October 7, 2019


Wako wadau wa soka ambao wanakumbuka miaka ile ya Chama cha Soka Tanzania (Fat). Chama ambacho wakati wa uongozi wake kilikuwa maarufu hata kuliko klabu zenyewe.

Fat hasa ya kipindi cha Muhidini Ndolanga akiwa mwenyekiti, ilikuwa maarufu kupita kiasi na mambo mengi yalifanyika chini ya chama hicho.

Chama hicho kilikuwa na nguvu utadhani ni nchi na wakati fulani ilifikia hata kuingia katika malumbano na serikali na kuipeleka serikali katika sehemu iliyosababisha Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kuitishia kuifungia Tanzania kwa madai kuwa kuna ubabe kwa serikali kuingilia habari za mpira.

Wakati wa Ndolanga, gumzo kwa viongozi wa Fat lilikuwa kubwa sana. Wao walikuwa maarufu hata kuliko wachezaji waliokuwa wanacheza soka kulingana na mambo yao ya uongozi.

Hata vyombo vya habari badala ya mpira wa uwanjani, zaidi viliripoti kuhusiana na malumbano au fitna za viongozi, mfano Ndolanga dhidi ya Katibu Mkuu wake, Ismail Aden Rage na wakati mwingine Michael Richard Wambura.

Siku hizi mambo yamebadilika sana licha ya kwamba kumekuwa na vipindi vingi vya mpito wakati wa uongozi wa kwanza wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Leodegar Tenga, baadaye Jamal Malinzi na sasa Wallace Karia.

Kila nyakati zina hadithi yake lakini vizuri kuzungumza nyakati tulizopo, wakati wa TFF chini ya Karia ambayo tunaona kuna juhudi kubwa ya kubadili mambo mengi.

Kuna methali moja ya “Kwanza kwa saburi, kwisha kwa sururi.” Methali hii inafafanua namna tunavyopaswa kuwa na subira kwa yale tunayofanya huku tukiwa tunataka mafanikio. Kabisa, inawezekana watu wamechoka kwa kuwa wamekuwa wakitaka mafanikio kwa muda mrefu na nyakati tulizopitia zimewaangusha.

Lakini hii haizuii kwa kuangalia tulipo na nini kinafanyika. Kwa kuwa kuanzia Fat baadaye TFF kumekuwa na upungufu unaofanana, basi usitukaririshe tukaamini na kuanza “kuona” kila TFF inafanana na ile nyingine iliyopita.

Tusikariri na kuanza kuamini TFF imekosea kama ile iliyopita na vizuri kutoa “hukumu” kulingana na unachokiona.

Kama watu wanafanya vizuri, basi vizuri kuwapa kongole na kueleza wazi kutokana na kile wanachokifanya kuwa ni kitu bora. Si vizuri hukumu iwe ya huyu kupitia yule aliyepita. Mfano, wako wamekariri kuwa TFF ni lazima ilaumiwe au kushambuliwa kwa kuwa tu miaka yote na TFF zote zilizopita ilikuwa ni namna hiyo.

Unawalaumu vipi kila wakati wakati wana vingi wanafanya vizuri? Vile ambavyo wanakosea, vizuri kuwasema na kuwakumbusha lakini vizuri tuwasifie au kuwapongeza na kuwapa moyo wa kuendeleza vingine bora zaidi na zaidi. TFF chini ya Karia na Katibu Mkuu, Wifred Kidao imekuwa na mambo mengi sana ambayo imeyabadilisha na hakika yanaonekana kuwa na mwelekeo bora sana.

Tumeona timu zetu za taifa za vijana zinavyoshiriki kwa ubora wa juu. Kambi bora na kumekuwa na mwanga kwamba kuna kitu kinakuja na vijana wanapambana sana.

Timu kubwa ukianzia michuano mikubwa na ile mingine kama Chan na kadhalika, zina mwonekano wa huduma bora na mwisho linabaki jambo la kucheza uwanjani ambalo wigo wake ni mpana, kwani mbali na wachezaji, benchi la ufundi basi hata mashabiki wanahusika.

Hivyo kuna kila sababu ya kuanza kubadili mawazo, kwamba kuna kizuri kinatengenezwa basi tuvute subira huku tukishiriki na pia kuachana na dhana ya kwamba ikiwa TFF basi kila andiko lazima liwe la kuwasema vibaya au kuwashutumu. Kama yako mabadiliko na yana faida kwa taifa letu, tuungane nao kuyasukuma mbele.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic