WALIMU 10 MBARONI KWA WIZI
Polisi mkoani Kagera linawashikilia walimu kumi kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa mtihani wa darasa la saba wilayani Ngara mkoani humo.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 12 majira ya saa 4:40 katika shule ya msingi ya Kumnazi iliyopo tarafa ya Nyamiaga wilayani Ngara.
Kamanda Malimi alisema kamati ya mitihani ya wilaya hiyo ilipata taarifa kuwa baadhi ya walimu watano waliokuwa wamejifungia ndani ya nyumba ya mmojawapo wa walimu hao walikuwa na mtihani wa sayansi wakiandaa majibu kwa ajili ya kuwapa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakiendelea na mitihani ya taifa.
Aliwataja walimu hao kuwa ni Manase Mtinange (50) mkuu wa shule hiyo, Prosper Pius (29), Joachim Kakuru (31), Christiana Ilete (27) na Eric Balbati (30).
Alisema kuna wasimamizi watano walioteuliwa kusimamia mitihani katika shule hiyo ambao wanaoshikiliwa pia kwa mahojiano majina yao yakiwa ni: Revocatus Juhudio (37) Shule ya Msingi Kashalazi, Jerusa Mganga (46) Shule ya Msingi Nyakahanga-Rusumo, Rusalo Izaac maarufu Petro (31) Shule ya Msingi Kashalazi, Jofrey Mshahiri (31) shule ya msingi Mayenzi na Hezron Eugo (43) msimamizi mkuu wa kituo kizima.
Aidha idadi na majina ya watoto waliokuwa wanaandaliwa majibu ya mtihani na walimu hao imehifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya kulinda haki za mtoto.
Vilevile, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa awali ambao umebaini kuwa mtihani huo ulipatikana katika mazingira ya shuleni hapo na kuongezea kuwa kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.
Aliongezea kwamba mtihani ni siri kuu ya nchi na wahusika hula viapo vya uadilifu, hivyo ikithibitika wamehusika na udanganyifu wa aina yoyote watafikishwa mahakamani.
0 COMMENTS:
Post a Comment