September 17, 2019



FURAHA kwa watanzania kiujumla baada ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufanya maajabu kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya wapinzani wao Burundi ambao hakika wameonyesha kile walichonacho kwa kupambana kwa ajili ya Taifa.

Haikuwa kazi rahisi hasa baada ya kuona kwamba mchezo wa kwanza wao walilazimisha sare ugenini licha ya kufungwa mapema na kasi ya wachezaji wa Burundi ilivyokuwa.

Safari ya kuelekea kuwania tiketi ya Kufuzu Kombe la Dunia ambalo linatarajiwa kufanyika nchini Qatar mwaka 2022 imeanza kupata aina fulani ya mwanga ambao bado umejificha gizani kutokana na safari kuendelea kupamba moto.

Kwa hatua ambayo timu imefikia kwa sasa hakuna haja ya kubweteka na kujisahau ni muda wa kujiaanda kwa ajili ya hatua inayofuata ambayo ni ngumu zaidi ya tuliyotoka.

Ushindi wa penalti ni mzuri kwani bahati ilikuwa kwa wachezaji wa timu ya Taifa pamoja na nguvu ya mashabiki ambao walijitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kushuhudia mchezo wa pili kati ya Taifa Stars na Burundi.

Kila timu ilipambana kwa hali na mali na uzembe wa wachezaji wetu ndio ulitugharimu kushidwa kupata matokeo pamoja na uzembe wa washambuliaji kushindwa kutumia nafasi ambazo walizipata bila kubisha ni lazima waambiwe ukweli kwamba walikuwa wanachezea furaha ya mashabiki na Taifa kwa ujumla.

Uhalisia utabaki kwamba mchezo ulikuwa kwetu na mashabiki walijitokeza wa wingi mwisho wa siku wachezaji walicheza kwa presha na kusahau kwamba ushindi ulikuwa unahitajika mapema kisha kazi nyingine kubwa ilikuwa ni kuulinda ushindi.

Mashabiki wanawaamini na wanapenda inaumiza pale mnaposhindwa kutimiza majukumu yenu mnapaswa mbadilike mara moja msiwe na dharau mnapokutana na timu ngumu hasa wakati mgumu wa kutafuta matokeo.

Ukweli ni kwamba mpira ni mchezo wa makosa na yule ambaye atayatumia makosa ya mpinzani ana nafasi ya kuibuka na ushindi hivyo ni jambo la msingi kulizingatia kwa wachezaji wawapo uwanjani kwa kujitoa kupambana kufa na kupona kutafuta matokeo.

Kuvuka hatua ya kwanza haina maana kwamba kazi imemalizika hapana safari bado inaendela na maisha ya soka bado yapo kikubwa ni kuona namna gani tutapenya hatua zinazofuata kutokana na ugumu wa timu ambazo tutakutana nazo.

Kiukweli kwa timu ambayo tumekutana nayo hatua ya awali endapo ingetokea bahati mbaya timu ikashindwa kupenya hapo tulikuwa tunapaswa kulaumiwa kwani timu ambayo tumecheza nayo rekodi za nyuma zinaonyesha kwamba tulikuwa tunawaburuza kwenye soka.

Kufungwa kwetu kungetoa picha kwamba hatupo tayari kwa mashindano makubwa bali tulitakiwa kuanza kujipanga upya kwa ajili ya wakati mwingine kushindana mashindano makubwa kitaifa na kimataifa.

Kabla ya mchezo rekodi zilikuwa zinaonyesha kwamba timu ya Taifa ya Tanzania ilikutana na Burundi mara 19 na ilishinda mara 11 sare 3 na kupoteza jumla ya michezo mitano hivyo ingekuwa ni ajabu kubwa kwetu kuendelea kuishusha rekodi hiyo ilihali tulishawafunga nje ya uwanja.

Kwa sasa ni wakati wa benchi la ufundi kulitazama kwa ukaribu mkubwa tatizo la ubutu wa wachezaji hasa kwenye nafasi ya ushambuliaji na kubaki na kikosi kimoja ambacho kitakuwa ni bora kuliko kukimbilia kubadili kikosi na kuwa na kikosi kipya wakati mwingine.

Hawa wachezaji ambao wametuvusha hatua ya makundi ni wakati wao kujengwa kisaikolojia na kupata nafasi ya kuzoeana zaidi huku wakitafutwa wengine wachache kuboresha makosa yaliyopo ndani ya kikosi cha Taifa.

Kwa Upande wa mabeki hapo sina tatizo napo sana ila nao wanapaswa waambiwe kwamba wawe na umakini katika maamuzi na namna ya kukamilisha majukumu kwa wakati imekuwa ni tatizo hasa pale wanaposhambuliwa kushindwa kuwasiliana kwa haraka.

Kila mchezaji ambaye analinda ni jukumu lake kufanya juhudi isiyo ya kawaida kulinda lango bila kujali ni wakati gani ama matokeo yao ni ya aina gani itasaidia kupunguza na kushusha presha ya wapinzani bila kusahahu mashabiki ambao wao wana presha ya kushinda muda wote.

Kuzungumza kwa mlinda mlango kutaimarisha zaidi safu ya ulinzi kwani yeye ndiye anaona ni namna gani anaweza kuzungumza na mabeki wake pamoja na kuwapanga pale anapoona mambo yanazidi kuwa magumu kwakwe.

Ni jambo la kuzingatia kwamba wachezaji kwenye mechi za hatua za makundi wasiwe na kujiamini kupita kiasi kutawamaliza na kuwaweka kwenye wakati mgumu kutafuta matokeo na kushindwa kuyalinda yale ambayo watayapata ni muda wa kusahau yale yaliyopita na kufanyia kazi upya hatua inayofuata.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic