September 28, 2019


















NA SALEH ALLY
MIJI imekuwa ikitanuka kwa kasi kubwa, hasa ile ambayo kwa sasa ni Manispaa au Majiji. Hii inatokana na watu wengi kuamua kujenga nje ya miji  hiyo.
Miaka kumi au 15 iliyopita, watu kujenga nje ya mji waliona ni kama bugudha, hasa kwa sehemu kama jiji la Dar es Salaam. Hali hii imekuwa hata katika majiji mengine ya Arusha, Mwanza na Mbeya.



Kila mmoja alitaka kukaa nje kama fasheni lakini mambo yamebadilika katika kipindi hiki. Kujenga nje ya mji, watu wanaamini sasa ni jambo linalowezekana kabisa.
Hii inawezekana imekuwa rahisi na inawezekana baada ya Serikali kusimamia kwa ukaribu sana suala la kiumiundombinu. Hakuna ubishi na tunapaswa kupongeza kuwa inajitahidi sana katika nyanja hiyo.



Inawezekana si kila sehemu lakini mikoa karibu yote barabara zimekuwa zikijengwa kwa kiasi kikubwa. Inawezekana eneo linakusanya kodi kwa kiwango gani, lakini Serikali inastahili pongezi kubwa katika hili.
Hii imekuwa chachu ya watu wengi kuamua kujenga nje kwa haraka kwa kuwa maeneo yanafikikika kwa wepesi na watu hawaoni kama wametenganishwa na maeneo yenye huduma.



Pamoja na hivyo, binafsi nimeingiwa hofu. Nimeona kama pamoja na maendeleo hayo, kuna jambo limesahaulika kutoka kwa Serikali za vijiji, kata, wilaya au mikoa.
Wakati wa utanuzi naamini, hakuna ramani bora zinazotoa nafasi kuwa na viwanja kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.


Unakuta sehemu ina makazi ya watu zaidi ya 10,000 lakini hakuna hata uwanja mmoja wa mpira. Hii ni hatari sana kwa mambo mengi sana.



Ninajua wataalamu wa masuala ya viwanja kutoka serikalini wanaelewa umuhimu wa kuwa na viwanja kwa ajili ya michezo katika maeneo ya makazi ya watu.


Kuna suala la burudani, kuna suala la afya lakini kumbuka michezo inawaunganisha wananchi. Mfano majirani watakaokwenda kuangalia na watakaoshiriki kucheza.


Hata kama si michezo ya mashindano, makazi yanapaswa kuwa na eneo kwa ajili ya kufanyia mazoezi kwa ajili ya afya zao. Kuna rundo la magonjwa kama yale ya moyo, kiharusi na kadhalika na wengi wanakumbana nayo na moja ya vyanzo vya magonjwa hayo ni kutokuwa na mazoezi.

Sasa kama unaona maeneo yanajengwa makazi tu na barabara pekee bila ya kuwa na sehemu maalum kwa ajili ya michezo kwa maana ya viwanja maalum au sehemu za wazi ‘open spaces’ kwa ajili ya kupumzikia na kadhalika, basi kuna tatizo.


Inawezekana tumekosea sana katika suala hili, maana ukiangalia maeneo mengi kwa asilimia kubwa, hakuna sehemu za wazi ambazo ni muhimu sana.
Tumejifunza kwa kuona madhara  yake, huenda kumekuwa na ahadi ya kufanya jambo itakapofikia wakati wa kutanua miji. Lakini tayari imeanza kutanuka bila ya kuwa na sehemu hizo muhimu sana.


Wataalamu msingoje wakati mwingine na kukubali kufanya makosa yaliyojitokeza wakati ule na leo tumekuwa tukijilaumu.


Wakati ndiyo huu, huo ndiyo wakati sahihi wa kulifanyia kazi suala hilo. Lazima kuwe na sehemu maalum kwa ajili ya viwanja vya mazoezi au michezo mbalimbali ili kuwapa nafasi au kuwashawishi wananchi au wakazi wa maeneo hayo kushiriki michezo kwa afya zao au kuwa sehemu ya kipato au hata kutoa nafasi kwa vipaji vinavyochipukia kuwa na sehemu ya kujiendeleza.

 Tusitengeneze kizazi cha wavivu, wasiopenda mazoezi, wakaishia kupenda vilevi kwa kuwa muda wa jioni wanakuwa hawana pa kwenda kwa kuwa maeneo yao hayana viwanja vya michezo.












0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic