Fifa, lakini Messi akaonyesha tofauti kabisa.


Hauwezi kusema Fifa wamempendelea Messi kwa kuwa wao hawapigi kura, badala yake wanaofanya kazi hiyo ni wadau ambao ni manahodha wa timu za taifa, makocha pamoja na waandishi wa habari.


Salah alishika nafasi ya nne baada ya kupata kura 26 wakati mshindi Messi alipata kura 46.

Gumzo kwa nini Misri hawakuwemo katika wapiga kura. Hakuna kura za nahodha wala kocha wake.


Salah anaamini hao ni watu waliokuwa wanastahili kumpigia kura ambazo zingemuongezea nafasi ya kufanya vizuri katika hatua hiyo.


Anaona kukosekana kwao, kumechangia kwa asilimia kubwa yeye kuanguka na kushika nafasi ya nne wakati msimu mmoja kabla alishika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa waandishi, nafasi ilikwenda kwa Hany Daniel ambaye alifanikiwa kupiga kura na aliwapigia Sadio Mane kama namba moja, Salah namba mbili na tatu ikaenda wa Ronaldo.


Kwa upigaji kura, unayemuweka namba moja anapata kura tano, namba mbili kura tatu na namba tatu kura moja.


Swali linaibuka, kwa nini hata mwandishi huyo hakumuweka Salah namba moja na badala yake akamuweka Mane? Utaifa uko wapi hapo?


Shirikisho la Soka la Misri (EFA), wao wanasema kila kitu kilikwenda vizuri, walisimamia utumaji wa kura za Kocha Mkuu wa muda, Shawki Ghareeb na nahodha Ahmed al-Mohamedi, baada ya hapo zilitumwa na baada ya siku tatu wakataarifiwa kwamba zilikuwa zimesajiliwa.


Hali hiyo ilimuudhi Salah ambaye aliamua kuondoa jina la Misri katika mitandao yake ya kijamii akionyesha anaicheza Liverpool tu. Huku akiweka ujumbe unaoonyesha kuwa wanaotaka kumtenganisha na mapenzi yake na watu wa Misri watashindwa.

Misri wanasema walituma, Salah hajaviona na kweli kura haikuwepo. Je, hujuma ipo wapi? Ndani ya Fifa au kwao Misri ambao huenda hawakutuma labda kuna ambao hawafurahii alipo Salah.

Pamoja na kuonekana nahodha na kocha wana matatizo lakini ukweli umethibitika wao hawana kwa kuwa EFA imesema walipiga kura ikatumwa. Je, aliyetuma ni nani na kweli aaminike kuwa kweli alituma? 


Unaweza kusema tuwaachie wao, lakini kumbuka wako Afrika ambako kwetu ni sehemu nzuri ya kujifunza.


Ukizungumzia maendeleo ya soka Afrika, lazima ujifunze kupitia walioendelea. Misri ni kati ya waliopiga hatua na Tanzania inaweza kujifunza lakini kama wanakwama namna hii, inaonyesha kiasi gani nchi za Afrika zina matatizo.

Katika uhalisia wa kawaida, Fifa haiwezi kuficha kura za nchi moja. Kuna tatizo ndani ya Misri ambayo inatukumbusha kiasi gani tunatakiwa kuungana mkono.


Salah anapaswa kuungwa mkono zaidi na Misri kuliko nchi nyingine yoyote duniani. Lazima tukubali kuwa matatizo ya Misri yamo ndani ya Tanzania.


Wako ambao watakuwa hawafurahishwi na mafanikio ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje. Watawaona wanaringa au wanaweza wasifurahishwe tu na wanachokifanya kwa kuwa wana husda au roho mbaya ‘mioyo michafu’ tu.


Mambo mengi sana hasa barani Afrika yamekwama kutokana na roho mbaya au wivu wa kijinga katika bara letu.

Tabia hizi zimetuangusha sana kwa kuwa tumekuwa tukirudishana nyuma wenyewe kwa wenyewe na mfano wa Misri, unatuamsha.


Tujifunze, matatizo kama hayo kama yapo, inafikia hata nahodha wenu, nyota wenu wa nchi mnaona hapaswi kuungwa mkono nanyi, basi kuna tatizo.



Tatizo lenyewe haliwezi kuwa dogo na lazima tubadilishe mambo na tuamini katika kuungana mkono na ujue, Mtanzania anapofanikiwa inakuwa faida kwa taifa kwa kuwa anavutia wengi kulitazama na mafanikio yake yanakuwa faida kwa taifa na taifa ni wewe pia.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic