September 20, 2019


STRAIKA mpya wa Simba, Mbrazili Wilker Henrique tayari ameshaanza mazoezi magumu ambapo kwa siku mbili pekee ambazo amefanya ameteka mazoezi ya timu hiyo kutokana na vitu ambavyo ameonyesha likiwemo suala zima la kufunga mabao.

Wilker ambaye alifunga bao moja wakati Simba ikiwa Afrika Kusini ilipoweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, hajaichezea tena timu hiyo kwenye mechi yoyote ya ligi kuu kutokana na kuwa nje akisumbuliwa na majeraha ya mguu.

Straika huyo kwa muda wote huo alikuwa akifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kurikava kabla ya juzi Jumatatu kuanza kujichanganya na wenzake kwenye mazoezi ya kuchezea mpira.

Mshambuliaji huyo mwenye mwili uliojengeka juzi Jumanne aliteka mazoezi ya timu hiyo kutokana na vitu ambavyo alivifanya kwenye mazoezi hayo yaliyofanyika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar.

Katika mazoezi hayo ambayo yalianza saa 3:40 asubuhi, kwa wachezaji kunyoosha viungo na baadaye kuhamia kupiga pasi za pembeni na mastraika kufunga, Wilker alionyesha umakini katika kuunga mipira hiyo kwa kufunga na mingine kutoa pasi kwa wenzake.

Katika zoezi hilo lililodumu kwa dakika 50, Wilker aliweka kambani mabao matano huku akitoa asisti nne kwa wenzake.

Mbrazili huyo hakuishia hapo kwani alionyesha uwezo wakati walipocheza mechi ya wachezaji nane nane ambapo aliwatikisa mabeki wa timu pinzani aliyoichezea Pascal Wawa na Yusuph Mlipili ambao walikuwa na kazi ya kumdhibiti kutokana na kile ambacho alikuwa akikifanya.

Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems alifunguka juu ya uwezo wa Wilker kwa kusema: “Huu ndiyo mwanzo wake baada ya kurejea akitoka kuuguza majeraha.

“Ninachokifanya sasa kwake ni kumpa mazoezi ya fiziki ili awe sawa na wenzake ikiwa ni baada ya yeye kuwa nje kwa kipindi kirefu. Ninataka hadi mechi na Kagera Sugar awe tayari na acheze kwenye mechi hiyo.

“Unajua kwa sasa nina straika mmoja pekee Kagere (Meddie) hivyo ni lazima naye awe sawa kwa kumpa programu ambayo itamfanya acheze mcheo wetu ujao.

“Nimepanga kumpa programu maalum ya siku nane (sawa na saa 192) za kumfanya sasa awe tayari kwa kupambana na naamini baada ya muda huo kila kitu kitakuwa sawa kwake,” alisema Aussems.

Wachezaji ambao walihudhuria kwenye mazoezi ya jana ya Simba ni Sharaf Shiboub, Francis Kahata, Shomary Kapombe, Wilker Henrique, Kennedy Juma, Ibrahim Ajibu na Said Ndemla. Wengine ni Pascal Wawa, Yusuph Mlipili, Tairone Santos, Fraga Vieira, Clatous Chama, Rashid Juma, Aishi Manula na Beno Kakolanya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic