Katika kuhakikisha wanafanikisha usajili wa kiungo mchezeshaji fundi Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Mhandisi Hersi Said fasta, Jumatano ya wiki hii alikwea pipa kwenda nchini Rwanda kwa ajili kumsainisha nyota huyo anayesubiriwa kwa hamu Jangwani.
Kiungo huyo ambaye alikuwa mchezaji wa Simba kwa msimu uliopita, ni kati ya wachezaji wanaotarajiwa kujiunga na timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo lililofunguliwa juzi Jumatatu ambalo litafungwa Januari 15, 2020.
Yanga tayari hadi hivi sasa imefanikisha usajili wa washambuliaji wawili ambao Tariq Seif, Ditram
Nchimbi na Adeyum Saleh huku wakiwa kwenye mazungumzo ya mwisho na viungo Luís Jose Miquissone wa Mamelodi Sundowns anayekipiga kwa mkopo UD Songo ya Msumbiji na Niyonzima mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili limezi paa ni kuwa bosi huyo juzi alisafiri kwenda Rwanda akitokea Uganda na kufikia Mariot Hotel alipokwenda kushuhudia nusu fainali ya Kombe la Chalenji lililomalizika nchini jana Alhamisi.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Niyonzima alitoa sharti la kufuatwa kusaini mkataba sambamba na kupewa fedha za usajili akiwa kwenye ardhi ya nyumbani kwao kabla ya kutua nchini kujiunga na kambi ya timu hiyo iliyoweka ikijiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Iringa FC utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Msimu wa 2017/18 Simba nao wakati wakitaka kumsaini Niyonzima kwa ajili ya kutumikia timu yao, kiungo huyo aliwataka mabosi wa timu hiyo kwenda kumalizana naye kwao huko Rwanda jambo ambalo Simba walitii na kijana akamwaga wino.
Aliongeza kuwa bosi huyo anamfuata Niyonzima baada ya kufikia muafaka mzuri kati ya uongozi na kiungo huyo aliyecheza kwa mafanikio makubwa Yanga akiipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, Kombe la FA na Kombe la Kagame.
“GSM hivi sasa wameamua kuingilia kati usajili wa dirisha hili dogo lililofunguliwa kwa kufanikisha wenyewe
usajili wa kila mchezaji aliyekuwepo kwenye mapendekezo ya kaimu kocha wetu Mkwasa (Charles).
“Tayari imefanikisha usajili wa Tariq, Nchimbi na Adeyum (Salehe) kwa kuwasajili wenyewe ikiwemo kufanya nao mazungumzo na kuwapatia fedha za usajili, hivyo baada ya kufanikisha usajili wa washambuliaji hao, nguvu zao wamezielekeza kwa Luis kiungo wa UD Songo na Niyonzima.
“Hivyo, bosi huyo wa GSM ambaye jina lake ni Hersi tayari yupo Rwanda tangu juzi Jumatano na aliondoka
kwenda huko akitokea Uganda alipokwenda kuangalia nusu fainali ya Kombe la Chalenji wakati Kilimanjaro Stars ilipocheza na Uganda na kufungwa bao 1-0,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuzungumzia hilo alisema: “Hizo taarifa za Niyonzima kusajiliwa na Yanga zipo lakini bado hazijakamilika, kama zikikamilika basi tutaziweka wazi.”
Hapa ndipo Brand inapofanyiwa kazi..watu wanataka biashara ifanye kweli na si mchezo..washabiki waende uwanjani kuangalia mpira na si butua butua. Brand inasaidia Yanga na GSM kufanya kazi pamoja. Hongera kwa kuijua biashara maana yake nini...wengi hawajui maana ya GSM inachokifanya
ReplyDelete