TAIFA
limeshuhudia upande wa kimataifa wawakilishi wa Tanzania wote wakianza kwa
kuchechemea kwani kila mmoja amejiongezea mzigo tofauti na matarajio ya
mashabiki pamoja na ahadi za wachezaji na benchi la ufundi.
Yanga wapo
kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, walilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi
ya Zesco United uwanja wa Taifa kisha Azam FC nao wakakubali kupoteza mara ya
kwanza uwanja wa Chamazi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Triangel United.
Mashabiki na
baadhi ya viongozi wanaonekana kukata tamaa na timu zao kwa sasa kwenye michuano hii mikubwa inayoandaliwa na Caf ila bado kuna
nafasi ya kufanya kuelekea kwenye marudio ya michezo hii ya kimataifa kwa
wawakilishi wa Tanzania ambayo inachezwa leo Septemba 28, ni dakika 90 za moto kwa timu zote ila endapo watafanya haya kuna nafasi ya kupenya:-
Kukubali matokeo ya nyumbani
Kwa sasa
Azam FC na Yanga hawana namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuyakubali matokeo
waliyoyapata kwani kuyakataa kutawaongezea ugumu wa kutafuta ushindi kwenye michezo
yao ya marudio ni suala la kuamini kwamba walifanya makosa na kupata kile
ambacho hawakutarajia.
Itakuwa
rahisi kwao kuwapa ugumu wa kupambana na kupata hasira za kutafuta matokeo
kwenye mchezo unaofuata endapo watakuwa na imani kwamba hawakustahili kupata
matokeo ya mwanzo.
Kuandaa mbinu mbadala
Hapa
mabenchi yote ya ufundi yana kazi ya kuandaa mbinu mbadala ambazo zitatumika
kuwamaliza wapinzani mapema.Kwa mfano tunaona namna ambavyo Yanga imekuwa
ikihaha kutafuta matokeo hasa kwa washambuliaji wake kushindwa kumalizia nafasi
ambazo wanazitengeneza huku kwa upande wa Azam FC namna washambuliaji
wanavyohaha kupata mipira kutoka kwa viungo.
Kwa timu
zote mbili kumekuwa na ugumu wa kutengeneza pasi za umaliziaji hasa wachezaji
wanapofika eneo la hatari, ni muhimu kwa benchi la ufundi kulitazama hili kwa
ukaribu na kulipa dawa washambuliaji wao wengi wamekuwa wakicheza mithili ya
viungo jambo ambalo linawaongezea ugumu kwenye kupachika mabao licha ya kupata
nafasi.
Kujiamini
Wachezaji
wanakazi kubwa ya kuongeza uwezo wa kujiamini ukizingatia kwamba mechi za marudio
wote watakuwa ugenini. Tumeona namna ilivyokuwa shida kwa Idd Chilunda wa Azam
FC alitokea benchi baada ya muda mwalimu akaona hajiamini akaamua kumtoa ni
pigo kwa wachezaji ambao wanatafuta ushindi kushindwa kujiamini.
Nidhamu nje na ndani ya uwanja
Imekuwa ni
kawaida wachezaji wakiwa nyumbani kuwadharau wapinzani jambo ambalo huongeza
wepesi kwa wapinzani kushinda kwa nafasi ambayo ipo mbeleni kwa wawakilishi
wetu kimataifa ni dhahiri kwamba mkiwaheshimu wapinzani wenu ugenini ni fursa
kwenu kutusua.
Tumeskia
Kocha wa Zesco United, George Lwandamina akisema kuwa ni ngumu kwake kupoteza
nyumbani, tayari kuna ukuta amejiwekea ambao ni kujiamini hapo ndipo pakuanzia
kupanda kabla ya kutusua ugenini.
Kutobweteka na matokeo yaliyopita
Azam FC na
Yanga zote mbili kwenye michezo yao ya kimataifa zilipata aina moja ya matokeo
sawa na waliyoipata kwa sasa kwenye michezo yao ya awali , Azam ilipoteza mbele
ya Fasil Kenema ugenini na Yanga ililazimisha sare mbele ya Township Rollers
nyumbani na mwisho wa siku wakapindua
meza kibabe.
Ushindi
ambao waliupata mbele ya Fasil Kenema na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2
usiwape kiburi Azam na kubweteka wakiamini miujiza wala Yanga ushindi wao wa
bao 1-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 mbele ya Township Rolers
usiwape kiburi hatua ya sasa ni ngumu kuliko ile ya awali.
Juhudi isiyo ya kawaida
Timu zote
kwa sasa zinapaswa zitambue kuwa juhudi zao ndani ya uwanja ndizo zitakazowapa
matokeo chanya. Wasijisahau pale watakapopata bao la mapema bali ni muda wa
kujipanga upya kwa kuongeza juhudi upande wa kujilinda na kushambulia.
Kutafuta majibu sahihi ya anguko lao
Kwa mfano
Yanga ambao walianza kushinda mapema walipoteza nguvu nyingi kufurahia ushindi
walioupata na kusahau kwamba mpira unaendelea na mwisho wa siku wakawapa nafasi
wapinzani. Azam wao ilikuwa ngumu kushinda baada ya kufungwa bao la mapema timu
ilipoteana na kila mchezaji akawa anacheza anavyojua.
Udhaifu wao kimataifa upo hapa
Kocha Mkuu
wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kuwa waliponzwa na uchu wa wachezaji kutafuta
magoli mengi zaidi jambo lililowapa nafasi ya kufunguka zaidi na kujisahau
kuweka ulinzi langoni.
“Tulifunga
bao la mapema kipindi cha kwanza, wachezaji wakawa wanahaha kutafuta bao lingine
la pili kujiweka kwenye nafasi nzuri na kusahau kujilinda jambo lililowapa
nafasi wapinzani wetu kutufunga,” alisema.
Etienne
Ndayiragije, Kocha Mkuu wa Azam FC alisema kuwa kushindwa kujiamini kwa
wachezaji wake kumemfanya akose matokeo kimataifa anajiandaa kwenda kupindua
meza ugenini.







0 COMMENTS:
Post a Comment