Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameguswa na kifo cha aliyekuwa mchezaji wa Azam FC, Simba na Mtibwa Sugar, Ibrahim Rajab Juma 'Jeba' aliyefariki juzi kutokana na kuugua kwa muda mrefu katika hospitali ya Mnazi mmoja iliyopo Zanzibar.
Rage amemuelezea Jeba kama mchezaji aliyekuwa mpole, mkarimu na mwenye nidhamu ya juu wakati anaichezea Simba baada ya kujiunga mwezi Juni mwaka 2012.
Rage ambaye pia hivi sasa ni mbunge msfaafu wa Jimbo la Tabora mjini, ameeleza mbali na kuwa mpole, Jeba alikuwa ni moja ya vijana wenye vipaji vya kucheza soka na akisema imekuwa ni pigo kubwa kumpoteza akiwa na ndoto za kuendelea na soka.
"Tumempoteza kijana ambaye alikuwa mkarimu, mpole na mwenye nidhamu ya hali ya juu.
"Naweza kusema Jeba alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliokuwa na vipaji zaidi akiwa uwanjani, Mungu tu ameamua kumchukua mapema lakini limekuwa pigo kubwa katika tasnia ya mpira wa miguu," alisema Rage.
Kwa upande mwingine, Rage ametoa ushauri kwa mamlaka za soka hapa nchini hususan Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya namna ya kuwawezesha wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu na Daraja la Kwanza kuwa na bima za maisha.
Amefunguka kwa kueleza wachezaji wanapaswa kufanyiwa mpango huo wa bima ili pindi inapotokoea wameondoka duniani, kipatikane kitu cha kuweza kusadia familia zao pamoja na watu wao wa karibu kuliko kuwaacha kwenye hali ngumu.
"Natoa wito ama ushauri kwa viongozi wa soka letu hususan TFF kuwafanyia namna wachezaji haswa wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza kuwafanyia wachezaji mpango wa kuwa na bima ya maisha, hii itawasaidia baada ya kifo kinapotokea.
"Kumekuwa na changamoto pindi wachezaji hawa wanapoondoka duniani huku wakiwa na familia ama wana wazazi ambao walikuwa wakiwategemea kuanza kuhangaika, lakini kama wakiwa na bima zao, itasadia kutatua matatizo madogomadogo," alisema Rage.
Mpaka umauti unamkuta juzi, Jeba alikuwa ni mchezaji wa timu ya Chuoni FC ya kwao Zanzibar.
0 COMMENTS:
Post a Comment