MHARIRI DILUNGA AFARIKI DUNIA
Aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Septemba 17, 2019, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wake tasafirishwa kwenda Morogoro kesho Septemba 18, 2019, na msiba uko Kimara Stop-Over jijini Dar es Salaam kwa dada yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile, amesema Dilunga aliyezaliwa Oktoba 28, 1976 mkoani Morogoro alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo na kabla ya kupelekwa Muhimbili alikuwa akitibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.
“Msiba umetokea leo saa 10 alfajiri kwa maradhi ya tumbo hasa ‘typhoid’ ambayo ilikuwa sugu na alihamishiwa Muhimbili Septemba 9, 2019, hadi jana jioni tulikaa naye kabla ya kuhamishiwa ICU (chumba cha uangalizi maalumu).
“Tulitoka jana usiku Muhimbili na alipewa huduma zote zilizotarajiwa, lakini kwa bahati mbaya leo asubuhi amefariki dunia. Hili ni pigo kwetu,” amesema Balile ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Ameongeza kwamba wakati Dilunga akijiunga na Jamhuri, Februari 1, 2019, alitokea gazeti la Raia Mwema na wao walianzisha mafunzo maalumu kwa ajili ya kumweka kwenye mkondo wa habari za uchunguzi.
“Kwa kweli alikuwa ameiva kwa kiwango ambacho ungeweza kumuachia gazeti na ukaendelea na shughuli zako bila wasiwasi. Lakini wakati amekomaa na kuweza kusimamia habari za uchunguzi ametutoka, ni pengo kubwa ametuachia kwenye kampuni,” amesema.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment