Na Saleh Ally
TAKWIMU zinaonyesha katika rekodi ya mechi sita za mwisho kukutana katika Ligi Kuu England, Liverpool haijawahi kushinda ugenini dhidi ya Sheffield United FC.
Katika mechi hizo sita, Liverpool imeshinda mbili kama ilivyo kwa Sheffield na kuna sare mbili pia.
Katika ushindi, Sheffield United wameshinda mechi moja nyumbani na moja ugenini wakati Liverpool, wameshinda mechi zao zote wakiwa nyumbani Anfield.
Katika mechi hizo za ushindi, Liverpool walishinda 4-0 na 2-1, wakati Sheffield walishinda 1-0 wakiwa nyumbani na 2-1 wakiwa ugenini Anfield. Leo wako ugenini katika Uwanja wa Bramal Lane, mali ya Sheffield United ambayo itaongozwa na nahodha wa zamani wa Everton, Phil Jalglieka.
Angalia pia Wolves dhidi ya Watford, itakuwa bonge la mechi kama ilivyo Crystal Palace wanaowakaribisha wabishi wapya wa msimu huu, Norwich wakiwa wanaongozwa na mtaalamu wa nyavu Teemu Pukki.
Mechi nyingine ni Everton waliojipanga vema wakiwa wamepania kucheza angalau Europa League msimu huu, wakiwa wanawakaribisha mabingwa watetezi Manchester City ambao baada ya kuonja kipigo walirejea na hasira za mbogo na kumrarua mtu kwa mabao 8-0.
Kesho kutakuwa na ile shughuli ya Manchester United dhidi ya Arsenal. Wanakutana kukiwa na joto la saizi ya kati lakini timu zina historia na rekodi zilizopitia, hivyo haitakuwa mechi laini kwa wageni nyumbani Old Trafford au wageni kutoka Emirates.
Kwa kifupi, mechi za leo na kesho za Premier League zitakuwa tamu sana kutokana na mzunguko wa hali ilivyo na namna ambavyo presha imeanza kupanda kwa kasi kadiri mechi zinavyozidi kuchezwa. Kumbuka sasa ni mzunguko wa saba, kila timu itakuwa ndiyo inacheza mechi yake ya saba, zikiwa zimesalia nyingine 31, ligi ndiyo mbicho kabisa.
Wakati hesabu iko katika mechi hizo, suala liko katika kuongoza ligi na ubora wa takwimu ambao kwanza umeshachagua mapema na unaonyesha kama mambo yatakwenda hivi, ifikapo mwakani wakati EPL inakwenda ukingoni, watakaokuwa wanashindana watakuwa ni walewale, yaani Manchester City.
Angalia hivi; baada ya mechi sita kwa kila timu, Liverpool wako kileleni wakiwa na pointi 18, wastani wa asilimia 100 baada ya kushinda mechi zote na wanaowafuatia ni Manchester City ambao wamepoteza mechi mbili, hivyo wana pointi 13.
Pointi sita ingawa ni mapema lakini si jambo dogo hata kidogo na lazima kupambana vilivyo kuweka mambo sawa mapema kwa upande wa Man City.
Ingawa ni mapema unaweza kusema kama vile Manchester City wamepotea mapema vile, lakini bado.
Wao wanaonekana wana nafasi ya kusimama baadaye na kufanya vema kwa kuwa licha ya Liverpool kutawala kwa pointi, Manchester City wanatawala kwa takwimu za ubora.
Ubora ndiyo unaoonyesha timu yenye nafasi ya kwenda ikipambana kwa usahihi kwa muda mrefu, jambo ambalo linaweza kuwa uhakika wa kufanya vizuri kwa muda mrefu.
Ukiangalia katika timu zinazoongoza kwa clean sheet katika ligi hiyo, yaani kucheza bila kufungwa bao, Manchester City ndiyo wanaongoza inaonyesha wacheza mechi tatu bila ya kuruhusu bao kama ilivyo kwa West Ham. Liverpool ina mechi moja tu yenye clean sheet.
Katika takwimu za wingi wa mabao, licha ya kuwa katika nafasi ya pili. Manchester City ndiyo wenye mabao mengi zaidi ya kufunga zaidi ya timu nyingine ya ligi hiyo.
Katika mechi sita walizocheza, Manchester City wamefunga mabao 24, wakifuatiwa na Liverpool yenye mabao 17 katika nafasi ya pili, Chelsea wakiwa na 12 nafasi ya tatu kama ilivyo kwa Tottenham na Arsenal wanakamilisha tano bora wakiwa na mabao 11.
Kawaida, timu inapofunga mabao mengi inakuwa na nafasi nzuri ya kujikusanyia pointi nyingi kwa kuwa inakuwa na fowadi yenye usumbufu kwa mabeki wa timu pinzani.
Takwimu nyingine muhimu ni asisti, pasi za mwisho zinazotengeneza uzalishaji wa mabao, Manchester wabaya pia hapa na unaona mchezaji wao Kevin De Bruyne amerejea kwa kasi ya kimondo akiwa na asisti saba katika mechi sita tu.
Wanaomfuatia ni Emiliano wa Norwich aliyepiga nne na David Silva wa Manchester City pia naye ana nne. Mnapokuwa na wapiga pasi wazuri wa mwisho, kunakuwa na nafasi nzuri ya kufunga mabao mengi ambayo yanazalisha pointi muhimu.
Baada ya hapo, takwimu nyingine muhimu ni ufungaji mabao. Kinara ni Sergio Aguero mwenye mabao saba, akifuatiwa na Tammy Abraham wa Chelsea mwenye mabao saba sawa na Pierre-Emerick Aubameyangu, Teemu Pukki na Raheem Sterling wa Manchester City tena, yeye ana mabao matano.
Liverpool wana mwendo mzuri, lakini inaonekana kuna kazi ngumu sana kuwazuia Manchester City kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England hasa kama mwendo wao utakuwa huu walionao sasa.
Kama Liverpool watakwenda vizuri nao wakaendelea hivi, hakuna ubishi, washindano wa mwisho kuwania ubingwa watabaki kuwa wao wawili.
MSIMAMO PREMIER
P W D L GF GA Pts Form
1.Liverpool 6 6 0 0 17 5 18 WWWWWW
2.Man City 6 4 1 1 24 6 13 WDWWLW
3.Leicester 6 3 2 1 8 5 11 DDWWLW
4.Arsenal 6 3 2 1 11 10 11 WWLDDW
5.West Ham 6 3 2 1 8 7 11 LDWWDW
TIMU ZILIZOPITA PASI NYINGI
1. Man City 3,881
2. Liverpool 3,390
3. Tottenham 3,375
4. Chelsea 3,286
5. Brighton 3,065
MABAO YA VICHWA
1. Liverpool 4
2. Everton 3
3. Man City 3
4. Bournemouth 2
MABAO YA PENALTI
1. Man City 2
2. Man United 2
3. Arsenal 1
4. Bournemouth 1
5. Liverpool 1
MABAO NDANI YA 18
1. Man City 21
2. Liverpool 14
3. Arsenal 9
4. Chelsea 9
5. Norwich City 9
MABAO NJE YA 18
1. Liverpool 4
2. Bournemouth 3
3. Chelsea 3
4. Man City 3
5. Tottenham 3














0 COMMENTS:
Post a Comment