NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na gumzo kubwa miongoni mwa wanamichezo baada ya mchezaji mkongwe wa Yanga, Mrisho Ngassa kutupia mtandaoni kauli inayoonyesha analalamika kuhusiana na suala la fedha.
Kauli ya Ngassa inaonyesha analalamika kuhusiana na fedha zake zilizocheleweshwa. Mbele ameongeza kwamba kumekuwa na tabia ya kutowapa kipaumbele wazawa.
Ujumbe huo wa Ngassa umezua mjadala mkubwa sana kwa juzi na jana kwa kuwa ulitoka muda mfupi baada ya mechi kati ya Yanga na Iringa United kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Yanga ilishinda kwa mabao 4-0 na Ngassa alikuwa kati ya wachezaji waliochagiza ushindi huo ulioendeleza kurudisha faraja kwa Wanayanga.
Mjadala ulikuwa mpana kwa kuwa wako walijaribu kuonyesha huyo hakuwa Ngassa, wako walionyesha ni yeye na kweli alistahili kufanya hivyo na wengine wakasisitiza kwamba kama ni hivyo angemalizana na uongozi tu.
Pia walikuwepo waliokuwa wakimshambulia Ngassa kwamba hayo kayataka mwenyewe kwa kuwa huko nyuma alikataa kwenda kusajiliwa na timu kubwakubwa zilizomtaka barani Afrika au wakati mwingine timu kadhaa za Ulaya lakini akagoma kwenda huko sababu ya Yanga.
Hawa nao walikuwa na hoja, huenda kwao ilikuwa wakati mwafaka wa kumfikishia ujumbe baada ya kukerwa naye kutokana na zile tabia za kuonyesha kuipenda Yanga tu badala ya kupenda kazi yake kama mwanasoka.
Pamoja na yote hayo, ukweli ni kwamba ujumbe wa Ngassa umefika na unapaswa kufanyiwa kazi na hasa kwa viongozi wetu wa soka hapa nyumbani.
Mara kadhaa, nimezungumza kuhusiana na hili kwa namna ambavyo wachezaji wa kigeni wanavyopewa huduma bora, mwanana na zenye tofauti kubwa na wachezaji wazalendo.
Ukiangalia nyumba zao ni bora kabisa, hata kama mchezaji atakuwa anatokea Burundi, nchi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na yetu. Lakini atakuwa na huduma bora kabisa na wakati mchezaji wa hapa nyumbani hapati hata nusu yake.
Kumekuwa na tabia ya kutoa mishahara maradufu kwa wachezaji wa kigeni huku wale wa hapa nyumbani wakionekana hawana lolote au wakipata huduma ya kawaida kabisa ukifananisha na zile za wachezaji wa kigeni.
Angalia unaporejea katika suala la uchezaji, wakati mwingi unakutana wachezaji wazalendo wa Watanzania wamekuwa wana mchango mkubwa sana kuliko hata wageni wengi katika vikosi vyao.
Jambo hili limekuwa likiwaumiza sana wachezaji wazalendo na ukiwasikia wanaelezea yanayotokea, unaona yana msingi sana.
Mara nyingi wanashindwa kusema kwa hofu ya kupoteza vibarua vyao. Wanabaki wananung’unika na hii kwa kiasi kikubwa inawachangia wao kushindwa kufanya vizuri na baadaye kuanza kulaumiwa hawana msaada.
Angalia wale wanaogoma, huingia kwenye lawama za mashabiki na kuonekana kama wasaliti. Lakini mashabiki huwa hawana nafasi ya kuuliza mchezaji huyo mzawa amedai kwa muda gani, amepewa ahadi hewa mara ngapi?
Mbaya zaidi wakati yeye akidanganywa au akiwa hajatimiziwa ahadi zake pamoja na juhudi zake, uongozi unasajili mchezaji mpya kutoka nje ambaye inaelezwa kuwa atalipwa mshahara mkubwa, mchezaji huyu mzalendo unafikiri atajisikiaje?
