Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 katika mchezo
wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United uliofanyika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface
Mkwasa, amelitaka benchi la ufundi kufanyia kazi mapungufu yaliyo kwenye safu
ya ushambuliaji kabla ya mchezo wa marudiano.
Yanga itakuwa na kibarua kizito dhidi ya miamba hao wa
Zambia kwenye dimba la Levy Mwanawasa,
Septemba 27, ambao kwa mujibu wa Kocha wao mkuu, George Lwandamina, alisema
hawajawahi kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Mkwasa ameeleza
Yanga imekuwa na tatizo kubwa la umaliziaji sababu ya kukosekana kwa muunganiko
mzuri kama ilivyoonekana kwenye mechi ya Jumamosi iliyopita.
Amesema ili kutatua tatizo hilo inabidi Kocha Mwinyi
Zahera alifanyie kazi kwa uharaka ndani ya kipindi hiki ambacho wana muda wa
kujiandaa kabla ya siku ambayo mechi itachezwa.
"Unajua Yanga mpaka sasa wana tatizo katika safu ya
ushambuliaji, nadhani labda inachangiwa na ugeni wa wachezaji ambao naamini
bado hawajazoeana.
"Katika mechi dhidi ya Zesco kulikuna na changamoto
nyingi ya wachezaji kukosa mawasiliano mazuri, inabidi Mwalimu aliangalie vema
kwa jicho la tatu ili kulirekebisha mapema.
"Naimani wanaweza kufanya vema endapo watajipanga
vizuri maana Zesco ni wazuri zaidi haswa wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani,
lakini kama wakichukulia poa itawagharimu na mwisho wa siku watafanya
vibaya," alisema Mkwasa ambaye alijuzulu ukatibu mkuu kutokana na hali
yake kiafya kuwa si rafiki.
Mbali na ushauri kwa benchi la ufundi, Mkwasa
amemzunguzia mshambuliaji mpya wa Yanga, Mkongomani, David Molinga 'Falcao'
kuwa ukubwa wa umbo lake si sababu ya yeye kufanya vibaya badala yake
utasaidia.
"Ukubwa wa umbo la Molinga si sababu ya yeye kufanya
vibaya, tunaona hata wachezaji wengi ulaya wana maumbo makubwa ambayo
yanasaidia katika kuilinda mipira isipotee, pia stamina ya mwili.
"Mchezaji anaweza kuwa na mwili mkubwa lakini
akakosa spidi na badala yake akawa anaweza kumiliki mpira vizuri pamoja na
kumuongezea morali ya kukabiliana na wapinzani wake."
http://www.tigosports.co.tz/news/full/story/1684/Samatta%20aweka%20rekodi%20UEFA
ReplyDelete