Kiungo mkabaji wa Yanga, Abdulazizi Makame amefunguka kuwa kosa lao pekee walilonalo kwa sasa ni kwenye eneo la ushambuliaji na kama kocha wao Mwinyi Zahera akirekebisha eneo hilo wana uwezo mkubwa wa kuwachapa Zesco United kwao.
Makame kwa mara ya kwanza alianza kuichezea Yanga kwenye mechi za kimashindano juzi Jumamosi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Zesco United ambapo walitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Juma Balinya na Patrick Sibomana imekuwa haina makali sana kuanzia msimu huu umeanza.
Yanga watarudiana na Zesco United Septemba 28, nchini Zambia kwenye mechi ya kumtafuta mshindi ambaye atasonga kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Makame amesema kuwa ili wasonge mbele kwenda hatua ya makundi, basi kocha wao Zahera arekebishe kwenye eneo la ushambuliaji ambapo kulikuwa na matatizo kwa kukosa mabao mengi ya wazi.
“Tumecheza vizuri kabisa kwa muda wote wa mchezo ila tatizo letu lilikuwa eneo la ushambuliaji. Tulipata nafasi nyingi lakini tulishindwa kufunga na wenzetu wakatumia kosa letu moja wakafunga.
“Ninaamini kama kocha atarekebisha katika suala hilo kwenye ushambuliaji basi ninaamini wazi kwamba tutasonga mbele kwenda hatua inayokuja,” alisema Makame.
Zesco 2 Yanga 0 mechi ya marudiano Ndola September 28, 2019
ReplyDelete