Na Saleh Ally
WAPENDA mpira ni wasahaulifu sana, huenda ni kutokana na mambo mengi yanayotokea kwa muda mfupi.
Kawaida michezo inakwenda haraka sana na mambo yanajitokeza mfululizo. Hivyo inasababisha watu kutupia akili zao kwa muda mwingi sehemu hiyo.
Mfano, timu sasa zinacheza mechi za Kombe la Shirikisho. Wakati huohuo gumzo la usajili ikiwa ni siku chache baada ya Simba kumaliza kutengeneza na kuzindua viwanja vyake vya mazoezi.
Kumbuka wakati huohuo, wachezaji wa kimataifa kadhaa wa Yanga waliamua kujiondoa na kuzua gumzo kubwa, Yanga wakaanza kusajili na kampeni kadhaa za kuwasaulisha mashabiki wao ikiwemo ile kampeni ya “kuwapoza” kwamba huenda wakamalizana na Kocha Patrick Aussems ambaye aliinoa Simba.
Mambo yanakwenda kwa kasi sana na ni mengi kwa kweli, hii inaweza kuchangia kuwasahaulisha mambo mengi kama ambavyo nimesema.
Ninachokilenga kuwakumbusha ni baada ya kuona mashabiki wa Yanga wakiwa na furaha kweli wakati timu yao ikisajili mfululizo wakati wa dirisha dogo la usajili ambalo sasa liko wazi.
Yanga inasajili wachezaji mfululizo, mfano tumeona Ditram Nchimbi kutoka Polisi Tanzania, imemrejesha Haruna Niyonzima kutoka AS Kigali ya Rwanda, imemsajili Adeyum Saleh kutoka JKT Tanzania.
Bado inaendelea na usajili kwa ajili ya kikosi chake. Iko tayari kuendelea kupata wachezaji wapya na maana yake huenda wanaweza kufikia watano kwa ajili ya dirisha hilo.
Kama unakumbuka walioondoka kama Sadney Urikhob na Juma Balinya pia walikuwa gumzo wakati Yanga wakifanya usajili kama huo.
Leo wameondoka wakiwa hawajaonyesha lolote na imeonekana kama kila upande una tatizo, uongozi ukisema hawakufanya vizuri, nao wakisema hawakuwa wakilipwa na kupata stahiki zao.
Wakati wanaondoka hao, Yanga tayari walimtimua Kocha Mwinyi Zahera kwa madai kuwa alishindwa kuonyesha kiwango bora lakini baadaye wachezaji wakadai hawakuwa wakilipwa mishahara na hili linaonekana lilichangia.
Maana yake, bado kuna tatizo ndani. Wakati linapatiwa ufumbuzi, Yanga wanarudia kufanya usajili mpana kwa muda mfupi. Hii maana yake wataingiza presha ndani ya kikosi na wachezaji wanaokuja wengi hawajazoeana vizuri na wenzao, watahitaji muda, wasipowavumilia watawapa presha na ‘stress’, mwisho wataonekana hawakuweza kufanya vizuri.
Niyonzima ni fundi hasa lakini anakutana na Yanga si ile. Atahitaji angalau muda kidogo hata kama atafanya vizuri katika mechi ya kwanza. Hali kadhalika kwa Nchimbi lakini pia Adeyum.
Angalia, hata Simba walifanya kosa kama hili. Wachezaji waliochangia kikosi chao kusimama kama Emmanuel Okwi na James Kotei walikubali waondoke. Wakasajili Wabrazili watatu ambao wanaanza kuonyesha kiwango chao taratibu.
Unaona Simba nao walikuwa na usajili mpana kwa kuwa pamoja na Wabrazili watatu, waliwasajili Sharaf Eldin Shiboub kutoka Sudan, wakamsajili Francis Kahata kutoka Kenya. Wachezaji watano wa kigeni kwa wakati mmoja, hii nao imewasumbua na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko ya kiwango.
Kawaida wachezaji wanahitaji mambo mengi katika ikosi kipya ili kuanza kuonyesha kiwango. Moja wapo ni kuzoea mifumo ya kikosi, mahitaji ya kocha, aina ya uchezaji, wachezaji anaocheza nao na ikiwezekana aina ya timu anazokutana nazo ambazo ndizo zinajenga aina ya ligi anayocheza.
Wachezaji wamefanikiwa kuanza na kwenda vizuri. Hawa ni aina ya wachezaji wachache ambao huzoea maeneo mapya kwa wepesi na wamekuwa wa aina hiyo sawa na Meddie Kagere wa Simba ambaye hata alipotoka Polisi Rwanda kwenda Gor Mahia ya Kenya alifanya hivyo, baadaye alipotua Simba, mambo yamekwenda hivyo, pia.
Wachezaji hao wataanza kuonekana taratibu kama ambavyo tumeona. Ndiyo maana unaona Simba wamelishitukia hili na katika dirisha dogo wamekaa kimya na taarifa zikieleza wanamtaka fowadi mmoja tu ili wasonge.
Kuna haja ya viongozi kuwa makini wakati wa usajili wakiangalia mambo muhimu na kujali masuala ya ufundi badala ya siasa za kuwafurahisha mashabiki kuwataka wajisikie vizuri.
Viongozi waangalie ABC za soka zinasemaje na si kuangalia kwa kuwa kuna uwezo wa fedha, basi kifanyike kila kitu ili mradi mashabiki nao watafurahi sana!
0 COMMENTS:
Post a Comment