Hawa wachezaji wetu nao ni binadamu lakini lazima tukubali, hata kama watakuwa na upungufu upi, wanaopaswa kuwa wa kwanza kuwalinda kimaslahi na kuwasukuma kiutendaji kwa faida ya klabu na timu yetu ya taifa ni sisi Watanzania na wenye nafasi hiyo ni viongozi wa klabu zetu.
Acheni kutukuza wageni kwa kiwango cha kupindukia wakati wanatokea katika nchi za DR Congo, sijui Kenya, Burundi, Rwanda, Zambia na nchi hizo nyingi tunazizidi kimaisha. Hivyo hakuna sababu ya kutenganisha huduma kwa kiasi kikubwa.
Kama kuna wachezaji wazawa wana juhudi, wanaonyesha matunda, basi huduma zao ziwe juu hata kuliko wageni. Ili kuwaamsha wazawa wengine wajue wanaweza kuwa juu ya wageni kama wakifanya vizuri zaidi.
Ndugu Salehe Ally mara nyingi huwa nasoma makala zako ni mfuasi wako mkubwa ila kwa hii ya leo, sijui umeandika ukiwa unawaza nini? Nimeshindwa kuelewa dhana nzima ya uandishi wa makala hii. Unapozungumzia utofauti wa mishahara ya wachezaji ni suala ambalo lipo duniani kote. Ukubwa au udogo wa mshahara hutegemea makubaliano mara baada ya mazungumzo ya mwajiri na mwajiriwa. Tusianze kuwachonganisha waajiri na watumishi wao wakati hivyo ndivyo walivyokubaliana. Tusigeuze suala la kucheleweshwa kulipwa kwa stahili za watumishi kuwa suala la udogo na ukubwa wa mishahara kwa kigezo cha ugeni na uzawa. Hata mzawa anaweza kulipwa pesa nyingi tu kama akitambua thaman yake na kuwa na msimamo pindi anapojadili mkataba wake.Ni kweli viongozi wa Yanga wanapaswa kufanya jitihada za kulipa stahili kulingana na makubaliano lakini tusiingize agenda za kugawa wachezaji kwa kigezo cha ukubwa na udogo wa mishahara.
ReplyDeleteHuyu jamaa hajui kabisa kuandika makala, mara nyingi hutoa hoja zake kwa kusikia , kuona mitandaoni lakini hafanyi ground work kupata sources za kueleka kuhusu anachokiandika. Achilia mbali kwanza uandishi wake hauna mvuto...
DeleteIlitakiwa kaka Saleh ukiandika wachezaji wa KIGENI WANAPEWA NYUMBA NZURI basi moja ya hizo picha ungeweka picha labda ya nyumba ya Molinga, halafu ukalinganisha na nyumba ya Ngassa. Na mifano mingine ya namna hiyo.
