SAMATTA AMTUMIA UJUMBE VAN DIJK LIVERPOOL
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amemchimba mkwara beki wa Liverpool, Virgil Van Dijk na beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly watakapokutana naye kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiyo wataelewa Tanzania inapatikana wapi.
Samatta anayekipiga katika Klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji ametoa kauli hiyo ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza hatua ya makundi ya michuano ambapo Genk imepangwa Kundi E ikiwa na klabu za Liverpool ya England, Napoli ya Italia na Red Bull kutoka Austria.
Samatta kwa sasa amepewa mapumziko mafupi na madaktari wa timu yake baada ya kuumia katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Burundi.
Baba mzazi wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Mbagala Market, mzee Ally Samatta alisema kuwa mtoto wake amemuhakikishia kuiwahi michuano hiyo huku akiwa amejipanga kuwavuruga mabeki hao wenye viwango vikubwa duniani.
“Nimezungumza naye, ameniambia anaendelea vizuri kwa sababu yupo chini ya jopo la daktari wa timu ambao wanamuangalia kwa karibu katika kipindi cha mapumziko, na wanafanya hivyo ili aweze kuiwahi Uefa.
“Nimeongea naye, alichonieleza kuona anakwenda kucheza na mabeki wa kubwa duniani ambao ni yule Koulibaly kutoka Napoli na Van Dijk ambaye ni beki bora wa Ulaya, yeye amesema atatumia nafasi hiyo kuwaonyesha kwamba kuna nchi inaitwa Tanzania na vipaji vipo kwa sababu wamekuwa wakiidharau nchi yetu,” alisema mzee Samatta ambaye anauelewa mkubwa wa ishu za soka.
0 COMMENTS:
Post a Comment