Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kwa kushirikiana na mamlaka nyingine lilifanikisha prodyuza mkali Bongo, Paul Mathyasse ‘P Funk Majani’ kupata kitita cha zaidi ya shilingi milioni mia moja ikiwa ni fidia kutoka kwa msanii wa Uganda, Jose Chameleone.
Ilikuwa ni baada ya Jose kutumia mdundo wa wimbo maarufu wa Nikusaidiaje uliotungwa na kuimbwa na Profesa Jay bila idhini ya wahusika.
Kwa vipindi tofauti, Basata imefanikiwa kuzifungia nyimbo na wakati mwingine kuonya wasanii wanaoimba nyimbo zilizo kinyume na maadili au zenye kuleta tafsiri isiyo sahihi kwa wasikilizaji na watazamaji.
Hayo ni baadhi ya mafanikio yanayaoonekana na wengi ya Basata. Ila kwa tathmini yangu, zaidi ya asilimia 60 ya wasanii nchini wanahisi Basata siyo baraza lao.
Wasanii wengi wanaona Basata ni kama taasisi fulani isiyo na tija ya moja kwa moja kwa ustawi wao na ustawi wa sanaa kwa ujumla.
Nitaeleza kwa uchache baadhi ya sababu zao. Wengi wanasema, Basata mara nyingi hujitokeza katika kutoa adhabu kwa wasanii ila ni mara chache mno hujitokeza wakati wa kuwasaidia na kuwatetea wasanii.
Likiwa kama baraza lenye mamlaka ya kusimamia sanaa na wasanii Bongo, watu wanahoji limefanikiwa vipi kumfanya msanii nchini ajivunie kuwa msanii na siyo mtumwa wa wamiliki wa vyombo vya habari na waendesha matamasha?
Mara ngapi tumesikia kuwa baadhi ya waandaaji matamasha wakiwanyonya wasanii na wakati mwingine kuendesha kampeni za kuwapoteza kisanaa kwa sababu wameenda kinyume na matakwa yao? Basata kama chombo halali chenye mamlaka kisheria ya kusimamia sanaa na wasanii nchini, limewahi kufanya utafiti kupata usahihi wa habari hizo na kutafuta mbinu muafaka za kuwasaidia wasanii?
Kuna muziki unaitwa Singeli. Ukiusikiliza kwa makini unagundua ni aina fulani ya kipekee ya kimuziki duniani. Singeli siyo ya Wakongo. Siyo ya Wanigeria. Siyo ya Wamerekani wala Wahindi. Ukiusikiliza vizuri muziki huu utagundua una kila sababu ya kujivunia muziki wa Kitanzania kwa sifa na vigezo vyote. Ila tatizo liko kwa wasanii wa Singeli.
Wengi wao siyo wabunifu na hawana mbinu muafaka za kuufanya muziki wao uwe na nguvu na heshima kama ilivyowahi kuwa muziki wa dansi au Bongo Fleva kwa sasa. Basata limewahi kuutafakari muziki huu kwa kina na kujua wanatakiwa kufanya nini ili kuusaidia kukua?
Basata limewahi kuwatumia watalaam kufanya utafiti wa namna bora ya kuendeleza muziki wa Singeli kisha kuwapa semina wasanii ili waione fursa iliyo mbele yao? Au wao wako kimya tu maofisini wakipigwa viyoyozi wakisubiri akina Dulah Makabila, Sholo Mwamba na Man Fongo waimbe haina ushemeji wawafungie?
Mimi ninafahamu mazingira ya wasanii wetu. Kabla ya kutoka, wengi wao wanatoka katika maisha duni na ya kimaskini sana. Baadhi wametoka kwenye jamii za wakorofi na walioathirika na mambo ya kihuni. Ila kutokana na kujitambua wana vipaji vya kuimba, wakaona waingie kwenye muziki ili iwe sehemu ya ajira yao.
Sasa kutokana na historia za maisha yao na mazingira waliokulia wengi wao wakipata nafasi ya kwenda studio wanafikiria pesa na umaarufu tu, bila kujali usahihi wa mashairi yao na muziki wao utafika wapi.
Kwa namna hii wengi wao hujikuta wakiimba mambo yasiyopaswa kutamkwa hadharani na matokeo yake jamii inamdharau msanii husika na pengine aina yenyewe ya muziki. Kisha Basata inakuja baadaye kumfungia mwanamuziki huyu na wimbo wake.
Siyo vibaya kumfungia mtu mwenye kuimba au kuonesha picha zisizo na maadili. Ila swali langu kwa baraza letu hili, hivi linajua kiuhalisia hali za wasanii wetu? Mara ngapi huwa linatoa semina za kuwapa elimu za kizalendo na mbinu za kuendeleza sanaa yao kwa kasi na viwango stahili?
Baraza la sanaa nadhani linapaswa kuanza kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wasanii wetu wawe na ustawi mwema. Kukaa tu ofisini na baadaye kutangaza kufungia nyimbo siyo tu kazi pekee ya baraza hilo, ila pia linajiweka katika mazingira ya kuonekana mzigo badala ya mkombozi wa sanaa na wasanii.
Tangu Kanumba amefariki dunia soko la filamu limeyumba sana. Kuyumba huko kumefanya hata baadhi ya wasanii wa filamu ghafla kukimbilia katika fani nyingine.
Basata limefanya tafiti na kugundua Kanumba alikuwa anasababisha vipi sanaa ya filamu iwe na msisimko na kifo chake kimeathiri vipi sanaa! Kumsubiri Rosa Ree, Meninah au Nandy warekodiwe na wapenzi wao ndiyo waibuke haisadii sana sanaa.
Zamani watu walikuwa wanababaika sana na sanaa za maigizo na maonesho. Ila sasa hali hiyo imepotea. Je, imepotea kwa sababu ya mabadiliko ya nyakati au kuna kitu kimepungua ndiyo maana msisimko wa maigizo na filamu umekwisha. Basata imewahi kuwaita akina Christant Muhenga na kuzungumza nao kwa sababu watu hawa ndiyo walikuwa magwiji wa sanaa za maigizo kipindi hicho?
Basata limeandaa semina mara ngapi kwa kuwatumia wasanii kama Muhogo Mchungu na wengine wa kariba hiyo kuwafundisha wasanii wa kizazi kipya cha filamu ili angalau wafanye kazi huku wakiheshimu miiko na maadili ya nchi?
0 COMMENTS:
Post a Comment