Watanzania ni watu wa kujipongeza kinafiki. Waache wachezaji wa kigeni walipwe zaidi ya wazawa kwani tusiwe wanafiki bali ukweli ni kwamba wachezaji wetu wazawa bado kabisa hawajajitambua tuwache kuwapongeza na kuwajaza viburi kuwa wapo zaidi ya wageni ni unafiki mtupu.Ni juzi tu imemalizika challenge cup kule Uganda Tanzania, unguja na bara tumeshindwa kuingia tatu bora kwenye ukanda dhaifu kabisa baani Africa.Halafu mtu bila aibu anathubutu kusema kuwa wachezaji wetu wapo juu kuliko kenya au Uganda?Kama wanadai haki zao ni wajibu kwa waajiri wao kuwalipa na ikiwezekana kwa wakati lakini tusianze kuleta fitina ya kusema wageni wanasthaaminiwa zaidi kuliko wageni huko ni kuanza kuotesha miche ya ubaguzi kwa wageni hata ulaya kasumba kama hizi ndizo zilizopelekea ubaguzi wa rangi kushamiri.Na sidhani kama timu zetu zinasjili wageni kwa kupenda? Sidhani kama kutakuwa na wazawa wenye uwezo zaidi ya wageni halafu wakanyanyasika na timu za bongo na ukiona bado wapo katika hali hiyo ujuwe hawjawa tayari kujikomboa sio kimajungu bali kiuwezo wa kazi yao.kitu kingine wachezaji wetu wazawa tunapokuja mechi za kimataifa iwe kwa vilabu au timu ya Taifa huwa wa hovyo kabisa sijui tatizo kitu gani. Mechi hizi za kimataifa ndizo zinazowaumisha vichwa viongozi wa vilabu vyetu na kupelekea kushawishika kusaini na kuwaamin wageni kutokana na hofu ya wachezaji wazawa kufulia kwenye mechi za kimataifa.Ukweli ni kwamba wachezaji wetu wazawa bado wanahofu na mechi za kimataifa kitu ambacho ndicho kinawafanya wachezaji wengi kushindwa kujiexpose au kujitangaza ili kupata vilabu vyenye maslahi bora zaidi kwa hivyo tuwache kuwajaza majungu ya kifitina na roho mbaya bali tuwaambie ukweli haki zao sawa bali wajitume nakuwa na uwezo zaidi ya wageni waone kama watanyanayasika. Samata aligoma Simba wakamtimizia matakwa yake na alipopewa nafasi akajipa nafasi zaidi kusonga mbele leo hii yupo Dunia nyengine.
ReplyDeleteAnasahau kila masika na mbu wake.Mbona hajazungumzia kipindi kile wakati Ngassa alipokuwa mfalme Yanga na kulipwa mshahara mkubwa kuzidi wachezaji wenzake?Mbona hajazungumzia kipindi kile Ngassa alipokuwa anaamua kufanya alilotaka kisa tu alikuwa kwenye peak na kuwashika Yanga kila mahali?Jinsi anavyojisika yeye sasa ndivyo jinsi walivyokuwa wanajisikia wenzake waliokuwa wanaonekana wa kawaida tu klabuni.Akumbukuke kuna kipindi ilifikia hatua Ngassa alikuwa anaenda mazoezini muda na siku alizotaka kufikia hatua hata kocha Mkwasa alichoshwa na tabia zake.
ReplyDeleteUshauri wangu kwa Saleh ni kwamba asiwatie ujinga wachezaji wazawa bali alipaswa kuwapa mbinu na hamasa za kuwa juu kuwazidi wachezaji wa kigeni ili kujijengea heshima na ufalme katika vilabu vyao.Tatizo ninaloliona kwa wachezaji wetu ni ile hali ya kukubali kuwa wao hawana uwezo kuliko wachezaji wa kigeni matokeo yake wameshakuwa brain washed kuwa wageni ni bora zaidi yao.Tukumbuke hili halipo kwa wachezaji hata maofisini hali ni hiyo hiyo lakini kwa wenye kujitambua wanaonesha ubora wao na kupata wanachostahili
Kifupi anapaswa mumjue Saleh Ally waulizeni watu waliofanya nae kazi Saleh naamini ni mwandishi mzuri ila ana kasoro nyingi za kibinadamu 'na utendaji wake wa kazi,ni mpenda kujivuna anaona waandishi wote hawajui zaidi yake ana tabia ya uandishi wa mipasho ni mtu anayetumika au anayependa sifa zaidi ktk hili hafanani waandishi na wachambuzi makini kinachombeba ni ukubwa wa kampuni ya udaku,kuhusu Ngassa n tone tu angalieni alivyokuwa akimpa nafasi mzee Akilimali ikiwa hakuwa na cheo chochote mbona alikuwa hampi nafasi Kilomoni kumzungumizia
ReplyDelete