October 7, 2019


Mashabiki wa mpira wana asili inayofanana sana hasa katika suala la kushabikia. Ndio maana huwa unaona wakati wa ushangiliaji uwanjani vitu vinakwenda kwa pamoja utafikiri watu walikuwa wamefanya mazoezi.

Kelele za ushangiliaji ni sawa, mtu anapokosa bao, sauti zinafanana na mambo yanakwenda sawa.

Hii ni sehemu ya kuonyesha mashabiki wa mpira wana mambo mengi yanayofanana hata kama wanatokea katika nchi au bara tofauti. Si vibaya, yako yanapaswa kuigwa kwa kuwa hakuna ubaya kufanya hivyo lakini yako yanapaswa kuepukwa kwa kuwa kuyaiga ni kufanya yasiyo sahihi.

Moja ya mambo ambayo naona wapenda soka wanapaswa kuyaepuka ni “kulishwa” maneno yasiyo sahihi na baadaye wakayaamini.

Baada ya kuyaamini wamekuwa wakiyasambaza utafi kiri wana uhakika nayo. Wakati mwingine inakuwa aliyesema alikosea, yaani bahati mbaya au kutojua au anajua lakini anafanya makusudi kuharibu jambo fulani kwa faida zake binafsi.

Moja ya mambo ambayo hakika si mazuri ni lile kuambiwa fulani ameisha sana, fulani hana uwezo au uwezo wake umeporomoka, halafu ukaamini tu licha ya kwamba na wewe umekuwa ukimshuhudia na anacheza vizuri tu.

Kwa kuwa kuna mtu amesema ameshuka kiwango, wewe pia unalichukulia suala hilo kwa maneno yake na kuliamini na kuanza kulisambaza. Mfano mzuri ni beki wa kati wa Simba, Serge Wawa. Binafsi namuona kuwa mmoja wa mabeki bora wa kati waliowahi kucheza katika Ligi Kuu Bara ndani ya kipindi cha misimu mitano.

Wakati anatokea Sudan ambako alionyesha cheche zake katika soka la kulipwa, alitua Azam FC na hakika alionyesha uwezo mkubwa ambao tunakumbuka sote. Amepata mafanikio Azam FC ikiwa ni pamoja na kubeba makombe kadhaa. Baadaye aliondoka na kurejea Sudan ambako baada ya muda, Simba wamemrejesha tena nchini.

Tokea amerejea nchini tumeona, baada ya msimu mmoja tu, Simba imeanza kurejesha heshima yake ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa.

Ingawa Wawa hatumkumbuki, tunasubiri hadi akosee, ubora wake umethibitika kwa kuwa safu ya ulinzi aliyoiongoza kwa msimu wa 2017/18, Simba ilifungwa mabao 15 tu katika mechi 30 na msimu uliofuatia wa 2018/19 ambao wamebeba ubingwa, katika mechi 38, Simba ilifungwa mabao 15.

Wawa ndiye kiongozi wa safu ya ulinzi na amecheza mechi nyingi zaidi. Misimu miwili mfululizo, kikosi cha Simba kimekuwa bingwa kikiwa ndio chenye safu bora ya ulinzi. Ubora wa safu yao ni kwa kuwa Simba imefungwa mabao machache zaidi. Hata mechi walizopoteza ni chache zaidi kuliko timu nyingine.

Hapo ndio unajiuliza, vipi wanaosema Wawa si bora wanawaaminisha wengine na wao wakaamini? Wakati Wawa anatua nchini akitokea Zambia, wakati wa mechi za kirafi ki alishindwa kuonyesha uwezo bora na sote tuliliona hili. Moja ya sababu tukaelezwa hakuwa amecheza kwa kipindi fulani soka la ushindani.

Kweli baada ya kuendelea kupata mechi kadhaa kwa maana ya match fi tness. Wawa alibadilika na kuwa lulu Simba. Kocha Patrick Aussems bila shaka anajua beki bora ni yupi. Kama anaendelea kumpanga Wawa, haiwezekani akawa ni beki asiye na uwezo au kuaminishwa eti amezeeka. Unakumbuka kipindi Simba walipopoteza mechi mbili za ugenini za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na AS Vita wakifungwa bao 5-0 kila mechi!

Ikaonekana tatizo ni Wawa lakini ukweli ulikuwa ni mfumo na safu nzima ya ulinzi na ukabaji wa kiungo na si mchezaji mmoja. Niliamua kuandika kuhusiana na Wawa baada ya kujikumbusha lakini pia baada ya shabiki mmoja kunihoji, kwamba vipi Wawa bado anacheza Simba na uwezo wake umeporomoka sana?

Nilipomhoji kuhusiana na sababu hizo za kuporomoka, alionekana hakuna alichokuwa anakijua zaidi ya kumtaja shabiki mwingine ambaye alisema kwa kuwa yeye anamuamini anajua sana. Kwa kiwango anachoonyesha, Wawa bado ana uwezo mkubwa na ataisaidia Simba. Beki bora, haina maana hatakosea au kupitwa.

Tumeona beki Virgil van Dijk wa Liverpool alivyokuwa gumzo baada ya kupigwa chenga na Liverpool ikafungwa dhidi ya Red Bull Salzburg katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, juzi. Gumzo limekuwa kubwa kwa kuwa beki huyo ni bora haswa na si rahisi kupitika.

Hivyo kuna siku Wawa atakosea kama beki lakini rekodi zake zinamuonyesha ni mmoja wa mabeki bora Simba imewahi kupata na mafanikio aliyonayo yako wazi kupitia mafanikio ya hatua walizofi kia kama robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili mfululizo na pia kuwa safu ya ulinzi iliyofungwa mabao machache zaidi.

Unapoambiwa kuhusiana na mchezaji fulani, inapokuwa ni ubora au udhaifu, basi takwimu ndizo zinapaswa kuamua au kuthibitisha badala ya hadithi tu za “sungura na fisi”.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic